Habari za Punde

Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya wa Wastaaf na Wazee Zanzibar Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka jamii kuzingatia umuhimu wa kuwaheshuimu na kuwatendea wema wazee, kwa kutambuwa kuwa ni misingi muhimu ya silka, malezi na utamaduni wa Wazanzibari.

Dk. Shein amesema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wazee na Wastaafu Zanzibar (JUWAZA), uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdul wakil, Kikwajuni mjini hapa.

Amesema jamii imekumbwa na vitendo vya udhalilishaji na  unyanyapaa dhidi ya wazee, huku kukiwa na watu ndani ya familia wanaowadharau wazee wao kwa kuwatukana pamoja na kuwahusisha na imani za  kuwashirikina  na dhana za kuhusika na vitendo viovu, ikiwemo uchawi na wanga.

Alisema kuna baadhi ha vijana mbali na kusomeshwa vyema na wazee wao, wamekuwa wakiwadharau wazee kwa kigezo kuwa hawaendani na hadhi walizonazo, mambo yanayochangia na kuwafanya wazee kukosa amani, matunzo, misaada na haki wanazostahiki.

“Haki ya kuheshimiwa na kutunzwa ni ya msingi kwa kila mzee, vijana wana wajibu wa kuwapa wazee wao haki zao kwani huo ni wajibu wao”, alisema.

Aliitaka jamii kuendelea kuwaheshimu wazee kutokana na mambo mbali mbali makubwa waliyolifanyia Taifa na kusisistiza haja ya kuendelea  kuwatunza an kuwaenzi ili kupata fursa ya kuchota hekima na busara kutoka kwao.

Alisema nchi zote zinazoendelea zimekuwa na utamaduni wa kuwaenzi na kuwathamni wazee na wastaafu na kuwatumia ipasavyo, hususan pale kunapohitajika ushauri wa mambo mbali mbali, kutokana ana maarifa, hekima na uzoefu wao katika masuala ya kimaisha.

Aidha, alisema ni muhimu kuzingatia suala la kuwatunza wazee kuwa limetiliwa mkazo katika mafunzo ya Dini zote, ikiwa ni hatua maalum katika kuwatendea wema.

Dk. Shein alisema katika kudhihirisha dhamira njema ya Serikali katika kuyashughulikia masuala ya wazee, mara baada ya Mapinduzi matukufu ya 1964, Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume alianzisha ujenzi wa nyumba za wazee kwa lengo la kuwahifadhi, hususan wale waliokosa uwezo na watu wa kuwahudumia.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiendeleza utaratibu wa kuwapa hifadhi na kushughulikia changamoto mbali mbali zinazowakabili wazee, kwa kutambuwa kuwa huo ni wajibu wake wa msingi.

“Lazima tuwathamini wazee wetu, tuwaheshimu na tuwahifadhi kwa kusikiliza shida zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kadri ya uwezo wetu”, alisema Dk Shein.

Aidha, alibainisha kuwa wajibu wa kuyashughulikia masuala yanayowahusu waze ni hatua ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa 2015 – 2020, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 135,

Dk. Shein alieleza taarifa ya  Idadi ya watu na iliofanyiika mwaka 2012 imebainishwa kuwepo zaidi ya wazee 53, 311 wenye umri wa kuanziza miaka 60, hatua iliyoifanya Serikali kuanzisha Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, wazee, wanawake na watoto baada ya kutambua thamani yao..
Aidha, alisema Serikali ilianzisha Sera ya Hifadhi ya Jamii mnamo mwaka 2014, kwa lengo la kusimamaia wazee wote nchini, ikiwemo wenye umri wa kuanzia miaka 70 na kuendelea na kuwapatia posho la shilingi 20,000 kila mwezi.

“Serikali itaendelea kuyaimarisha makaazi yao na kuhakikisha kuwa wazee hao wanapewa huduma zote muhimu wanazostahili, zikiwemo za chakula, matibabu, maji safi na salama pamoja na ulinzi wa maisha yao”, alisema.

Dk. Shein aliweka wazi malengo ya serikali ya kuwapatia wazee hao mazingira bora zaidi ya kuishi ikiwa pamoja an kuwaandalia ziara za kuzitemebelea sehemu mbali mbali za kihistoria na za maendeleo.

Alisema amefurahishwa sana mafanikio makubwa yaliopatikana kupitia JUWAZA kutokana na kazi kubwa ya kuwaunganissha wazee kwa lengo la kuimarisha hali zao kiafya, kiuchumi na ustawi bora wa maisha yao.

Akigusia maomba mbali mbali yaliowasilishwa kwake, Dk. Shein alisema Serikali inalifanyia kazi ombi la kuongeza kiwango cha posho ya Pensheni  jamii na kuahidi kulitolea uamuzi kutegemea na wakati husika.

Sambamba na hilo, Dk. Shein alisema ni jambo zuri kuwepo kwa sheria, itakayozingatia mambo mbali mbali ya wazee, huku akionyesha imani kubwa aliyonayo ya Rais ajaye kuendelea na ataratibu wa utoaji wa Pensheni jamii kwa kuzingatia kuwa atakuwa na uelewa mpana wa Ilani ya CCM.

Aidha, Dk. Shein alikubali kuwa mlezi wa Jumuiya ya Wazee na Wastaafu (JUWAZA) pamoja na kuunga mkono rai ya uanzishaji wa mfuko maaalum, ili kusaidia shughuli mbali mbali za kuendeleza Jumuiya hiyo.

Katika hatau nyengine, Dk. Shein alipokea Cheti cha Uongozi bora kutoka JUWAZA pamoja kupokea Kadi ya Uanachama wa Jumuiya hiyo.

Nae, Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na watoto Modline Castico, alisema kuwepo kwa mswada wa sheria kuhusiana na utoaji wa Pensheni jamii, umewafanya wazee kufurahia jambo hilo, kwa kuzingatia kuwa utawahakikishia ulinzi wa haki zao, sambamba na kuondokana na vitendo vya udhalilishaji.

Alisema Wizara hiyo itaendelea na juhudi zake za kupigania  na kuimarisha haki na ustawi bora wa maisha ya wazee nchini.

Mapema, akisoma Risala ya Jumuiya hiyo, Amour Haji Nassor aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha Posho la Pensheni jamii  kwa wastani wa asilimia hamsini ya kima cha chini cha mshahara, kabla ya kumaliza kwa awamu ya saba ya Uongozi.

Aidha, alipongeza juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kuwapatia wazee huduma mbali mbali za kijamii, ikiwemo suala la afya bora , akibainisha juhudi hizo zimefanikiwa kuimarisha hali zao.      

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.