Habari za Punde

Kukabidhiwa Jengo la Kihistoria la Bi. Hole Bungi Wilaya ya Kati Unguja.

Na Mwashungi Tahir     Maelezo       3-9-2019.
Waziri wa Habari  Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo amesema wananchi wa Zanzibar wanahitaji kujua mambo mengi ya kale ili waweza kujuwa historia ya nchi yao.
Hayo ameyasema huko Bungi Wilaya ya Kati wakati wa makabidhiano ya jengo la kihistoria la Bi hole baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa na Kampuni ya Ujenzi ya Azim.
Amesema hali ya jengo hilo hivi sasa lipo katika hali nzuri hivyo amewataka wananchi kujenga utamaduni wawe wa kutembelea sehemu za historia zikiwemo eneo la Bi Hole, Dunga, Mkandamume, Fukuchani na Mvuleni ili kuendeleza Utalii wa ndani.
Amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka Idara maalum inayoshughulika Mambo ya Kale ni moja ya njia ya kuwekeza na  kukuza uchumi hasa ukizingatiwa kwamba Zanzibar inautajiri mkubwa wa mambo ya kale .
 Aidha amesema sehemu hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo mkubwa ya wageni na wenyeji kutembelea na kutakuwa kuna mvuto kama Forodhani au hata Fumba  kutakuwa na sehemu nzuri ya kupumzikia  biashara  za vyakula zitakuwepo.
“Eneo hilo likikamilika linatarajiwa kuwa na mambo mengi yaliyo mazuri ikiwemo sehemu ya kupumzikia, biashara za vyakula ili kuweka mazingira mazuri  pahala hapo”, alisema Waziri Kombo.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Mambo ya Kale Khadija Bakari amesema Serikali inachukuwa juhudi kubwa kwa makusudi ili kuimarisha majengo ya mambo ya kale na kuwa vivutio vikubwa kwenye kukuza mambo ya Utalii.
Hivyo amewaomba watakaokuwa wanashughulikia jengo hilo kuhakikisha wanaweka ulinzi ulio imara ili jengo hilo lisichafuliwe na liweze kudumu kwa muda mrefu.
“Nawaomba walinzi kuwa imara na kuhakikisha jengo hili isiwe watu wanaingia na kutoka na  lisichafuliwe kwa makusudi ili liendelee kupendeza pia  liweze kufanya kazi kwa muda mrefu”,alisema Katibu huyo.
Vile vile Injinia wa kampuni ya AZIM Contract Mkurugenzi wa  Miradi Abdullah Omar amesema ujenzi huo umeanza mwaka mmoja uliopita  na mambo yote waliyokubaliyana kwenye mkataba umemalizika.
Mradi huo wa jengo la Bi Hole hadi  kukamilika kwake umegharimu zaidi ya  Milioni mia nane ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwekeza jengo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.