Habari za Punde

Viwanja vya ndege kukuza utalii Nyanda za Juu Kusini


Watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakiwa mbele ya banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini, ambayo yamezinduliwa leo na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Akson

Na Mwandishi Wetu
UBORESHAJI wa miundombinu ya viwanja vya ndege na barabara kwa Nyanda za Juu Kusini kutachangia kukuza utalii kutokana na kuwa na vivutio vingi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Akson alipozindua maonesho ya Karibu Utalii Kusini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo, ambapo yanashirikisha taasisi za umma na watu binafsi.
Hatahivyo, Dkt. Akson amesema tayari amepata taarifa kuwa kuna matengenezo makubwa ya kiwanja cha ndege cha Iringa, ili kiweze kuhudumia ndege kubwa zaidi ya Bombardier ambayo inabeba abiria 72.
“Nimesikia hapa mkuu wa mkoa amesema kiwanja chetu cha hapa Iringa kitafanyiwa upanuzi mkubwa wa barabara ya kutua na kuruka ndege, na pia viwanja vya mikoa ya Mbeya, Mpanda, Songea na Katavi vyote vitaboreshwa zaidi,” amesema Dkt. Akson.
Lakini, amewataka wakazi wa Nyanda za Juu Kusini kuwa wabunifu kwa kuvutia watalii kutembelea vivutio vilivyopo, ikiwemo milima mingi, Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Udzungwa, Katavi na Kitulo; Kimondo cha Mbozi, Maporomoko ya Maji ya Kalambo na Ziwa Ngosi.  
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ya kiwanja hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale amesema barabara ya kwenda kwenye Hifadhi ya Ruaha itaboreshwa,  pamoja na Kiwanja cha ndege cha Iringa nacho kipo kwenye mchakato wa maboresho hayo.
Katibu Kata ya Nduli mkoani Iringa, Wilbert Chale (kulia) akipata maelezo ya uboreshaji wa viwanja mbalimbali vya Ndege vilivyopo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kutoka kwa Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Bahati Mollel, alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini yaliyofunguliwa leo na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Akson yanayofanyika kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo.
Afisa Usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Miyaga Juma (kushoto) akisikiliza maswali ya Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga wa Mkoa wa Iringa, Rosalia Makwaya, alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ya Karibu Utalii Kusini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.