Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Shein Azungumza na Wazee wa Wilaya ya Chakechake Pemba leo.


Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wazee wa CCM Wilaya ya Chakechake katika ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi,akiwa Kisiwani Pemba kwa ziara. 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwatunza na kuwaenzi wazee.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta na Makonyo Wawi Mkoa wa Kusini Pemba wakati alipofanya mkutano na Wazee wa CCM wa Wilaya ya Chake Chake.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea kupatikana uhuru wa Tanganyika na uhuru wa Zanzibar kupitia vyama vya ASP na TANU.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee ndio walioijenga Zanzibar na kuleta ukombozi na kuwakomboa wanyonge.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wazee walioipigania Zanzibar na hadi hivi leo Zanzibar kuweza kupiga hatua na kupata maendeleo makubwa.
“Hapa tulipofika ni nguvu za Mwenyezi Mungu pamoja na Wazee wetu, hivyo pia, yunapongezana kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 -2020 kuna mengi tumeyafanya na sote tumeshiriki kikamilifu”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa na taarifa ya wazee hao waliyoisoma huku akieleza kuwa ahadi zote zilizoahidiwa na chama hicho zitatekelezwa hatua kwa hatua.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitumia wastani wa zaidi ya milioni 600 kwa mwezi kwa ajili ya kuwapa wazee pencheni jamii.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha wazee wote wanaorodheshwa kwa ajili ya kupata fedha hizo za pencheni jamii kwa kila mwezi mpaka wale wazee ambao hawana vyeti vya kuzaliwa.
Alisema kuwa si nchi nyingi duniani zilizo na mfumo huo wa kuwapa pencheni jamii wazee katika Ukanda wa Afrika Mashariki ni Zanzibar pekee yenye kufanya utaratibu huo na kusisitiza kuwa kima hicho kilichoanzwa cha elfu 20 si kidogo.
Dk. Shein alieleza namna Serikali ilivyoongeza fedha za Bajeti kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua dawa ambapo hivi sasa vituo vyote vya afya vya Zanzibar vimekuwa vikipata dawa kwa wakati huku akisisitiza kuwa endapo akisikia kuna kituo cha afya kinawauzia dawaa wananchi wahusika watashughulikiwa.
Alisema kuwa haiwezekani wananchi wakateseka kwa kukosa dawa na kueleza kuwa huduma za afya na elimu hapa Zanzibar zitaendelea kuwa bure na hakuona sababu ya kuanzishwa kwa Bima ya Afya hapa Zanzibar.
Aidha, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja ya kuwekwa mikakati maalum ya kushughulikia suala zima la unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa watoto wadogo.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa WanaCCM kujenga umoja miongoni mwao kwani umoja wao ndio nguvu zao huku akitumia fursa hiyo kueleza kuwa Chama hicho ni lazima kiulinde na kuutetea Muungano uliopo.
Alisisitiza haja ya kutumia busara ndani ya chama hicho sambamba na kuwatumia wazee katika kufanikisha masuala mbali mbali ndani ya chama hicho kwa maendeleo ya chama na maendeleo ya nchi kwa jumla.
Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ipo haja ya kupokea mawazo ya wazee  sambamba na kuwaheshimu na kuwalinda wazee kwani kuna kila sababu ya kufanya hivyo hasa ikizingatiwa historia ya wazee wa nchi hii.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisema kuwa hikma za kuwaenzi wazee zimeanza kabda ya Mapinduzi na hadi hivi leo hikma na busara hizo zinaendelea kutumika ikiwa ni pamoja na kuwatuza wazee wote wa Unguja na Pemba.
Naibu Mabodi alieleza kuwa ndani ya Chama hicho kuna Mabaraza ya Wazee ambayo yamekuwa yakisaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza majukumu ya wazee katika kufikia malengo waliyoyakusudia.
Alisema kuwa WanaCCM wana kazi kubwa ya kulinda utamaduni na silka katika kuilinda Zanzibar ili kuweza kupata mafanikio, uzalendo sambamba na kuiarisha na kuduisha amani na utulivu uliopo hapa nchini.
Alieleza namna ya kuwatumia kuwa kuwepo kwa wazee na kuwatumia wazee hao wamekuwa wakikwamaua changamotio kadhaa
Nao Wazee katika taarifa yao walimpongeza kwa kuwapatia wananchihuduma za kijamii yakiwemo aji safi na salama mjini na vijijini, afya na elimu bure sambamba na ujenzi wa majengo ya skuli za ghorofa kwa azma ya kuondosha changamoto zilizopo.
Walieleza mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Matawi, wanafunzi kuendelea kupata elimu bure, vifaa vya kusomea pamoja na ujenzi wa barabara.
Wazee hao walimpongeza Dk. Shein kwa kusimamia Ilani kwa kuanzisha utaratibu wa kuwatunza wawzee kwa kuwapatia elfu 20 kwa kila mwezi bila ya ubaguzi wowote na kueleza jinsi wanavyompongeza Rais Dk. Shein.
Katika taarifa yao hiyo wazee hao walieleza juhudi wanazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha wanaendelea kushikamana ili kuongeza ushindi wa chama chao.
Wazee hao pia, walieleza changamoto ya matumzi ya dawa za kulevya pamoja na unyanyasaji wa kijinsia ambao utatokana na matumizi wa dawa za kulevya jambo ambalo linaondosha silka za Kizanzibari.
Walisisitiza haja ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa yeyote atakaehusika kufanya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
Nao viongozi wa CCM Wilaya na Mkoa huo wa Kusini Pemba walimpogeza Dk. Shein kwa jinsi alivyoweza kuwahudumikia wananchi katika kuwatekelezea huduma za kijamii na kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. John Pombe Magufuli, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuahidi kushirikiana nae
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.