Habari za Punde

Mwakilishi jimbo la Jang'o'mbe azitembelea maskani jimboni


 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande (kushoto),akimkabidhi seti moja ya jezi Meneja wa timu ya mpira wa miguu ya Kidongo chekundu City ndugu Omar Shamna (kulia).
 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande (wa pili kutoka kulia), akikabidhi mabati saba kwa Katibu wa maskani ya Butihama ndugu  Ali Mabrouk Makashari (kushoto) katika ziara hiyo
 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande (kushoto) , akimkabidhi fedha taslimu shilingi 70,000 Mjumbe wa maskani ya Karume ndugu Ibarahimu Abass Faki kwa ajili ya matengenezo ya maskani hiyo.
-MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande (kushoto) ,akimkabidhi mabati saba ya kuezekea maskani ya Bora Imani iliyopo Urusi Jang'ombe ndugu Omar Said Salum 'Saa nane' (wa nne kutoka kulia).(PICHA NA IS-HAKA OMAR-ZNZ

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande, ametoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 1.5 kwa maskani nane za Chama Cha Mapinduzi zilizomo katika jimbo hilo.

Akizungumza katika mwendelezo wa ziara zake katika maskani mbali mbali za CCM jimboni humo, Mhe.Ramadhani alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo ni Mabati ya kuezekea nyumba, Jezi za mpira wa miguu na fedha taslimu ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizowaahidi wananchi katika kampeni za uchaguzi zilizopita.

Alisema kwamba wakati akiomba ridhaa ya wananchi katika jimbo hilo aliahidi kuzipatia vifaa hivyo maskani za Chama Cha Mapinduzi zilizokuwa na changamoto mbali mbali  zilizotakiwa kutatuliwa na viongozi wa Chama.

Alieleza kuwa katika uongozi wake ndani ya jimbo hilo ataendelea kuwa karibu na Wananchi wa makundi yote, bila kubagua rika zao kwani kila mmoja ana umuhimu wake katika maisha ya kisiasa.

Katika maelezo yake Mwakilishi huyo Mhe.Ramadhan, aliwambia viongozi na makada wa maskani hizo kuwa Chama Cha Mapinduzi kinawathamini kutokana na mchango wao wa kuimarisha taasisi hiyo Kisiasa na Kiuchumi.

Alitoa nasaha zake kwa  wanachama mbali mbali wa maskani hizo kubuni miradi  ya ujasiriamali ili Vijana,Wanawake na Wazee wapate sehemu mbadala ya kujiingizia kipato.

Katika ziara hiyo aliwakumbusha Wananchi hasa Wana CCM kuhakiki vitambulisho vyao vya mzanzibar mkaazi sambamba na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate uhalali kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi na kuhakikisha kinashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alieleza kwamba kutokana na kazi aliyopewa na Wananchi wa Jimbo hilo ametekeleza Ilani ya Chama kwa zaidi ya asilimia 70 na anaendelea kukamilisha ahadi zake ili ifika mwishoni mwa mwezi Desemba awe amemaliza utekelezaji wa ahadi zake.

"Nawashukru sana Viongozi wenzangu wa jimbo letu wakiwemo mbunge ,madiwani na viongozi wote wa Chama na Jumuiya zake kwa ushirikiano wenu, ulioteta tija kubwa kwa wananchi wetu wote.

Naye Diwani wa wadi ya Kwaalinatu Mhe.Fatma Suleiman Juma, aliwataka wananchi kuendelea kujali na kuitunza  miradi ya maendeleo inayotekelezwa na viongozi wa CCM ili idumu kwa muda mrefu kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Diwani wa wadi ya Urusi Mhe.Ibrahimu Abass Faki, alisema kwamba jimbo hilo limeendelea kuimarika kimaendeleo kutokana na ushirikiano wa viongozi wake katika kutekeleza Ilani ya CCM.

Akizungumza Katibu wa Siasa na Uenezi wa Jimbo hilo Ali Hamad Ibrahim, alisema ziara hiyo imeongeza hamasa kubwa wa wana maskani hao kwani changamoto zao za muda mrefu zimetafutiwa ufumbuzi na kudumu na mwakilishi huyo.

Aliongeza kuwa kila mwanachama na viongozi wa CCM ndani ya jimbo hilo anatakiwa kuandaa vizuri zana zake za mapambano ya vita ya kisiasa kuelekea 2020,kwani muda kusema kwa maneno umepita na kilichobaki ni kutekeleza kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.