Na.Is-haka Omar - Zanzibar.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku kumi (10) katika Mikoa Sita kichama visiwani Zanzibar kuanzia Novemba 26 hadi Disemba 4 mwaka 2019.
Dkt.Bashiru anafanya ziara hiyo kwa mara ya pili tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.
Akitoa taarifa ya ziara hiyo ya Katibu Mkuu huyo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema CCM Zanzibar tayari kimekamilisha maandalizi yote ya mapokezi ya kiongozi huyo.
Catherine alisema katika ziara yake hiyo pamoja na mambo mengine anatarajia kuzungumza na viongozi mbalimbali wa CCM na jumuiya zake na kuzindua miradi mbali mbali ya kijamii na Chama kwa ujumla.
Alisema ziara hiyo ya Dkt.Bashiru itakuwa ni ya kikazi hivyo atatembelea maeneo mbali mbali nchini na kutoa maelekezo mbali mbali ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi. “Natoa wito kwa Viongozi,Watendaji na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kujiandaa vizuri katika maeneo yao ambayo Katibu Mkuu wetu Dkt.Bashiru atatembelea”, alisema Catherine.
Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine alisema Novemba 25 Dkt.Bashiru atapokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar (AAKIA),Novemba 26 hadi Disemba 1 mwaka huu atatembelea na kufanya ziara katika Mikoa Minne ya CCM kwa upande wa Unguja.
Katika maelezo yake Catherine, alisema Katibu Mkuu huyo baada ya kukamilisha ziara yake Unguja, Disemba 2 hadi Disemba 4 ataendelea na ziara yake katika Mikoa Miwili ya Pemba na kuhitimisha ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment