MAKAMO
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuridhishwa na kasi kubwa
inayoendelea ya ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni.
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Wazee wa Wilaya ya Kaskazini “A” huko
katika ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini “A”, na Ofisi ya
CCM Wilaya ya Kaskazini “B” iliyopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliwaleza wazee hao wa
CCM pamoja na viongozi wengine wa chama hicho waliohudhuria katika mkutano huo
kuwa kutokana na kasi hiyo kubwa ya ujenzi wa barabara hiyo yenye Kilomita za
mraba 31 anamatarajio makubwa ya kuzinduliwa barabara hiyo katika sherehe za
Mapinduzi zijazo.
Rais Dk. Shein alieleza na kushangazwa na kasi kubwa inayochukuliwa
na mkandarasi wa barabara hiyo na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaendelea kuwasogezea huduma muhimu za kimaendeleo wananchi wake wote
wa mjini na vijijini kwani hilo ndio lengo la Mapinduzi matukufu ya Januari 12,
1964.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja kwa
wazee kuwaeleza vijana juu ya heshima ya wazee na vipi wazee wanatakiwa
kuenziwa na kutunzwa sambamba na kupema heshima yao kutokana na mambo makubwa
waliyoyafanya.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea
kupatikana uhuru.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM
pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho, Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee
ndio walioleta ukombozi na kuwakomboa wanyonge wa nchi hii hivyo ni vyema
wakaendelea kuthaminiwa.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa na taarifa ya wazee
hao wa Kaskazini “A” na kuahidi kuwa ahadi zote alizoziahidi katika Wilaya hiyo
atazitekeleza na kuzifanyia kazi kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi.
Rais Dk. Shein alieleza haja kwa wazee kuwaeleza vijana na
kuwafahamisha historia ya chama hicho pamoja na kuyarekebisha mambo ambayo
yanaondoa mila, silka na desturi katika jamii.
Alieleza haja ya vijana kukumbushwa juu ya ukombozi wa
Zanzibar ili wajue kwamba kazi hiyo imefanywa na wazee tokea kuanzishwa kwa ASP
hadi Mapinduzi yaliyoongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Alieleza kwamba sio mambo yote yameandikwa katika vitabu
lakini hata hivyo hakuna kitabu kizuri kama mzee huku akisisitiza kwamba hakuna
chama kilichoikomboa Zanzibar isipokuwa ni chama cha ASP.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya
ukombozi wa Zanzibar na jinsi wazee walivyoshiriki kikamilifu katika
kuhakikisha uhuru kamili unapatikana chini ya chama cha ASP.
Alisisitiza haja ya kuijua na kuifahamu historia ya
Zanzibar hatua ambayo alisema ndio iliyomsukuma kuanza kuzungumza na wazee
kwani wao wana historia kubwa hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio waanzilishi wa vyama
vya ukombozi vya ASP na TANU.
Alieleza kuwa ushindi wa CCM katika chaguzi zake zote ni
jambo ambalo halina mbadala hivyo, aliwaeleza wazee hao pamoja na wanachama wa
CCM kuhakikisha wanaendelea kukiunga mkono chama hicho ili kiendelee kushika
hatamu.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi
alisisitiza kuwa CCM inathamani kuwepo kwa wazee na kueleza kuwa Serikali zote
mbili zimeeleza jinsi zitakavyowajali wazee.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar kwa niaba ya
wazee hao alimpongeza Rais Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kuwafuata wazee katika
Wilaya zao Unguja na Pemba.
Naibu Mabodi alieleza jinsi ya uwepo wa Mabaraza ya Wazee
katika ngazi zote huku akieleza jinsi ya juhudi za Rais za ushirikishwaji wa
Serikali na Chama pamoja na ushirikishwaji wa wananchi.
Nao Wazee wa Wilaya ya Kaskazini “A”, walimpongeza na
kumshukuru Rais Dk. Shein kwa uongozi wake uliotukuka na jinsi anavyoendesha
Serikali kwani wamepata matumaini na wameridhika sana na jitihada zake za utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 kwa vitendo.
Wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa ujenzi wa
barabara mbali mbali ndani ya Zanzibar hususan katika Wilaya ya Kaskazini “A” na
kuzitaja barabara zenyewe kwua ni barabara ya Kwanyanya hadi Mkokotoni, Matemwe,
Kijini, Muyuni hadi Nungwi na Mkwajuni, Kiongele hadi Pale.
Kwa upande wa sekta ya afya wazee hao walipongeza Makamo
Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar kwa kuipandisha hadhi Hospitali ya Kivunge kuwa
Hospitali ya Wilaya pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mbuyumaji.
Wakieleza kuhusu sekta ya elimu wazee hao walitoa pongezi
kwa Makamo Mwenyekiti hyo wa CCM Zanzibar kwa kujengewa Skuli ya Mlilile pamoja
na Skuli ya Mbuyumaji zote zilizomo katika Wilaya yao.
Katika risala yao hiyo, Wazee hao waliahidi kuendelea
kukitumikia chama hicho kwa gharama yoyote ile pamoja na kuyaenzi na kuyalinda
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Pamoja na hayo, wazee hao wa Wilaya ya Kaskazini “A”
walimpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuendeleza kasi kubwa ya maendleo ya
kuijenga Tanzania na kumuomba azidi kuudumisha Muungano ambao sasa umetimiza
miaka 55 tangu kuasisiwa kwake.
Waliongeza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa
yaliopatikana katika Wilaya yao kutokana na Utekelezaji huo wa Ilani ya Uchagizi
ya CCM ni pamoja na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji safi na salama Chaani
Masingini, maji safi na salama katika vijiji vya Mbuyumaji na Mlilile.
Aidha, mafanikio mengine ni mradi Mkubwa wa umeme wa
Kijini, Mbuyutende, Mbuyumaji na Mlilile pamoja na kuwapatia Pencheni jamii
Wazee wapatao 4,161 wenye umri wa miaka 70 katika Wilaya yab Kaskazini A.
Wazee hao pia, walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendeleza
kwuapatia Pencheni Wastaafu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na
Wastaafu wa kiwanda cha Sukari Mahonda.
Kwa upande wa TASAF Wazee hao walieleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inawapatia Kaya Masikini 4227 jumla ya TZS milioni
147.548,000 kila baada ya miezi miwili wananufaika na fedha hizo.
Nao wazee wa CCM wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja
walieleza kuwa wanashuhudia mafanikio ya uongozi wa Rais Dk. Shein na
wanaridhika na huduma zote wanazozipata kutoka katika Serikali anayoiongoza.
Walieleza kuwamafanikio hayo wanayoyashuhudia ni katika
utekelezaji mahiri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo imeanisha pamoja
na mambo mengine yakiwemo upatikanaji wa huduma bora za maji safi na salama,
elimu, afya, kilimo, miundombinu, barabara kuu na barabara za ndani, huduma za
umeme pamoja na huduma nyengine za kijamii.
Walieleza kuwa katika Wilaya ya Kaskazini “B” wazee 1912
waliotimia umri wa miaka 70 wanapata Pencheni ya TZS 20,000 na kumpongeza sana
kwa uamuzi wake huo wa kijasiri na kiungwana.
Wazee wa Kaskazini “B” Unguja walimuahidi Makamo Mwenyekiti
huyo wa CCM ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao hasa kwa kuzingatia
kuwa ahadi zote zimeshakamilishwa sambamba na utekelezaji bora wa Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Aidha, wazee hao walieleza kuwa CCM bado ndio chama bora na
pekee chenye dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi wote pamoja na kuwaenzi
wazee na kuyalinda Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyowakomboa wanyonge.
Nao Wenyeviti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja walimpongeza
Rais Dk. Shein kwa kusimamia vyema madhumuni na malengo ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuendelea kukiimarisha chama hicho cha (CCM).
Pia, Mwenyekiti hao walieleza jinsi wananchi wa Wilaya ya
Kaskazini “A”, walivyofarajika kwa ujenzi alioufanya wa Tawi lililoanza
kujengwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume huko Mshezashauri pamoja na ujenzi
wa Maskani mbali mbali za CCM katika Wilaya hiyo.
Aidha, Wenyeviti hao walitumia fursa hiyo kwa kumpongeza
Rais Dk. Shein kwa kusimamia na kuuendeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
sambamba na kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa hapa nchini ambao umepelekea
kuwepo kwa maendeleo endelevu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment