Na MwandishiWetu
TAASISI zilizopo katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano zimetakiwa kupanga bajeti ya michezo katika bajeti zao za mwaka ili
kuhakikisha wanashiriki vizuri katika michezo, imeelezwa.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migire baada ya
kukabidhiwa vikombe vya ushindi wa Mashindano ya Mei Mosi 2019 kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Uchukuzi
Sports Klabu (USC), Hassan Hemed.
Akijibu changamoto zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Uchukuzi
Sports Club, Mbura Tenga, ambaye katika risala yake ya utangulizi alieleza
moja ya changamoto zinazowakabili ni kwa baadhi ya taasisi kushindwa kutenga fedha
kwa ajili ya michezo.
Tenga alisema kuwa hilo la kushindwa kutenga fedha linatokana na taasisi
hizo kutokuwa na bajeti kabisa ya michezo na wengi wa maofisa rasilimali watu wake
kutojua kabisa umuhimu wa michezo na kuona kama ni kupoteza muda na fedha tu.
Migire alisema kuwa taasisi nazo zinatakiwa kuiweka michezo
katika bajeti za idara zao za kila mwaka ili kuhakikisha wachezaji wao wanashiriki
na kutoa wachezaji katika Uchukuzi Sports
Club.
Migire pia aliipongeza Uchukuzi Sport Klabu kwa kutwaa ubingwa wa jumla kwa mara ya pili
mfululizo katika Mashindano ya Mei Mosi,
baada ya mwaka
huu kutwaa jumla ya vikombe tisa, vinne vikiwa
katika nafasi ya kwanza, ambavyo ni Kuvuta
Kamba kwa Wanaume na Wanawake na Baiskeli kwa Wanauame na Wanawake.
Uchukuzi Sports
Klabu katika Mashindano ya Mei Mosi mwaka huu yaliyofanyika Mbeya, walitwaa vikombe tisa kati ya 14, ambavyo hushindaniwa kila mwaka.
Uchukuzi pia ndio
klabu pekee katika mashindano hayo kupeleka timu za michezo yote 14 ya mashindano
hayo, tofauti na wizara zingine, ambazo wakati mwingine hupeleka timu au
mchezaji mmoja.
Akijibu kuhusu timu ya Uchukuzi mara mbili kualikwa Zanzibar (Unguja na Pemba) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
ya Zanzibar (ZAA) na kufanya utalii wa ndani,
alisema hilo ni suala ni muhimu sana, hasa ukizingatia linahusu Muungano, ambapo liwataka kupanga utaratibu kuona USC
wanafanyaje ili kuwaalika Bara Wazanzibari.
Pia alisema changamoto ya kutokuwa na ofisi inayoikabili
USC linaweza kushughulikiwa, hasa ukizingatia kuwa Katiba ya USC inaeleza kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, lazima atoke wizarani, hivyo itakuwa rahisi kuwepo kwa ofisi wizarani
kwa ajili ya klabu yao.
Akielezea kuhusu ushindi huo wa jumla, alisema kuwa ni
mkubwa sana, hivyo hauwezi kupita kimyakimya,
kwani lazima na wakubwa nao wajue nini kimeletwa na USC, hivyo hafla hiyo itaandaliwa tena kwa ukubwa
wake.
Aidha, Tenga alisema
wanatarajia Februari 7, 2020 kufanya Mkutano mkuu kwa ajili ya mabadiliko ya Katiba
pamoja na kuchagua viongozi wapya, ambapo kila taasisi inakuwa na mwakilishi katika
klabu hiyo, tofauti na sasa ambapo taasisi moja inaweza kuwa na zaidi ya mjumbe
mmoja na nyingine isiwe nayo kabisa.
No comments:
Post a Comment