Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki akitazama bidhaa ya nyama
iliyochakatwa na kuwa soseji inayozalishwa na Kiwanda cha ORI Meat Product Ltd
kilichopo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho
leo Jumatano (Desemba 18, 2019) na kujionea uzalishaji. Kushoto ni Mfanyakazi
wa Kiwanda hicho, Martha Gwali.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kariuki akizungumza jambo na
Viongozi wa Kiwanda cha ORI Meta Product Ltd kinachochakata bidhaa ya nyama na
kuwa soseji wakati alipofanya ziara yake katika Kiwanda hicho leo Jumatano
(Desemba 18, 2019). Kushoto ni Meneja Uzalishaji wa Kiwanda hicho, Mitesh
Dhokie na katikati ni Mkurugenzi Mtendaji, Goodluck Hussein.
(PICHA
NA MAELEZO)
Na Mwandishi Wetu,MAELEZO DAR ES SALAAM 18.12.2019
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki amelipongeza Shirika la Utafiti wa Maendeleo
ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kuweka msukumo na mkakati endelevu wa kuwaendeleza
na kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji wadogo nchini.
Akizungumza na Uongozi na Wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchakata nyama cha ORI Meat
Product Ltd leo Jumatano (Desemba 18, 2019), Waziri Kairuki alisema TIRDO
imeendelea kutekeleza vyema majukumu kupitia shabaha iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika ujenzi wa
viwanda unaochochea katika kukuza
mnyororo wa thamani na kuleta tija
iliyokusudiwa.
Aliongeza kuwa msukumo
uliowekwa na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji) ni kuhakikisha kuwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo
wanakuwa na fursa kuwa katika kukuza uchumi kwa kuwawezesha kujenga viwanda
vidogo vidogo na kuchakata bidhaa zenye ubora.
‘’Niwapongeze TIRDO kwa
kutambua wajibu wenu katika masuala ya utafiti na viwanda lakini pia kutoa eneo
lenu lenye ukubwa square (mraba) mita 600-700
na ghorofa moja na kukodisha kwa kiwanda cha ORI na kwa msukumo huu tutaweza
kuwasaidia wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye viwanda vidogo kuweza
kufikia malengo yaliyokusudiwa’’ alisema Waziri Kairuki.
Aidha Waziri Kairuki aliitaka
TIRDO kuhakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu ili kuwafanya
wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali wadogo wanaendelea kupata maeneo
makubwa zaidi kupitia miradi yake hatua itakayowawezesha kuweza kuongeza
mnyororo wa thamani ya uzalishaji na hivyo kuleta tija kwa taifa.
Waziri Kairuki pia aliipongeza
Kampuni ya ORI Meat Product Ltd kutokana na juhudi na ubunifu mkubwa
walioufanya katika kuchakata bidhaa za nyama kupitia soseji za ng’ombe na kuku,
na kuongeza kuwa Ofisi yake itawasiliana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuona
namna bora mauzo na uzalishaji wa bidhaa za kampuni hiyo.
‘’Ndani ya muda mfupi wa
kipindi cha mwaka mmoja vijana hawa wa Kitanzania wameweza kuwekeza mtaji wa
Tsh Bilioni 1.1, walianza na wafanyakazi 50 lakini sasa wapo 64 lakini pia
wameweza kuongeza mnyororo wa thamani kupitia label (alama), vifungashio vya
plastiki, wazalishaji wa kuku ambapo wajasiriamali wanaweza kuuza kuku katika
kiwanda hiki’’ alisema Waziri Kairuki.
Akifafanua zaidi Waziri Kairuki
aliitaka Kampuni hiyo kuendelea kupanua shughuli zake ikiwemo kuimarisha
mtandao wa masoko ya ndani na nje ya nchi, ikiwemo soko la Nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na
kuzalisha bidhaa zenye viwango na ubora unaostahiki.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Humphery Ndossi Ofisi yake imeendelea kufanya kazi na
wawekezaji wa ndani kwa kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara zao, na
miongoni mwao ni Kiwanda cha ORI Meat ambapo wamekuwa wakitoa msaada mbalimbali
ikiwemo upimaji wa ubora wa bidhaa za kiwanda hicho.
Aliongeza kuwa TIRDO imeendelea
kusimamia wajibu wa msingi wa majukumu yake kwa kuwasisitiza wafanyabiashara
kuzingatia ubora wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ili kuweza
kuliepusha taifa na mlundikano wa bidhaa bandia na zisizo na ubora na kuzuia
matumizi yake ili kulinda afya za wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORI
Meat Product Ltd, Goodluck Hussein alisema Ofisi yake imeendelea kupata
ushirikiano mkubwa kutoka kwa Serikali na imeweza kuuza pakiti 1200-1500 kwa
mwaka, jambo ambalo lilikuwa gumu kwa miaka ya nyuma kutokana na uwepo wa
bidhaa nyingi za nyama kutoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment