Habari za Punde

LUKUVI AJA NA MUAROBAINI WA UCHELEWESHA UTOAJI HATI ZA ARDHI NCHINI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wataalamu wa sekta ya ardhi wakati akifungua mafunzo ya Utunzaji Kumbukumbu na ukusanyaji Maduhuli ya Serikali kupitia Kodi ya Pango la Ardhi jijini Dodoma leo tarehe 27 Januari 2020.Wataalamu hao wanatoka mikoa sita ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma na Morogoro.
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekuja na muarobani wa ucheleweshaji utoaji hati za ardhi kuagiza Karatasi na Majalada ya kutunzia kumbukumbu za ardhi sasa kuchapishwa Chuo cha Ardhi Tabora sambamba na idara za ardhi katika kila halmashauri kupatiwa vifaa  vitakavyowezesha uandaliwaji Hati za Ardhi.
Lukuvi alisema hayo leo tarehe 27 Januari 2020 wakati akifungua mafunzo ya Utunzaji Kumbukumbu na ukusanyaji Maduhuli ya Serikali kupitia Kodi ya Pango la Ardhi kwa Wataalamu wa sekta ya ardhi kutoka mikoa sita ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma na Morogoro yanayoendelea jijini Dodoma.
Alisema, pamoja na uchapishwaji Karatasi na Majalada ya utunzaji kumbukumbu za ardhi kuanzia bajeti ijayo ya Serikali hataki kusikia Afisa Ardhi kwenye halmashauri yoyote anatumia fedha zake za mfukoni kununua vifaa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
‘’Kuanzia sasa karatasi zote tutachepa wenyewe kwenye Chuo chetu cha Ardhi pale Tabora ili kuepuka ucheleweshaji uliokuwa ukijitokeza halafu nije kuona halmashauri inachelewesha hati kisa karatasi’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, katika halmashauri kuna wananchi wamekamilisha taratibu zote za kupatiwa hati za ardhi lakini wamekuwa wakicheleweshewa jambo linalosababisha wananchi kukosa hati kwa wakati na kuikosesha serikali mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.
‘’Tatizo Maafisa Ardhi badala ya kushughulikia Majalada ya ardhi wanataka mpaka wawaone Wamiliki wake, usipomuona Mpima au Afisa Mipango Miji basi unaweza kuambiwa eneo lako ni hatarishi au la makaburi, wanataka kula bila kunawa ’’ alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Lukuvi alisema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha wananchi hawasumbuki tena kufuatilia Hati ambapo kwa aliyekamilisha taratibu zote anatakiwa kuipata hati yake ndani ya mwezi mmoja bila gharama yoyote isipokuwa kodi zilizopangwa kwa mujibu wa sheria.
Alibainisha kuwa, mapema mwaka huu Wizara itaanzisha ofisi za ardhi za mikoa zitakazokuwa na wataalamu wa Upimaji, Mipango Miji, Wathamini na Usajili na mwananchi hawatakwenda umbali mrefu kuchukua hati na hakuna huduma ya ardhi itakayotolewa kwa kuvuka mkoa mmoja.
Pia Lukuvi amwataka maafisa ardhi kwenye Halmashauri nchini kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi wanalipa malimbikizo yao ya kodi ili kukusanya maduhuli ya serikali na kusisitiza utendaji kazi wa Maafisa hao sasa utapimwa pia kupitia makusanyo ya kodi kwenye maeneo yao.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, Wizara yake sasa imejipanga kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchi nzima na kutoa hati za kielektroni ambazo sasa zinatolewa katika halmashauri za Ubungo na Kinondoni na kubainisha kuwa ofisi zote za ardhi zitaunganishwa kwenye Kituo cha Taifa cha Utunzaji Kumbukumbu za ardhi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabuala kupitia mafunzo hayo yaliyoshirikisha wataalamu 106 alisema sekta ya ardhi imekuwa ikikabiliwa na changamoto kama vile ucheleweshaji utoaji hati za ardhi, utunzaji kumbukumbu za ardhi usiozingatia taratibu, kutoingizwa viwanja katika mfumo na ukusanyaji hafifu wa maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Alisema , hayo yote yanachangiwa na utendaji wa baadhi ya Maaafisa ardhi wasiokuwa waaminifu pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kutozipa kipaumbele idara za ardhi katika maeneo yao jambo linalosababisha watumishi wa sekta hiyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Naye Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wolter Lungu aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa makusanyo ya kodi ya pango la ardhi yamekuwa na chanagamoto mbalimbali kama vile miamala ya simu kugoma katika mfumo wa ukadiriaji kodi ya pango la ardhi , uhamishaji miliki za viwanja pamoja na utumiaji mfumo wa eneo lingine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.