Habari za Punde

Vijana wa Halaiki na Uhamasishaji Wajumuika Katika Chakula Maalum Waliyoandaliwa Katika Viwanja Vya Polisi Ziwani.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Katibu wa Kamati ya Uhamasishaji na Halaiki Zanzibar,Ndg Ali Mohammed Bakari, alipowasili katika Viwanja vya Polisi Ziwani Jijini Zanzibar kuhudhuria hafla ya Chakula Maalum alichowaandalia Vijana wa Halaiki wakati wa Maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameungana pamoja na Vijana wa Halaiki na wahamasishaji  walioshiriki katika maadhimisho ya sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika chakula maalum alichowaandalia.

Chakula hicho maalum cha mchana aliwaandalia  kinatokana na ushiriki wao kwenye sherehe hizo za miaka 56, zilizofanyika January, 12 mwaka huu katika Uwanja wa Amani,mjini Unguja.

Hafla  hiyo ilifanyika leo katika Viwanja vya Polisi Ziwani na kuhudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma.

Wengine ni pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na Washauri wa Rais wa Zanzibar.

Katika shukrani zake Rais Dk. Shein kwa vijana hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Issa Haji Ussi ‘Gavu’, alisema ana imani kubwa kuwa vijana hao watakuwa sehemu ya ulinzi wa Taifa hili kutokana na kujitowa kwao na uzalendo waliouonesha.

Alisema katika kipindi chote cha maandalizi ya sherehe hizo  vijana hao  walikuwa wakipokea vyema maelekezo wanayopewa na Viongozi wao  na kuyafanyia kazi kwa maslahi ya taifa.

Aliwatakiwa kheri na mafanikio katika masomo yao ili waweze kufaidika katika maisha yao na kulisaidia Taifa kupiga hatua za kimaendeleo. 

Aidha, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa uongozi wake madhubuti uliopelekea kuwepo kwa amani na utulivu, umoja  na mshikamano, na kusema  umesaidia sana kuharakisha maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.

Waziri Gavu aliwashukuru vijana hao kwa kufanikisha vyema sherehe hizo, huku akitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote waliohudhuria sherehe hizo zilizofana sana.

Nae, Katibu wa Halaiki na Uhamasishaji Ali Mohamed Baraka alitoa shukurani za dhati kwa Rias Dk. Shein kwa mwaliko huo na kutoa ahadi ya vijana hao kuendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha  vyema  shughuli  zinazoandaliwa.

Aidha, alimshukuru Rais Dk. Shein kwa kuwa karibu na vijana hao na kuonyesha imani upendo mkubwa kwao.

Hafla hiyo ilipambwa kwa matumbuizo kutoka  mashirikiano ya wasanii kutoka fani mbali mbali, ikiwemo taarabu asilia, Zenj Fleva, Muziki wa Dansi na ngoma za asili.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.