WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (katikati) akiangalia namna
vifaranga vya samaki aina ya Kambamiti vinavyozalishwa na Kampuni ya
Aphakrust alipofanya ziara kukagua uzalishaji wa kampuni hiyo kisiwani
Mafia. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Ganeshan Vedagiri na Kulia
ni Mkurugenzi Msaidizi Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi, James
Mganga. Picha na Mpiga Picha Wetu.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akivua samaki aina Kambamiti
alipotembelea mabwawa ya Kampuni ya Aphakrust kisiwani Mafia. Kwenda
kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Ganeshan Vedagiri na Mkurugenzi
Ukuzaji Viumbemaji, Dk. Nazael Madala na Mkurugenzi wa Uvuvi, Magese
Bulayi. Picha na Mpiga Picha Wetu.
Na.Mwandishi Wetu.- Mafia.
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda timu ya wataalamu kufanya
uhakiki wa takwimu, mauzo, uzalishaji na uendeshaji wa Kampuni ya
Alphakrust inayojishughulisha na uzalishaji wa samaki aina ya Kambamiti
pamoja na uhalali wa mapato ya Serikali kufuati kuwepo udanganyifu
kwenye biashara hiyo.
Kulingana na takwimu za mauzo ya Kambamiti
nje ya nchi kampuni hiyo ilipaswa kulipa shilingi milioni 300 kama
ushuru wa huduma kwa Halmashauri hiyo lakini imekuwa ikilipa shilingi
milioni 100 kwa mwaka na hivyo kuipunja Serikali kiasi cha shilingi
milioni 200 kila mwaka.
Waziri Mpina amebaini njama hiyo
inayofanywa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kushirikiana na Mwekezaji
wa Kampuni ya Alphakrust inayofuga samaki aina ya Kambamiti kisiwani
humo kwa lengo la kuiibia Serikali mapato yake yanayotakiwa kutozwa kama
ushuru wa huduma yaani ‘Service Levy’
Alisema Halmashauri ya
Mafia imetengeza makadirio ya kutoza ushuru wa huduma ya shilingi
milioni 9 kwa mwezi kutoka Kampuni ya Apha Krust na kuacha Kanuni
maalumu iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya ukokotoaji wa mapato
yanayopatikana ya kutakiwa kulipa asilimia 3 ya mapato yote
yanayopatikana kwenye biashara husika.
Udanganyifu huo
umebainika wakati wa ziara ya Waziri Mpina ya kukagua Kituo cha
kutotoleshea vifaranga na Shamba la ufugaji samaki aina ya Kambamiti
lilomilikiwa na Kampuni ya Alphakrust kisiwani Mafia.
Waziri
Mpina katika ziara hiyo aliambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani,
Ramadhani Maneno na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mafia
ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaib Nnunduma, Wakurugenzi na
Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mpina alihoji iweje
Halmashauri ya Mafia itoze ushuru kinyume cha Sheria wakati kanuni za
ukokotoaji wa mapato zinajulikana na hivyo kuamini kuwa huo ni mkakati
wa siri uliosukwa baina ya Halmashauri ya Mafia na Kampuni ya Apha Krust
kwa lengo la kukwepa kulipa mapato stahiki ya Serikali.
“Haiwezekani
Halmashauri ya Mafia ikaacha kufuata fumula ya uchukuaji wa ‘service
levy’ uliowekwa na Serikali na kutengeneza utaratibu wake
yenyewe..mwisho wa siku watu wa nje tunachoweza kukielewa ni njama
inayowekwa baina ya Halmashauri na Mwekezaji kuiibia Serikali” alisema
Mpina.
“Kwanini mkokotoo huo usizingatie sheria takwimu za
makusanyo zipo, bei inayotumika kuuza na masafirisho ya nje ipo kwanini
haikutumika kukokotoa..kwanini itumike fumula ya kukubalina nje ya
utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria”alihoji Waziri Mpina.
Waziri
Mpina alisema kama halmashauri inatoza fedha nyingi zaidi za ushuru wa
huduma tofauti na iliyowekwa kwenye Sheria ni makosa kwani Serikali
haiwezi ikatoza fedha ambazo haziko kwenye utaratibu wa sheria lakini
kama halmashauri inakusanya fedha kidogo kuliko sheria inavyosema nalo
ni kosa kwa mujibu wa sheria.
“Kwanini uchukue fedha kidogo
wakati fomula ya kupata makusanyo halisi kwa niaba ya wananchi
ipo..kwanini wewe utumie fumula ya kwako ya kubuni wewe wakati fumula ya
kisheria ipo”alihoji Waziri Mpina.
Mbali na dosari hizo za
ukwepaji kodi, Waziri Mpina alielezea kusikitishwa kwake na kitendo cha
mwekezaji huyo kushindwa kuwashirikisha wananchi wanaozunguka eneo hilo
kujifunza teknolojia hiyo ili kukuza sekta ya ukuzaji viumbe maji hasa
ufugaji wa Kambamiti.
Alisema Serikali haijapokea maombi yoyote
ya upungufu wa wataalamu wenye utaalamu na uzoefu maalum kuendesha mradi
kwani wataalamu hao wanazalishwa katika vyuo vyetu kikiwemo Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Vyuo vya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi
(FETA).
“Mradi huu unaendeshwa kwa usiri na wivu mkubwa kiasi
kwamba wananchi wa kawaida hawawezi kupata utaalamu kupitia mradi
huu..kwenye taarifa yenu sikuona mkichukua vijana wanaomaliza vyuo au
kuingia makubaliano na vyuo (MOU) kufanya mafunzo ya vitendo kwenye
mradi huu na kuwalipa kima cha chini cha mshahara”alihoji Waziri Mpina.
Alisema
wawekezaji kutoka nje wanapofika nchini wanalojukumu katika mikataba
yao ya kusambaza taaluma katika eneo lao la uwekezaji ili kuwawezesha
watanzania wengi kunufaika na uwekezaji wao na kueleza kusikitishwa
kwake na kampuni hiyo kuwabagua wazawa na kuwapa nafasi wageni hata
kwenye kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania.
“Toka
nimeanza kutembelea miradi hii kuanzia Dar es Salaam nimekuja kwenye
shamba la kambamiti na kituo cha kutotoleshea vifaranga mapokezi na
utolewaji wa maelezo na ufafanuzi unafanywa na wageni hii ni ishara
kwamba uongozi wote umeundwa na wageni au ni sehemu ya kuficha ukweli
juu ya undeshaji wa biashara hiyo’ alihoji Waziri Mpina
Mbali na
hilo Waziri Mpina alisema Serikali inazo taarifa za vijana wanaokwenda
kufanya kazi kwenye uwekezaji huo wanashindwa kufanya kazi kutokana na
ujira mdogo wanaolipwa na mwekezaji huyo na kuvunjika moyo na kisha
kuondoka.
“Kulipwa mshahara mdogo haijulikani wanalipwa hivyo ili
wakate tamaa waondoke na baadae itengeneze nafasi ya ajira kutoka nje
ya nchi au tatizo ni nini”alihoji Waziri Mpina.
Kwa upande wake
Meneja wa Alphakrust, Ganeshan Vedagiri amelalamikia kukosa wataalamu
wenye weledi na pindi watanzania wanapoajiriwa wanakaa muda mfupi na
kuondoka huku akilalamikia kudaiwa ushuru kwenye halmashauri zaidi ya
moja
Alisema mradi huo wa Mafia una mabwawa 31 ya Kambamiti
ambapo kwa mwaka huzalisha wastani wa tani 400 huku asilimia 90 ya
samaki hao wakiuzwa nchini ufaransa huku asilimia 10 zikiuzwa hapa
nchini.
Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia, Chuchu Silvery licha ya kuwepo
kwenye ziara hiyo hakuweza kuzungumzia chochote kuhusiana na dosari
hizo.
No comments:
Post a Comment