Habari za Punde

SERIKALI YAWATAKA WAAJIRI WA MAKOCHA KUTOKA NJE KUTOA TAARIFA ZAO TRA ILI WALIPE KODI


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma.

Na. Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imezitaka timu zote za mpira zinazoajiri makocha na wachezaji kutoka nje ya nchi kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya waajiriwa walionao wanaotakiwa kulipa kodi.

Hayo yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Nyongeza la Mbunge wa Chemba Mhe. Juma Selemani Nkamia, aliyetaka kujua Serikali inatambuaje Kocha au Mchezaji wa Nje aliyelipa na asiyelipa kodi kwa kuwa malipo yao hufanywa kiholela kwa kuwa hakuna mfumo rasmi.


“Kila mgeni akifikisha miezi 6 anahesabika ni mkazi (local resident) na anapaswa kulipa kodi, ni jukumu la mwajiri kutoa taarifa ya nani analipwa nini ili kodi zote stahili ziweze kulipwa kwa mujibu wa sheria”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa ulipaji wa kodi ya ajira ni kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 na ni jukumu la mwajiri kwenda kutoa taarifa kwenye Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ya waajiriwa walionao wanaotakiwa kulipa kodi hiyo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya Sh. milioni 1,733.6 zilikusanywa kama malipo ya kodi ya ajira kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.