Habari za Punde

Wahariri wa Vyombo vya Habari Waelezea Umuhimu wa Kutumia Kiswahili Sanifu Katika Uandishi wa Habari Zanzibar.

Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo akisisitiza jambo wakati akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusiana na Matumizi ya kiswahili sanifu katika Uandishi wa Habari hafla iliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Zanzibar.


Na Khadija Khamis – Maelezo  Zanzibar 06/07/2020.
Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mohamoud Thabit Kombo  amewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kuitumia lugha ya Kiswahili fasaha kwa lengo la kufahamika na jamii
Hayo aliyasema huko katika Ukumbi wa Wizara ya habari utalii na mambo ya kale Kikwajuni wakati wa Mkutano wa Wahariri wa Vyombo  vya Habari  vya Zanzibar .
Alisema utumiaji wa lugha ya  Kiswahili fasaha utasaidia muongozo mzuri wa kufahamika na jamii pamoja na kuilinda lugha ya Kiswahili isipotee.
Aidha alisema Wahariri, Waandishi wa Habari pamoja na Watangazaji  ni vyema kuisimamia lugha hiyo ili iweze kurekebisha mapungufu yanayojitokeza katika matamshi .
Alifahamisha kuwa katika kuikuza lugha ya Kiswahili sanifu ili itumike kama inavyohitajika Baraza la Kiswahili (BAKIZA) wameweza kusambaza makamusi katika vituo vya Habari nchini.
Waziri huyo alisema baada ya mafunzo hayo anatarajia mabadiliko makubwa katika utumiaji wa lugha ya Kiswahili fasaha kwa Watangazaji wa Vyombo vya Habari ikiwemo Radio  Televisheni pamoja na Magazeti
Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili (BAKIZA) Dkt Mwanahija Ali Juma alisema tafiti mbali mbali zimeshafanywa na baraza hilo na kuweza  kuona makosa ya Kiswahili sanifu yaliyofanyika katika  magazeti mbali mbali ikiwemo na gazeti la Serikali  la  Zanzibar leo.
Alisema kuwa wameweza kugundua makosa mengi yakiwemo udondoshaji  wa viambishi katika vichwa vya habari ,  vitenzi kudondosha wakati jambo ambalo linachangia mkanganyiko kwa msomaji wa gazeti hilo
Alisema kuna makosa ya kijumla kwa upande wa viambishi hata katika matini vipashio katika uwambishaji wa maneno,tahajia pamoja na utaratibu wa uundaji wa maneno .
Alielezea kuwa Kiswahili kimesanifiwa kuwa  lugha ya Kiswahili sanifu na lahaja zipo kwa lengo la  kuusaidia uhai wa lugha hiyo kwa kuengeza misamiati.
Akizungumzia kwa upande wa Radio jamii alisema Watangazaji hawajakatazwa kutumia lugha zao kupitia katika vituo vya jamii kwa lengo la mafahamiano ya lugha  na jamii  husika,  sio kwa radio za kitaifa ambazo zinawasikilizaji wengi.
Nae Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar  Omar Said Ameir  alisema katika kuimarisha na kujenga upendo na wahariri, watayarishaji vipindi pamoja na watangazaji wameandaa mashindano ya matumizi ya  lugha sahihi ya Kiswahili sanifu kwa vyombo mbali mbali vya habari, kukusanya vipindi vyao vilivyoanzia Januari mosi hadi Januari 31 mwaka 2020  vitakavyoshinda vitapatiwa  tunzo maalum  ya ushindi huo .
Mkutano wa siku moja wa  Wahariri wa  Vyombo mbali mbali umetayarishwa na  Idara ya Habari Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dk Juma Mohamed Salum akitoa hotuba ya Makaribisho katika Mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusiana na Matumizi ya kiswahili sanifu katika Uandishi wa Habari hafla iliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Zanzibar.
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar Mwanahija Ali Juma katikati akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yalioulizwa katika Mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusiana na Matumizi ya kiswahili sanifu katika Uandishi wa Habari hafla iliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.