Habari za Punde

Madereva wa Bajaji Mkoani Iringa Watajirika Kwa Udhamini wa Kampuni ya ASAS

Mlezi wa umoja wa Madereva wa Bajaji Mkoa wa Iringa Ndg. Ahamed Asas akizungumza na kuwapongeza Vijana wa Kikundi hicho cha (UMBI) kwa kujiajiri na kuaminika kutimiza ahadi zao pale wanaposaidiwa 

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
KAMPUNI ya Asas Group ya mjini Iringa imeudhamini Umoja wa Madereva Bajaj Iringa (UMBI) kupata mkopo wa zaidi ya Sh Milioni 650 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita-uliowawezesha kununua bajaj 97 zilizokopeshwa kwa mwanachama mmoja mmoja.

Kati ya bajaj hizo, bajaj 40 zenye thamani ya Sh 280 zilikabidhiwa juzi kwa wanufaika wa mkopo huo katika hafla iliyoongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela na mlezi wa umoja huo, Ahamed Asas.

Mwenyekiti wa UMBI, Noberth Sumka alisema kwa udhamini wa kampuni hiyo ya Asas umoja wao uliaminika na Finca Microfinance Bank na kwa nyakati tofauti kupata mikopo iliyowawezesha kufikia mafanikio hayo.

“Baada ya huko nyuma kutoa mikopo ya bajaj 57 kwa wanachama wetu, leo tena wanachama 40 ambao awali walikuwa madereva wa bajaj za watu wengine nao wananufaika na mkopo huu,” alisema.

Kwa kupitia umoja huo alisema, kila dereva aliyokopeshwa bajaj anatakiwa kufanya marejesho ya mkopo ambao thamani yake pamoja na riba ni takribani Sh Milioni 9 katika kipindi cha miezi 12 kuanzia sasa.

Kwa upande wake mlezi wa umoja huo, Ahamed Asas aliwapongeza Umbi akisema unaundwa na vijana wenye hali ya kujiajiri, wanaoaminika na kutimiza ahadi zao pale wanaposaidiwa.

“Bila uaminifu wao katika urejeshaji wa mikopo wanayopewa, umoja huu usingefikia hatua waliyofikia hivisasa. Ni vijana wenye dhamira ya dhati na wanapokusudia wanafanya,” alisema.

Katika kuwaongezea hali ya kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, mlezi huyo ameahidi kuchangia malipo ya leseni kwa madereva 100 wa umoja huo na kuwakatia bima ya afya ili iwe rahisi kwao kupata huduma za matibabu pale wanapohitaji.

“Gharama ya leseni ni Sh 70,000 kwahiyo mimi nitachangia Sh 50,000 kwa kila dereva na dereva atakayepata ofa yangu atalazimika kuchangia 20,000 ili aweze kupata leseni hiyo,” alisema.

Na kwa kupitia umoja huo, mlezi huyo ametoa Sh Milioni moja kukidhamini pia Chama cha Walemavu Iringa hatua iliyokiwezesha kukopeshwa bajaj moja.

Akikabidhi bajaj hizo, Waziri Lukuvi aliipongeza kampuni ya Asas kwa udhamini wake kwa madereva hao akisema hatua hiyo itawawezesha kujitegemea lakini pia kuendana na falsafa ya Rais Dk John Magufuli ya Hapa Kazi Tu.

“Yote haya yanafanyika na kufanikiwa kwasababu Rais Dk Magufuli ametengeza mazingira mazuri ya watu wa kipato cha chini kukopesheka na kufanya shughuli zao bila kubughuziwa,” Lukuvi alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwapongeza madereva hao na akawataka wazingatie sheria zote muhimu zikiwemo za barabarani wakati wakitumia vyombo hivyo.

“Msiwasilikilize wanasiasa, zingatieni sheria kama mnataka fursa hii mliyoaipata iwapeleke hatua ya mbele zaidi,” alisema.

Kasesela alisema mkoa wa Iringa unazo fursa nyingi katika sekta mbalimbali na kama vijana watakuwa tayari kuzitumia ipasavyo, zina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.