Habari za Punde

Masauni-Wahamiaji Haramu kusakwa Nyumba za Wageni,Mahotelini

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiongozana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwenda  kukagua maeneo mbalimbali yanayosemekana yanatumika kupitisha wahamiaji haramu,ambapo serikali imetangaza kuanza operesheni maalumu kudhibiti wahamiaji hao kipindi hiki nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu
Afisa Uhamiaji Mkoa Kigoma, Kamishna Msaidizi, Remigius Pesambili akisoma taarifa ya Utendaji kazi kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (hayupo pichani), wakati wa kikao cha ndani kilichohusiana na utendaji kazi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu
Serikali imetangaza kuanza operesheni, doria na misako  maalumu ya kuwasaka na kuwakamata wahamiaji haramu katika sehemu mbalimbali ikiwemo  katika  nyumba za kulala wageni, stesheni za mabasi, stesheni za reli, mahoteli, mialo ya uvuvi pamoja na maeneo yenye muingiliano wa shughuli za kibiashara hasa vijiji vinavyojishughulisha na shughuli za kilimo,makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, mkoani Kigoma baada ya kikao cha ndani na   Wakuu wa Vyombo vilivyopo chini ya wizara yake ikiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji, Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) na Idara ya Wakimbizi.
“Nchi yetu inaelekea katika Uchaguzi Mkuu,kama vyombo vya ulinzi na usalama lazima tutimize majukumu yetu na sasa tunaanza msako nchi nzima hasa katika mikoa iliyopo mipakani,tutaimarisha vizuizi vyetu vya barabarani nchi nzima,tutatoa elimu kwa wananchi wetu jinsi ya kuwatambua watu wasio raia ambao wameingia nchini bila kufuata utaratibu na kubwa zaidi tutafanya ukaguzi katika makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali” alisema Masauni
“kumekuwepo na wimbi kubwa la watu kuingia nchini bila kufuata utaratibu,sisi kama serikali hatukatazi mtu kuingia nchini basi wafuate utaratibu,kila mtu kwa kada yake anaetaka kuingia nchini kuna utaratibu wake wa kufuata na serikali haijawahi kumnyima raia yoyote yule wa kigeni fursa ya kuingia nchini.
Masauni pia aliwataka wananchi kutowahifadhi au kuwasafirisha  watu wasio raia kwani ni kinyume na sheria na adhabu yake ni kifungo cha muda wa miaka ishirini au faini ya milioni ishirini  au vyote kwa pamoja ikienda sambamba na kutaifishwa kwa chombo cha usafiri kilichohusika kuwasafirisha washtakiwa na kwa mwananchi atakaekutwa akimhifadhi au kumsafirisha mhamiaji haramu adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka mitatu na faini isiyozidi laki tano au vyote kwa pamoja.
Akizungumza katika kikao hicho Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma,Kamishna Msaidizi Remigius Pesambili alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba,2019 wamekamata wahamiaji haramu 3.992 na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria”
“Idara ya Uhamiaji hapa Kigoma kwa kushirikiana na vyombo vingine  vya Ulinzi na Usalama tumefanikiwa katika mwaka uliopita kuanzia Januari hadi Disemba kukamata wahamiaji haramu kama ifuatavyo; raia wa Burundi 3,293, Kongo 631, Kenya 12, Uganda 28, Rwanda 16, China 9, Somalia 2 na Msumbiji , ambapo jumla yake ni wahamiaji haramu 3,992 na tayari washachukuliwa hatua na wengine wako magerezani tayari wakitumikia adhabu” alisema DCI Pesambili
Aliongeza pia katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2019 raia wa kigeni 1,544 waliondoshwa nchini,815 walipewa amri ya kuondoka,534 walifikishwa mahakamani,231 waliachiwa huru baada ya kubainika kuwa hawana makosa ya kuwafikisha mahakamani na 868 walikabidhiwa Idara ya Wakimbizi.
Kuwepo kwa wahamiaji haramu nchini kunatajwa kushamiri sana katika mikoa iliyopo mipakani huku upatikanaji wa nyenzo za kutosha ikiwemo magari,elimu kwa wananchi juu ya kutoa taarifa za wahamiaji katika eneo lao,utoaji wa vitambulisho vya taifa uelekezewe nguvu hasa zaidi katika mikoa ya mipakani,vikao vya ujirani mwema baina ya Tanzania na nchi tunazopakana nazo na utolewaji wa vibali vya wakimbizi ikiwemo kufanyika upewaji wa uraia vikitajwa uenda vikawa suluhisho la kupunguza uhamiaji haramu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.