Habari za Punde

Abiria wanaotoka mikoa iliyoathirika kukaa Karantini Rukwa huku wananchi wakitakiwa kuvaa barakoa.


                 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. 

Katika harakati za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID – 19) Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa maelekezo kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanavaa barakoa wanapokuwa katika mikusanyiko pamoja na maeneo yao ya kibiashara hasa kwa wale wanaohusika na kutoa huduma kwa jamii huku akivitaka vyombo husika kuhakikisha abiria wote wanaotoka katika maeneo yaliyoathirika ndani ya nchi kuingia mkoa wa Rukwa washauriwe kujitenga kwa hiari kwa muda wa siku 14.

Mh. Wangabo amesema kuwa abiria hao wanaoingia ndani ya mkoa wanatakiwa kupimwa afya zao kwa kipima joto (Thermal Scanner) kwenye vituo vitatu vya mabasi mkoani humo ikiwemo Laela kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kituo cha mabasi Namanyere kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja na kituo kikuu cha mabasi Sumbawanga na kuongeza kuwa abiria hao wanatakiwa kuvaa Barakoa.

“Abiria wanaoingia Mkoa wa Rukwa kutoka kwenye maeneo yaliyoathirika wanashauriwa kujitenga wao wenyewe kwa hiari yao kwa muda wa siku kumi na nne (14). Endapo watahisi au kugundua kuwa wanaona dalili zozote za matatizoya kiafya watatakiwa kuripoti kwenye kituo chochote cha Afya cha karibu,” Alisema.

Aidha, Mh. Wangabo amewashauri wafanyabiashara wote ndani ya mkoa wenye tabia za kusafiri kwa nia ya kufuata mizigo ya kibiashara kuacha kufanya hivyo na badala yake wajenge tabia ya kuagiza bidhaa hizo kwa njia ya sim una kulipa kwa njia za mitandao ya simu ama benki inapobidi na pia kuwashauri wafanyabiashara wadogo kujiunga na kuagiza mzigo kwa pamoja ili kuwa na urahisi wa kupata usafiri wa pamoja.

“Watu wote wanaofanya kazi za kutoa huduma kwenye maduka, Maeneo yote ya kuuza vyakula, Saluni, Super Market, Wahudumu wa nyumba za kulala Wageni wanatakiwa kuvaa barakoa. Familia zinapotaka kufanya manunuzi ya jumla, inashauriwa aende mtu mmoja tu kutoka kila familia kufanya manunuzi hayo. Hata kwenda hospitali kuona wagonjwa aende mtu mmoja tu na mtu huyo asisahau kuvaa barakoa,” Alisisitiza.

Halikadhalika, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa minada yote na Magulio inadhibitiwa na kuendeshwa kulingana na maelekezo ya wataalamu wa afya na serikali kwa ujumla, na kubainisha kuwa serikali ya mkoa haitasita kusitisha mnada ama gulio endapo taratibu na maelekezo ya wataalamu ama ya serikali yatakiukwa.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa leo tarehe 20.4.2020 kwa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu hadi kufikia tarehe 20.4.2020 watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Corona nchini ni 257 ambapo kati ya hao mkoa wa Rukwa ina wagonjwa wawili (2)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.