Habari za Punde

Kinondoni Yapuliza Dawa Hoteli za Kitalii Kudhibiti Corona

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Abduli Hemed (mwenyekoti la bluu) akihakiki gari la zimamoto kabla ya kuanza kwa zoezi la umwagiliaji dawa katika hotel zakitalii eneo la Masaki.
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea kupambana vikali kuthibiti kuenea kwa virusi vya COVID 19 (Corona) kwa kupuliza dawa katika hotel za kitalii zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Hatua hiyo ni muendelezo wa mkakati uliowekwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Daniel Chongolo, Mkurugenzi Aron Kagurumjuli, Mstahiki Meya Benjamini Sitta, pamoja na Mganga Mkuu, Samweli Laizar kwa pamoja katika kuhakikisha kuwa  maambukizi ya  virusi hivyo hayasambai kwa wananchi na hivyo wanaendelea kuwa salama.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Kaimu Mganga Mkuu wa Kinondoni, Dkt. Said Hemed amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama katika kuepuka maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.
Amefafanua kuwa mbali na kuthibiti maambukizi ya virusi hivyo, lakini pia wanachukua tahadhari ya mlipuko wa homa ya dengu kwa kuwa hivi sasa ni kipindi cha mvua.
Ameongeza kuwa kupuliza dawa katika maeneo hayo ni mahususi kwa kuwa wageni wengi hufikia katika hoteli hizo na kwamba wataendelea kuthibiti kwenye maeneo mbalimbali  ili virusi hivyo visienee kwenye makazi ya wananchi.
“ Tunapopuliza hizi dawa ni kwa malengo mawili, kwanza tunathibiti Corona isisambae lakini pia tunathibiti homa ya dengue, ukiangalia kipindi hiki ni cha msimu wa mvua, magonjwa mengi ya mlipuko hutokea , kwa hiyo hii ni njia ya kuwakinga wananchi wetu wa Kinondoni wasipate maambukizi yoyote” amesema Dkt. Hemed.
Aidha ameongeza kuwa hotel hizo za kitalii ni maarufu na ndio ambazo zinapokea wageni wengi hivyo nawasishi muendelee kuchukua tahadhari kwa kutoa ushirikiano na Halmashauri yetu ili mlipuko huu usiendelee kwenye maeneo watu.
Awali, Kinondoni ilianza mchakato huo wa kupuliza dawa katika vituo vya daladala, mwendokasi, na maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo Kanisani na Misikitini pamoja na maeneo ya wananchi na kwamba bado zoezi hilo linaendelea.
Hadi sasa zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa Kinondoni linaendelea kwani Kata 20 zilizopo kwenye Halmashauri zimeshafikiwa sambamba na matangazo ikiwemo kubandika mabango, kugawa vipeperushi kwa wananchi vyenye ujumbe wa kuelimisha namna ya kujikinga na virusi vya COVID19 ( Corona).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.