Habari za Punde

MIAKA 36 YATIMIA TOKA KIFO CHA CAMARADA EDWARD MORINGE SOKOINE!!!


1. USULI:

Jumapili mujarab ya leo, tarehe 12.4.2020, Taifa letu linatimiza miaka 36 toka kipenzi cha Watanzania, Mh. EDWARD MORINGE SOKOINE afariki kwa ajali ya gari siku ya Alhamis, tarehe 12.4.1984 eneo la Dakawa, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro.

ATIKALI hii inamuelezea Kiongozi huyu shupavu toka alipozaliwa hadi alipofariki. Hii itawasaidia wengi, hasa The Dot.Com Generation, kuelewa kwanini Taifa linamuenzi Kiongozi huyu ambaye alikuwa ni Zawadi ya Mungu kwa Watanzania.

2. SOKOINE Azaliwa

Jumatatu ya tarehe 1.8.1938, katika kitongoji cha Kilasho, kijiji cha Emairete, Monduli Juu, Arusha, huku mvua kubwa na radi vikirindima,  alizaliwa mtoto wa kiume buheri wa afya, aliyeitwa EDWARD MORINGE SOKOINE. Baba yake aliitwa SOKOINE OLE SEVERE na mama yake aliitwa NAPELEL SINYATI NOOMAYAKI.


3. SOKOINE Apelekwa Shule

Mwaka 1949, akiwa na miaka 11, wazazi wa wake walimpeleka shule ya msingi Monduli.  Mwaka 1953, alifanya mtihani wa kitaifa "STD Four Territorial Examinations" na baada ya kufaulu akajiunga na "Monduli Middle School " hadi mwaka 1956 na baadaye akajiunga na shule ya sekondari Umbwe.

4. SOKOINE Ajiunga TANU

Tarehe 1.1.1961, SOKOINE alijiunga na chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilichokuwa kikipigania uhuru wa Tanganyika.

5. SOKOINE Agombea Ubunge 1965

Tarehe 25.10.1965, SOKOINE, akiwa kijana mdogo tu wa miaka 27, lakini mwenye akili na ubunifu mwingi, aligombea na kushinda ubunge kwa kishindo jimbo la Monduli.

6. Mh. SOKOINE Aukwaa Uwaziri Mdogo

Mwaka 1967, SOKOINE akiwa na miaka 29 tu, aliteuliwa na Rais NYERERE kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Uchukuzi na Kazi.

7. Mh. SOKOINE Ashinda Ubunge 1970

Katika uchaguzi mguu, tarehe 25.10.1970,   Mh. SOKOINE aligombea tena ubunge jimbo la Manduli na kushinda kwa kishindo.

8. Mh. SOKOINE Aukwaa Uwaziri Kamili

Mwaka 1970, baada ya Uchaguzi Mkuu, Rais NYERERE alimteua Mh. SOKOINE kuwa Waziri wa Nchi. Aidha, mwaka 1972, baada ya kuvutiwa na uchapakazi wake usio wa kawaida, Rais NYERERE alimteua SOKOINE kuwa Waziri katika Wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

9. Mh. SOKOINE Awa Mjumbe wa CC

Baada ya TANU na  ASP kuungana tarehe 5.2.1977 huko Zanzibar, Mh. SOKOINE akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC).

10. Mh. SOKOINE Ateuliwa Waziri Mkuu

Kutokana na uchapakazi wake mujarab usio na mawaa yoyote, tarehe 13.2.1977, Rais NYERERE, baada ya kulifumua Baraza la Mawaziri, akamteua Mh. SOKOINE kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa TZ.

11. Mh. SOKOINE Ajiuzulu Uwaziri Mkuu 1980

Tarehe 7.11.1980, Mh. SOKOINE alijiuzulu Uwaziri Mkuu na kwenda masomoni Yugoslavia. Rais NYERERE akamteua Mh. CLEOPA  DAVID MSUYA kuwa Waziri Mkuu.

12. Mh. SOKOINE Arejea 1983, Ateuliwa Waziri Mkuu

Mh. SOKOINE alirejea nchini mwaka 1983. Kutokana na imani kubwa aliyokuwa Rais NYERERE kwa Mh  SOKOINE, mara moja akamteua tena kushika wadhiwa wake wa Waziri Mkuu, tarehe 24.2.1983.

13. Mh. SOKOINE Atinga Bungeni Machi 1984

Mh. SOKOINE aliwasili bungeni Dodoma mwezi Machi 1984 na kama Kiongozi wa Serikali bungeni, aliliongoza Bunge kwa umahiri na weledi wa hali ya juu.

14. Mh. SOKOINE Ajumuika na Wabunge

Jumatatu ya tarehe 9.4.1984, Mh. SOKOINE alijumuika na wabunge waliokwenda kusali asubuhi kanisa la Mt. Paul.

Usiku wa Jumanne, tarehe 10.4.1984, Mh. SOKOINE aliandaa karamu kabambe "Cocktail party" na kuwaalika Mawaziri na Wakuu wa Mikoa. Katika dhifa hiyo, Mh. SOKOINE alizunguka na kuongea na kila mmoja wao.

Kesho yake jioni, siku ya Jumatano, tarehe 11.4.1984, Mh. SOKOINE, aliyekuwa mtu mwema na mwenye utu, aliandaa karamu kwaajili ya wabunge wa mkoa wa Arusha ambapo aliwasisitizia kuhakikisha wanafanya kila wawezalo ili kuwasaidia Wamasai kuondokana na ufukara mkubwa walionao.

15. Mh. SOKOINE Alivunja Bunge

Siku ya Jumatano, tarehe 11.4.1984, Mh. SOKOINE alilivunja bunge na kuliaga ambapo alitiririka:

"Ndugu Spika, ningependa kumalizia kwa kukubaliana na wabunge kuwa lazma tutafute njia ya kuikomesha tabia hii ya kutumia fedha bila ya idhini ya Bunge........ Mungu akipenda tutakutana katika kikao kijacho. Mimi nitasafiri kwa njia ya barabara ili nijionee hali ya mazao ya wakulima wetu.....".

16. Mh. SOKOINE Apata Ajali, Afariki

Alhamis, tarehe 12.4.1984, Mh. SOKOINE aliondoka Dodoma na msafara wake akiwa ndani ya Mercedes Benz yake huku msafara huo ukiongozwa na gari la polisi. Magari yote yaliyokuwa yakikutana na msafara huo, yalikuwa yakipaki pembeni kuupisha, baada ya kuamriwa na gari la mbele la polisi. 

Baada ya msafara huo kufika Dakawa, kilometa 30 toka Morogoro, ghafla kilisikika kishindo kikubwa sana!. Mercedes Benz ya Mh. SOKOINE iligongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Landcruiser lililokuwa likiendeshwa na DUMISAN DUBE(23), mpigania uhuru wa ANC aliyekuwa akiishi Mazimbu, Morogoro. DUBE, aliyekuwa kwenye mwendo kasi kama MICHAEL SCHUMACHER, hakuweza kusimama aliposimamishwa na polisi. DUBE alikuwa na abiria wawili ambao ni BOYCE MOYE na GEORGE PERCY.

Mh. SOKOINE, aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma huku akiwa hajafunga mkanda, alirushwa na kugonga kioo cha mbele ambapo aliumia sana shingoni na kifuani na kufariki akiwa njiani kupelekwa hospitali ya serikali Morogoro ambako alipofikishwa madaktari walieleza kuwa amekwishafariki!.

Bw. YUSTO CHUMA, aliyekuwa mlinzi wake ambaye alikaa kiti cha mbele kushoto, aliumia vibaya na Bw. ALLY ABDALLAH, aliyekuwa dreva wake, alivunjika mguu.

17. Rais NYERERE Alitangazia Taifa Kifo

Alasiri ya siku hiyo ya Alhamis, Radio Tanzania Dsm ilisitisha ghafla vipindi vyake na kupiga wimbo wa Taifa. Rais NYERERE, mara tu baada ya wimbo wa Taifa, kwa uchungu mkubwa lakini kwa ujasiri wa hali ya juu, akalitangazia Taifa kuhusu kifo hicho cha kipekee, ambapo alisema-:

"Ndugu wananchi, leo mnamo saa saba mchana, ndugu yetu na kijana wetu, Edward Sokoine, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipokuwa akirudi Dar Es Salaam kutoka Dodoma, gari lake lilipata ajali na amefariki dunia. Naomba muamini Edward amefariki kwa ajali na si kitu kingine".

18. Nchi Nzima Yakumbwa na Vilio, Simanzi

Baada tu ya taarifa hiyo,  nchi nzima, toka Kalumbulo Kyela hadi Kahororo Kagera, vilio vilitamalaki na wananchi walikumbwa na simanzi kubwa kwa kuondokewa  na kipenzi chao na kupelekea kazi na shughuli zote kusimama. Kikao cha UWT kilichokuwa kikifanyika ofisi ya CCM Lumumba kilisambaratika mara tu baada ya Mwenyekiti wa UWT, Mh. Mama SOPHIA KAWAWA alipowatangazia wajumbe habari hizo za kusikitisha zilizoleta jakamoyo na jitimai kubwa!.

 Aidha, watanzania waliokuwa nje ya nchi nao walimlilia sana SOKOINE.

19. Serikali Yatangaza Maombolezo

Kufuatia kifo hicho cha Jemedali SOKOINE, serikali ilitangaza maombolezo ya wiki mbili na bendera kupeperushwa nusu mlingoti nchi nzima.

20. Mwili wa SOKOINE wafikishwa Ikulu

Mwili wa marehemu SOKOINE ulifikishwa Ikulu, saa 11 jioni ya siku hiyo hiyo ukiwa umefunikwa kwa bendera ya Taifa.

21. Rais NYERERE Ashindwa Kuvumilia, Aangua Kilio:

Mwili wa marehemu SOKOINE uliwekwa sehemu maalum Ikulu. Rais NYERERE, akiambatana na mama MARIA, alijongea kwenye mwili huo na kuifunua bendera ya Taifa. Kisha akaweka mikono yake miwili kwenye paji la uso wa SOKOINE. 

Rais NYERERE na mama MARIA, aliyekuwa ameshika kitambaa cheupe, walishindwa kuvumilia na wakalia kwa uchungu mno hadi walinzi wao walipowaondoa. Rais NYERERE alikuwa na huzuni kubwa na ilikuwa ni mara ya kwanza kwa watu kumuona akilia hadharani!.

Kwa hakika ilikuwa ni huzuni kubwa kwavile marehemu SOKOINE ndiye aliyekuwa akitarajiwa kwa 99% kuwa ndiye angekujakuwa Rais wa TZ mwaka 1985.

22. Mh. JOSEPH NYERERE Azua Timbwili na Kimuhemuhe Ikulu

Mh. JOSEPH NYERERE, mdogo wa Rais NYERERE, ambaye alijulikana kwa kutomung'unya maneno, ghafla bin vuu, alitinga ulipo mwili wa SOKOINE huku akilia kwa uchungu. Akiwa na uchungu na hasira kwa pamoja, Mh. JOSEPH akazomoka maneno mengi mf-:
"Mwalimu, huna ulinzi. Waziri Mkuu anakufa barabarani?!!.

Kufuatia kimuhemuhe na taharuki hiyo, walinzi wa Ikulu walimuondoa haraka maeneo ya Ikulu.

Jioni hiyo ya Alhamis, mwili wa SOKOINE ukapelekwa hospitali ya Lugalo kuhifadhiwa.

23. Jeneza Latengenezwa Usiku wa Manaani!

Bw. GEORGE CHRISTOS alipewa jukumu la kutengeneza jeneza la marehemu SOKOINE. Baba yake bwana huyu alikuwa Mgiriki na mama yake alikuwa Msukuma aliyeitwa MARIA, mmoja wa mabinti wa Chifu KIDAHA.

Bw. CHRISTOS ndiye aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu, TZ.

Bw. CHRISTOS na mkewe, Bi. ELIZABETH WALKER, walitinga hospitalini na kuchukua vipimo vya marehemu SOKOINE aliyekuwa mtu wa miraba minne.

Bw. CHRISTOS, Bi. WALKER na Mh. PAUL MKANGA, aliyekuwa Katibu Mkuu, Ujenzi walienda kwenye kiwanda cha Hem-Singh, Chang'ombe ambapo walimkuta mwenyewe akiwa katika harakati za kufunga. Kutokana na unyeti wake, ikabidi aendelee na kazi na akamaliza kulitengeneza jeneza hilo usiku wa maanani na Bi WALKER akalipamba kwa umahiri mkubwa kisha likapelekwa hospitalini. 

24. Marehemu SOKOINE Aagwa Dsm

Ijumaa, tarehe 13.4.1984, wakazi wa jiji la Dsm, ZNZ na mikoa ya jirani walifurika kumuaga kipenzi chao. Kwa hakika, ulikuwa ni umati mkubwa ambao ulikuwa haujawahi kuonekana toka tupate uhuru. Rekodi ya umati huo ilikuja kuvunjwa na umati uliojitokeza kumuguaga Baba wa Taifa, Octoba 1999. 

25. DALADALA Zawapeleka Watu Bure "Airport'!

Jumamosi, tarehe 14.4.1984, ilikuwa ni siku ya wananchi kuelekea "Airport" kuusindikiza mwili wa SOKOINE kuelekea Arusha.

Daladala zote Dsm ziliwachukua wananchi na kuwapeleka bure "Airport" , ukiwa ni mchango wao kuntu kwa kipenzi chao, marehemu SOKOINE.

Mh. SOKOINE, mwaka 1983, baada ya kuona UDA "inambwelambwela", ndipo alipoanzisha utaratibu wa "DALADALA". Jina hilo lilitokana na neno "Dollar" ambapo "Exchange  rate" kwa wakati huo ilikuwa ni shilingi TANO ambayo ndio ilikuwa nauli ya Daladala.

Mwili wa SOKOINE, hatimaye, ukafika salama Arusha.

26. Mh. SOKOINE Apumzishwa Nyumba yake ya Milele

Jenerali JOHN BUTLER WARDEN "Black Mamba", Mtanzania chotara, akisaidiwa na Vijana wa TPDF alijenga kaburi la aina yake. Hii ilipelekea Jenerali WARDEN aje kupewa kandarasi ya kujenga kaburi la marehemu Rais SAMORA MOSES MACHEL wa Nchumbiji aliyefariki baada ya ndege yake aina ya Tupulov Tu 134, kuanguka tarehe 19.10.1986.

Mazishi ya marehemu SOKOINE, huko Monduli, yalipewa heshima zote za kitaifa na yalihudhuriwa na maelfu ya watu wakiongozwa na Rais NYERERE na yalihudhuriwa pia na viongozi toka nje ya nchi.

Miongoni mwao ni Mh OLIVER TAMBO aliyekuwa Rais wa ANC na Mh. ALFRED NZO aliyekuwa Katibu Mkuu, ambao walieleza masikitiko yao kwa kifo hicho kusababishwa na raia mwenzao wa Afrika Kusini, DUMISAN DUBE.

27. Mh. SOKOINE Aacha Wake 2, Watoto 11

Mh. SOKOINE alipofariki aliacha wake wawili (NAPONO na NAKITETO) na watoto 11, wakiwemo wawili ambao walikuwa kuwa viongozi ie Balozi JOSEPH na mbunge NAMELOK.

28. DUBE Afikishwa kwa "PILATO", "Apigwa Mvua 3!"

Tarehe 12.6.1984, DUMISAN DUBE alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro, mbele ya Mh. Mh. SIMON KAJI (PRM). Upande  wa Mashtaka uliongozwa na JOHNSON MWANYIKA (SSA) ambaye alikuwa na mashahidi 21, aliwemo mkulima aliyeshuhudia ajali hiyo.

DUBE aliposomewa mashtaka 7, alikiri hivyo Mh. KAJI akampa kifungo cha miaka 3.

29. Mambo yaliyofanya Mh. SOKOINE Kuwa Kipenzi cha Rais NYERERE na Watanzania:

29.1 Mh. SOKOINE alichukia Rushwa, hakupenda Utajiri

Msibani Monduli, Rais NYERERE alieleza- "Marehemu Edward alichukia na kupambana na rushwa kwa dhati kabisa. Hakuwa na mali yoyote ukiachilia ng'ombe wa urithi. Alikuwa na suti 3 na viatu pea 2 tu".

29.2 SOKOINE Alipenda Usawa

Mh. SOKOINE alieleza, tarehe 1.2.1977- "Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi lazma yawe kwa faida ya wote".

29.3 SOKOINE Alisisitiza Maendeleo

Mh. SOKOINE alieleza, tarehe 11.12.1982:- "Naskia huko mikoani baadhi ya viongozi wanagombea nyumba na magari. Hayo sio mambo muhimu. Viongozi wanapaswa kugombania maendeleo ya wananchi wetu. Huu ni ugomvi mtakatifu".

29.4  Mh. SOKOINE Alikuwa Mbunifu

Mh. SOKOINE alianzisha Mfuko Maalum "The Presidential Trust Fund" Ikulu, ambapo kila mwezi alikuwa akiweka sehemu ya mshahara wake ili kuwasaidia akina mama kukopa!. Wakinamama wengi wamenufaika kwa mfuko huu.

29.5 Mh. SOKOINE Alikuwa Mchamungu

Mh. SOKOINE alikuwa mchamungu sana. Alikuwa Mkristu Mkatoliki na Mwanachama wa  Utawa wa Tatu wa Mt. Francisca.

29.6 Mh. SOKOINE alikuwa Mchapakazi Hodari

Mh. SOKOINE alifanya kazi hadi mara nyingine usiku wa maanani. Aliwachagua vijana 2 hodari MARTENS LUMBANGA na PHILLEMON LUHANJO waliokuwa chini ya Katibu Mkuu,  HORRACE KOLIMBA. Hawa watatu walibatizwa jina "Wafuasi wa SOKOINE" kwani nao walikuwa waadilifu na wachapakazi makini na waliongozana nae kila alikokwenda.

29.7 SOKOINE alichukia sana Viongozi Wazembe

Mh. SOKOINE hakuwa na simile na Viongozi wazembe, kama alivyoeleza tarehe 26.3.1983- "Ole wake Kiongozi mzembe nitakayemkuta. Viongozi wazembe na wabadhilifu wahesabu siku zao".

29.8 SOKOINE alichukia Upuuzi

Mwezi Machi 1983, Mh. SOKOINE alifanya ziara mkoani Singida. Mmoja wa viongozi mkoani humo akamfuata Bw. ACCADOGA CHILEDI aliyekuwa "Press Secretary" wa SOKOINE  na kumwambia- "Mzee tumeishamtayarishia blanketi chapa ya mtu, atafurahi sana kwani huku Singida ni wazuri mno". Bw. CHILEDI akamjibu- "Hivi we mheshimiwa, je, SOKOINE unaumjua au unamsikiaga tu? Ebu ondoka na huo upuuzi wako maana nikimwambia Mh. SOKOINE, ujue utapoteza kazi yako hapahapa!".

Mbio alizotimua Kiongozi huyo baada ya kuelezwa hivyo na Bw. CHILEDI, hata kishada USAIN BOLT angesubiri!.

30. Dr. JPM alimkubali Sana SOKOINE

Dr. JPM, tarehe 12.4.2018, alieleza kinagaubaga kuwa alimpenda sana SOKOINE-

"Tarehe 12.4.1984, Mh. Edward Sokoine alipofariki kwa ajali ilikuwa huzuni kubwa sana nchini. Mimi nilikuwa JKT Mpwapwa "OPERESHENI YA NGUVUKAZI". Mimi nilimpenda sana marehemu Sokoine kwani alipiga vita rushwa, wizi na unyonyaji. Marehemu Sokoine alikuwa Mzalendo kwelikweli na kamwe hatasahaulika Tanzania. Ni wito wangu tumuige marehemu Sokoine".

31. MWISHO:

Marehemu EDWARD MORINGE SOKOINE alikuwa ni Zawadi ya Mungu kwa Watanzania.

32. TAFAKURI JADIDI:

Je, wewe Kiongozi au Mwananchi wa kawaida, unamuishi vipi marehemu SOKOINE kama Rais wetu Dr. JPM alivyotuasa?.

Imeandikwa na MZEE WA ATIKALI 

Aprili 12, 2020

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.