Na Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), leo
imezindua rasmi filamu inayoitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi katika
maeneo mbalimbali ya utalii ambayo inaendana na kauli mbiu ya Tanzania
Isiyosahaulika “Tanzania Unforgettable”
yenye kuitambulisha Tanzania duniani kote.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mwenye dhamana
ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala amesema kuwa Tanzania imeendelea
kutangaza utalii pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19, kwani, Rais Dkt.John
Pombe Magufuli ameiongoza vyema nchi katika mapambano bila kuathiri sekta za
kiuchumi ikiwemo Utalii.
“Namshukuru Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kutuongoza vyema katika mapambano ya covid-19 bila kuathiri sekta za kiuchumi
ikiwemo hii ya utalii, kwani kwa sasa
tumefungua sekta hii, kama mnavyojua biashara ni ushindani atakeyewahi kufungua
na kuweka misingi mizuri ya kuwahudumia wageni na wahudumu sekta ya utalii
ndiye atakayepata faida zaidi, tumeamua kufungua utalii wetu na sasa anga letu
lipo wazi kwa watalii”, Dkt.Kigwangala.
Amefafanua kuwa Tanzania imejipanga kuwahudumia vyema
watalii watakao watawasili nchini na kuhakikisha kuwa wanaondoka salama ili
wakifika katika nchi zao wapeleke habari njema kwamba Tanzania ni salama na
watalii ambao walisita kuja waje bila woga.
Amebainisha kuwa Serikali imeamua kufungua sekta ya
utalii kwa kufuata tahadhari zote zinazotolewa na mamlaka husika ikiwemo Wizara
ya Afya ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO), na kuwakaribisha watalii.
Katika uzinduzi huo, Waziri Kigwangala ametoa rai kwa Watanzania
kuisambaza filamu hiyo kwenye mitandao
yao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, Instgram, telegram na mitandao
mingine, ili iweze kuwafikia walengwa kwa lengo la kutangaza Tanzania kiutalii
katika soko la utalii la kimataifa.
“Hii ni video rasmi au filamu fupi kwa lengo la
kuitambulisha nchi yetu kiutalii katika soko la utalii kimataifa, na hii
imeendana sawa kabisa na kauli mbiu ya Tanzania
Unforgettable kwa hiyo ninaomba Watanzania wenzangu tuisambaze kwenye
mitandao yetu ya kijamii kwa maana imetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili,
Kingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiisrael na Kichina”, Dkt. Kigwangala.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania
(TTB), Bi.Devotha Mdachi alisema kuwa Tanzania kwa sasa imejikita zaidi
kutangaza vivutio vya utalii kupitia mitandao ya kijamii, kwa hiyo kuzinduliwa
kwa filamu hiyo fupi kutawasaidia kuteka soko la ndani na nje ya nchi.
“Sisi Kama Bodi ya Utalii tumejikita zaidi kutangaza
utalii kwa kutumia mitandao ya kijamii, kwani mpaka sasa tuna vipindi
vinavyoruka mubashara kupitia mitandao yetu kwa mfano kipindi cha Serengeti safari show na kile
kinachorushwa na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro, hizi ni moja ya njia za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi”, Bi.
Mdachi.
Ameongeza kuwa kupitia filamu hiyo fupi watalii
watapata fursa ya kuona utamaduni na maeneo mbalimbali ya kuvutia na kuweza
kuchagua sehemu sahihi ya kwenda kutembelea, amewataka Watanzania hasa watu
maarufu kusambaza filamu hizo za dakika moja, dakika tatu, dakika saba na
dakika 10 kwenye kurasa zao ili ziweze kufika mbali zaidi.
No comments:
Post a Comment