Habari za Punde

Jangombe Boys Iko Katika Njia Panda Kuendelea Na Ligi Kuu ya Zanzibar Kutokana na Uhaba wa Fedha



NA MWAJUMA JUMA
TIMU ya soka ya Jang’ombe Boys ipo hatiani kuendelea na ligi wakati itakapoanza kwa kile walichodai kukabiliwa na ukata wa fedha.

Rais wa timu hiyo ambayo inashiriki ligi Kuu ya Zanzibar Ali Othman Kibichwa alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba mpaka sasa hawana uhakika mkubwa wa kuendelea na ligi kwa kipindi hichi.

Alisema kuwa timu yao haina udhamini hata kidogo na inategemea mchango kutoka kwa wanachama na viongozi lakini kutokana na hali ya maradhi ya Corona uchumi wao umeyumba.

“Hatuna uhakika mkubwa kama tutaendelea na ligi timu yetu kama unavyojuwa inategemea wanachama wetu na sisi viongozi lakini sasa hivi kwa kuwa tumelala biashara haziendi sijui kama tutakuwa na uwezo huo”, alisema Kibichwa.

Alisema kuwa uongozi wao hivi karibuni ulikutana kwa njia ya mtandao kama ambavyo walivyoanzisha kawaida yao baada ya kutokuwepo mkusanyiko ambapo moja kati ya mambo waliyojadili ni hilo kuhusu kurudi katika
ligi au la.

Alisema kuwa timu yao imebakisha michezo saba nayo ni ya nyumbani na genini sasa kutokana na ukata wa fedha ambao unawakabili ni Dhahiri kwamba hawatoweza kumudu usafiri.

“Na hilo sio usafiri tu hata hayo maandalizi ya mechi pia yatatushinda kwa sababu sasa hivi kila ambae unamtazama hana kitu”, alisema.

Hata hivyo alisema kuwa uhakika kamili juu ya kurudi au kutokurudi utajuulikana mara baada ya kukaa kikao na vilabu vyengine ambavyo mkutano wao ulikuwa ufanyike Jumamosi iliyopita na kuhaairika.

Alisema kuwa kikao hicho kitakaa tena mara baada ya kumalizika suintafahamu kati ya Kamati Tendaji ya Shirikisho la Soka Zanzibar “ZFF” na rais wao.

Alisema kuwa katika kikao cha umoja wa vilabu viongozi hao walitaka kukutana na viongozi wa kamati hiyo ambao walichaguliwa kwa kura.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.