Habari za Punde

Makamu wa Rais aendelea na ziara ya kichama mkoa wa kaskazini Unguja

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM ya Mkoa wa Kaskazini Unguja  alipowasili katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja  iliopo Mahonda  leo Julai 01,2020. Makamu wa Rais yupo katika ziara ya Kichama Mkoa wa kaskazini Unguja.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM MKoa wa Kaskazini Unguja wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumza nao katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini iliopo Mahonda leo Julai 01,2020. Makamu wa Rais yupo katika ziara ya Kichama Mkoa wa kaskazini Unguja.  (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM ya Mkoa wa Kaskazini Unguja katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini  iliopo Mahonda Unguja  leo Julai 01,2020. Makamu wa Rais yupo katika ziara ya Kichama Mkoa wa kaskazini Unguja. kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Idi Ali Ame.


 NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Taifa ambaye pia ni Makamu wa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi na wanachama wa CCM Mkoa huo kuweka mbele maslahi ya Chama badala ya maslahi yao binafsi.

Hayo ameyasema katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama, wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, huko katika Ofisi za Chama Mahonda.

Alisema kila kiongozi anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka huu.

Mhe.Samia aliwambia wajumbe hao kuwa wamepewa dhamana kubwa ya kiuongozi hivyo wanatakiwa kuwa mfano bora kwa wanachama wanaowaongoza.

" Tufanyeni kazi kwa upendo,ushirikiano na uadilifu mkubwa kwa lengo la kuhakikisha Chama kinashinda kwa asilimia kubwa na kulinda heshima ya Mkoa huu.", alisema Mhe.Samia.

Katika maelezo yake Mhe.Samia,alisema kila mwana CCM anatakiwa kulinda kwa vitendo tunu za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na Muungano kwa kuhakikisha CCM inashinda na kubaki madarakani.

Kupitia kikao hicho Mhe. Samia, aliwapongeza viongozi wa mkoa huo kwa mabadiliko makubwa yaliyofikiwa katika kuimarisha chama na kuwasihi walinde heshima hiyo kwa kukiletea ushindi chama katika uchaguzi.

Naye Katibu wa Chama Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa huo, Mulla Othman Zubeir, alisema chama kimejipanga vizuri kuhakikisha kinashinda katka uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mulla alisema, ndani ya mkoa huo Ilani ya uchaguzi ya  CCM ya mwaka 2015/2020 imetekelezwa kwa asilimia 99 katika sekta za elimu na afya.

Aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ndani ya Mkoa huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.