Habari za Punde

NAIBU WAZIRI MHE.KANYASU ASIKITISHWA NA TAASISI MBILI ZA SERIKALI KUTOKUELEWANA KISA ARDHI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu jana akiwa ameongoza na Watumishi wa Shamba laMiti la Sao Hill  akipewa maelezo na Afisa Misitu, Glory Fortunatus wakati alipokuwa akitembelea bustani ya miti ya shamva hilo lililopo katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa 
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza  na baadhi ya Wafanyakazi wa Shamba la Miti la Sao Hill wakati alipofanya ziara ya kutembelea bustani ya miti katika shamba hilo lilipo katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhe.Constantine Kanyasu akiwa ameongoza na baadhi ya Watumishi wa Shamba la Miti  Sao Hill wakati akikagua vifaa maaalum vya kuoteshea miti kabla ya kupelekwa shambani kwa ajili ya kupandwa.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhe.Constantine Kanyasu akizunguma na Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill pamoja na Afisa Misitu Glory Fortunatus ( wa kwa kushoto) wakati akiangalia miti iliyooteshwa kwa vifaa maalumu ambayo ipo tayari kwa ajili ya kupelekwa shambani kwa ajili ya kupandwa.
( Picha zote na Wizara ya Malasili na Utalii) 


lusungu helela

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Constantine Kanyasu ameonesha kusikitishwa na uwepo wa mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10  baina ya Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT) Mafinga na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  ambazo zote ni  Taasisi za Serikali kuwa jambo hilo sio la kawaida.

Ameyasema hayo  jana wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Shamba la Miti la Sao Hill linalosimamiwa na TFS  lililopo katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa 

Amesema eneo hilo la ardhi lenye mgogoro lina ukubwa wa hekta 1705 ambazo kati ya hizo hekta 600 zilishapandwa miti na TFS ila baada ya mgogoro huo kuibuka kila Taasisi ikidai kuwa eneo hilo ni lake ilipelekea TFS kushindwa kumalizia kupanda miti katika eneo lililokuwa limebaki lenye jumla ya  hekta 800.

Kufuatia hali hiyo, Mhe. Kanyasu ameitaka  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo  ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ishughulikie mgogoro huo uliopo baina ya JKT Mafinga  na Shamba la Miti Sao Hill ili kila Taasisi ijikite kwenye majukumu yake ya msingi.

"Mgogoro huu usipotafutiwa ufumbuzi wa haraka utaleta athari, Kitendo cha JKT Mafinga kung'oa vigingi vilivyowekwa na TFS kwa ajili ya kubainisha  mipaka haileti picha nzuri ikizingatiwa kuwa zote hizo  ni Taasisi za Serikali"  alisisitiza.

Amesema endapo Kamati hiyo Ulinzi na Usalama itafika mwisho na kushindwa kupata majibu juu ya mgogoro huo imshirikishe Mkuu wa mkoa wa Iringa ili mgogoro huo uweze kuisha.

Amesema ni lazima  mgogoro huo ufike mwisho na ikishindikana Mkuu wa Mkoa ashirikishwe hali itakayosaidia kuleta suluhu ya kudumu na kuzifanya Taasisi hizo kuendelea kutoa huduma kwa jamii badala ya kuendelea kusigana kila kukicha.

"Nina amini Mkuu wa mkoa ana vyombo na. uwezo wa kumaliza mgogoro huu kwa vile hizi zote ni Taasisi za Serikali" alisisitiza Mhe.Kanyasu

Hata hivyo, Mhe.Kanyasu amesema endapo Mkuu wa Mkoa atashindwa  kuutafutia majibu mgogoro huo basi aitaarifu Wizara ya Maliasili na Utalii ili iweze kukutana Wizara husika kwa lengo la  kumaliza  mgogoro huo.

Amesema anataka mgogoro huo ufike mwisho na kama nyaraka zitaonesha kuwa eneo hilo la JKT basi JKT wapewe na kama ikithibitika ni eneo hilo ni mali ya TFS wapewe ili waweze kupanda miti.

"Jukumu letu sisi ni kupanda miti   tunachotaka ni kuona eneo hilo linapandwa miti bila kujali kapanda nani JKT au TFS " alisisitiza Mhe.Kanyasu.

Hata hivyo, Mhe.Kanyasu amempongeza Mkuu wa wilaya hiyo kwa kuushughulikia mgogoro huo licha ya kuwa umekuwa ukienda taratibu sana na hivyo kasi ya TFS kumalizia kupanda miti katika eneo hilo imekuwa ikitatizwa na kuwepo kwa mgogoro huo.

Kwa upande wake, Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill, Juma Mwita  amesema mgogoro huo wa ardhi umekuwa ukitishia amani baina yao, hivyo endapo utafikia mwisho utaweza kurejesha mahusiano baina ya pande hizo mbili ambazo zote zinaihudumia jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.