Habari za Punde

TAMWA Zanzibar Yawapongeza Wagombea Wanawake Waliojitokeza Kuwania Urais wa Zanzibar Kupitia CCM.


Wakati zoezi la uchukuaji wa fomu na kurejesha kwa nafasi ya Urais Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) likifikia tamati, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania  (TAMWA) Zanzibar kinawapongeza kwa dhati wanawake wote waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa wagombea wa kiti cha Urais Zanzibar kupitia Chama hicho.
Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya mgombea Urais Zanzibar ulioanza Juni 15, mwaka huu, jumla ya wanachama 32 wamejitokeza kwenye kinyanganyiro hicho ambapo wanachama watano (5) sawa na asilimia 15 walikuwa ni wanawake.

Wanawake hao ni pamoja na Bi. Mwantum Mussa, Bi.Hasna Attai Masoud, Bi. Fatma Kombo, Mhe.Mgeni Hassan Juma na Mhe. Maudline Castico.
Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kujitokeza wanawake kugombea katika nafasi hiyo ya juu ya nchi kutokana na mifumo dume ambayo inamtenga mwanamke katika kuwania nafasi za maamuzi sambamba na mwenziwe mwanamme.

Hadi miaka ya 1940 ilionesha kuwa mwanamke alikatazwa kuhudhuria hata skuli, nyenzo muhimu katika kukwaa ngazi za kisiasa na kijamii kwa madai kuwa anaweza kupoteza ujanajike wake.

Hali hii ilirejesha nyuma sana maendeleo ya wanawake na nchi kwa jumla kwa vile wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya wakaazi wa Zanzibar kwa mujibu wa Sensa ya 2012 na makisio ya idadi ya watu yaliyofuata.
 
Tafiti duniani kote ikiwemo na Zanzibar zinaonesha kuwa wanawake ni watendaji wazuri, waaminifu, waadilifu na wanaofanya maamuzi kwa njia ya ushirikishi na hivyo wakiwa kwenye uongozi huharakisha sana maendeleo ya nchi.


TAMWA Zanzibar inapenda kuipongeza CCM kwa kuwawezesha wanawake hao kutoka chama hicho kuweza kugombea hadi katika hatua hiyo ya uongozi.
 
Tunaamini sasa wakati umefika kwa jamii wakiwemo wanasiasa kulichukulia suala hili kwa uzito unaostahiki na hivyo kuwapa nafasi wanawake kuonesha uwezo wao wa kuongoza katika nyanja mbalimbali.
 
Tunatamani pia CCM itachagua mmoja kati ya wanawake hao ili kuweza kupeperusha bendera ya Chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

TAMWA Zanzibar inaamini kwamba ujasiri huo ulioonyeshwa na wanawake hao waliojitokeza utasaidia kuongeza hamasa zaidi kwa wanawake vijana kuendelea kujiamini na kuona kuwa wanayo nafasi sawa ya kushiriki katika ngazi zote za maamuzi kwa mstakabali wa taifa lao.

TAMWA Zanzibar inawaomba wanawake wa vyama vyengine vyote kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali ili kuongeza mabadiliko haya ya wanawake katika ngazi za maamuzi itakayopelekea pia kutatua kwa matatizo mbalimbali yanayowaaathiri kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.