Habari za Punde

TUNZO YA TANO YA FILAMU INAYOTOLEWA NA MFUKO WA EMERSON'S ZANZIBAR FOUNDATION KUTANGAZWA JULAI 4


Na. Mwandishi Wetu -ZANZIBAR
TAASISI ya Mfuko wa Emerson's Zanzibar Foundation (EZF) inatarajiwa kutangaza matokeo ya uhakiki wa filamu 21 zilizowaswilishwa  kwenye tunzo ya filamu iliyokusudiwa kuendeleza na kukuza Vipaji vya Vijana wa Kizanzibari wanaotengeneza filamu. 

Akitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari leo, Mwenyekiti wa Mfuko wa Wakfu wa  Emerson's Zanzibar Foundation, Said el-Gheithy alisema Wadhamini wa Bodi ya mfuko huo EZF ulipokea jumla ya filamu 21 kutoka Unguja na Pemba zilizoletwa katika tuzo hiyo inayotolewa  kila mwaka. Kati ya hizo  filamu Nane (8) pekee ndio zilizokidhi vigezo na sifa  zilizowekwa.

"Mwaka huu tunatoa tunzo ya tano....
Filamu 21zilizoandaliwa na Vijana wa Kizanzibari kutoka Unguja na Pemba, nane pekee ziliweza kupenya kwenye mchujo, na kuhakikiwa na Jopo la Majaji katika hatua ya mwisho. Matokeo yatatangazwa Julai 4 mwaka huu hapa Unguja." Alisema Mwenyekiti wa EZF, Said el-Gheithy.

Aliongeza kuwa:

"Bodi ya Wadhamini ya Emerson  Zanzibar Foundation imekuwa na utaratibu wa kutoa tunzo hiyo mwezi wa Julai kila mwaka linapofanyika Tamasha la Filamu za Kimataifa na za Nchi za Majahazi (ZIFF). Lakini  mwaka huu Tunzo hiyo itafanyika  kupitia mitandao ya kijamii.

"Tunzo ya Tano kwa mwaka huu itafanyika mitandaoni kutokana na janga la Kirusi cha Covid-19.", alimalizia Said el-Gheithy. 

Kwa upande wake Meneja Mwandalizi wa shughuli za Tunzo hiyo, Salma Adim alieleza kuwa tayari majaji wamekamilisha kuzikhakiki filamu hizo. Sasa inasubiriwa kutangazwa matokeo.

"Filamu zilizotengenezwa na Chipukizi ndio kauli mbiu ya mwaka huu. Hivyo basi katika filamu hizo 21 ni nane pekee zilizokidhi vigezo....... .", alisema Salma Adim.

Salma Adim aliwataja Majaji  Sita ambao ni wabobezi waliohakiki filamu hizo. Nao ni Helen Peeks, Bi. Maryam Hamdan, Lisenka Beetsra na Salum Stika ambao walihakiki hapa Zanzibar. Majaji wengine, Vanessa Victor na Amil Shivji wao walihakiki filamu hizo kwa njia ya mtandao (online).

Alizitaja filamu hizo zilizoingia Nane Bora ni:

'Mashaka', 'Kipaji', 'Urithi wa Mila', 'Youth Africa Life', 'Kijiji changu', 'Fikra yakinifu', 'Hofu ya Subira' na 'Tubadilike'.

Wadhamini wa bodi hiyo wameeleza kuwa, Mpewa mstahiki atatunukiwa fedha, Milioni Mbili (Ml.2), Tunzo maalum ya EZF na cheti cha ushiriki katika tukio adhimu Mjini Unguja. 

Tunzo hiyo imekuwa ikitolewa kila mwaka kuibua vipaji vya Vijana wengi Visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.