Habari za Punde

Dr Bashiru awataka watia nia kubaki majimboni wakisubiri uteuzi wa majina yao

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Ali Bashiru  akiangalia picha  zilizopambwa katika kituo hicho za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli na  Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi,  
 Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Ali Bashiru akizungumza na vyombo habari wakati wa uzinduzi wa  Kituo cha CCM CHA Mawasiliano ya Habari za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania. Picha ya juu akiangalia picha  zilizopambwa katika kituo hicho za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli na  Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi,  

Na Richard Mwaikenda, Dodoma 

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Ali Bashiru  amewataka wote waliotia nia kugombea ubunge kubaki kwenye majimbo yao kusubiri majina yatakayopitishwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho inayokaa Dodoma Agosti 20, 2020.

Dk. Bashiru amesema inabidi wabaki kwenye majimbo yao ili iwe rahisi kwa watakaopitishwa kugombea, kwenda kuchukua fomu, kutafuta wadhamini na kurejesha fomu ili Agosti 25 mwaka huu wazirejeshe Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya uteuzi.

Ameyazungumza leo baada ya kuzindua Kituo cha CCM CHA Mawasiliano ya Habari za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ambao kampeni zake zinatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Amesema kuwa leo kimekaa kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kuandaa taarifa ya wagombea itakayopelekwa kesho katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuchuja majina kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na hatimaye kuyapeleka Halmashauri Kuu Agosti 20 itakayoteua jina moja la mgombea kwa kila jimbo na wagombea wa viti maalumu.

“Kazi ya Sekretarieti siyo kufanya uteuzi bali ni kuandaa nyaraka, kufanya uchambuzi  taarifa  za vikao vya wilaya na mikoa za watia nia ubunge na wa viti maalumu ngazi ya Taifa, tunachambua na kuandaa mapendekezo na kuvipeleka Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa  na hatimaye  Halmashauri Kuu ya Taifa kwa aijili ya uteuzi.” Amesema na kuongeza kuwa…

“Tunatarajia sifa za chama chetu ndiyo msingi mkubwa, na chama chetu kwa sifa zake tutakuwa pia na viongozi wenye sifa hizo, kwa hiyo sifa za viongozi wanaotakiwa zipo kwenye Katiba na kanuni za uteuzi , mwadilifu, mchapakazi, jasiri, mzalendo, msikivu kwa anaowaongoza, mwenye nidhamu ya kutii maelekezo ya vikao wa chama.”

Amesema kuwa anatatarajia katika waliotia nia  kugombea zaidi 10,000,  kati yao watapata  wagombea bora, kwa sababu ya kipimo cha chama ni kuwa na hazina ya  viongozi, ni idadi ya waliotia nia na kwamba  mchakato umekuwa wazi kwa nchi nzima, kwenye urais, ubunge na udiwani. Kuhusu wawakilishi utaratibu wake utafanyika baadaye kwani  ratiba ya uchaguzi na kampeni imekuwa tofauti kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.