Habari za Punde

WAZIRI WA FEDHA ATEMBELEA KIWANDA CHA NGUO CHUMBUNI ZANZIBAR

Mkurugenzi  wa Kiwanda cha Nguo cha Basra (Basra Textilemills LTD )  Ahmed Osman Ahmed akimtembeza  Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Balozi  Mohamed  Ramia Abdiwawa wakati alipofanya ziara katika kiwanda hicho  kilichopo  chumbuni.    

Na Khadija Khamis –Maelezo   21/08/2020.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Balozi  Mohamed  Ramia Abdiwawa  amesema kukamilika kwa kiwanda cha nguo, (Basra Textilemilis L.T.D )  kutasaidia kuzalisha ajira mpya kwa vijana wa Zanzibar .
Hayo aliyasema wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho  ambacho kinaendelea na matayarisho ya kuanza kazi ya kuzalisha vitambaa mbali mbali ikiwemo vitenge, sare za wafanyakazi na wanafunzi , Madira  na nyenginezo kilichopo chumbuni .
Alifahamisha kuwa ujenzi wa kiwanda hicho  utazidisha ongezeko la  ajira kwa vijana ambazo zinatarajiwa kutolewa kwa awamu tofauti jambo hili litasaidia vijana wengi kujipatia fursa hiyo .
“Kazi zenu wenyewe vijana, mjitokeze kufanya kazi  katika kiwanda hichi ili  kujipatia kipato chenu cha halali,”alisema Balozi Ramia .
Aidha amefahamisha kuwa kutakuwa na utaratibu maalumu wa mpango ambao unatarajiwa kugawiwa katika maeneo matatu kwa awamu tofauti ambapo katika awamu ya kwanza tayari imeshaanza .
Alisema  Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kuongeza nguvu kwa wawekezaji ambao wanania ya kuwekeza miradi yao Zanzibar sambamba na  kuwapunguzia kodi za mali ghafi ambazo wanaziingiza nchini .
Aidha aliwataka wakaazi wa eneo hilo kumsaidia muekezaji huyo kutunza eneo hilo ili usitokezee  uharibifu wa mali na kufanya kazi zake kwa amani
Nae Meneja wa Kiwanda cha Basra textilemills L.T.D Ali Idrissa Mohamed ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano ya  pamoja katika kuwaunga mkono kwa lengo la kuendeleza kiwanda hicho .
Aidha amesema zaidi ya dola milioni 23 zimeshatumika hadi sasa kwa shughuli za utayarishaji wa kiwanda cha Basra Textilemills LTD na kutarajia .
Vile vile ameeleza kuwa wanatarajia kuajiri vijana kwa awamu tatu kwa idadi tofauti,vijana 453  kwa awamu ya kwanza 1200 awamu ya pili na 1600 kwa awamu ya tatu .
Ziara hiyo ni miongoni mwa ziara ya Mhe Balozi Mohamed Ramia  Abdiwawa alizotembelea maeneo mbali mbali ya  vianzio vya kiuchumi .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.