Na.
Immaculate Makilika- MAELEZO
Sikusudii kuamsha upya
hisia za huzuni zilizotugubika mara tu baada ya kusikia taarifa ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli akitangazia umma juu ya kifo cha Rais Mstaafu
wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa
kilichotokea usiku wa kuamkia Julai 24, 2020.
Ni dhahiri kuwa kifo
cha Rais huyo mstaafu na mwanadiplomasia
mkongwe ni pigo kwa taifa, Afrika pamoja na dunia kufuatia mchango wake
ulioakisi mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, mahusiano ya kimataifa na mapinduzi
katika sekta za umma na binafsi nchini.
Hakika, watanzania hawana budi kujifunza
mambo mengi aliyoyafanya Mzee Mkapa na pia
kumuenzi kwa kuthamini mchango wake uliosaidia kuleta mabadiliko katika kuleta maendeleo
ya kijamii, kiasiasa na kiuchumi.
Katika
uongozi wake mzee Mkapa alianzisha mikakati ya kimaendeleo kwa jamii katika nyanja
mbalimbali. Nyanja mojawapo ambayo chini ya uongozi wake iliandaliwa kimkakati ni
uendelezaji wa sanaa na muziki.
Kama
tunavyokumbuka, sekta ya sanaa na muziki kwa miaka mingi imekuwa na changamoto nyingi
hususan kuwepo kwa dhuluma kwa wasanii na wanamuziki ambao wamekuwa wakitegemea
kazi zao kwa lengo la kujipatia kipato. Wamekuwa wakitengeneza filamu na kutunga
nyimbo ambazo hazikuwanufaisha wasanii kutoka na kudhulumiwa , sababu kubwa
ikiwa ni kukosekana kwa Sheria ya Hakimiliki.
Kutokana na kilio cha
muda mrefu cha wasanii na wanamuziki kwa kuibiwa kwa kazi zao, mzee Mkapa
alianzisha Chama cha Hakimiliki Tanzania
(COSOTA), chombo ambacho ni cha kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria
ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999.
Chombo
hiki kimepewa mamlaka ya kusimamia Sheria ya Hakimiliki. Hatua hii ilikuwa ni
mwanzo wa safari ndefu ya wasanii na wanamuziki katika kuwaletea mafanikio
makubwa ikilinganishwa na sheria ya zamani ambayo miongoni mwa mambo mengine, haikuweka
kipengele cha kusimamia Hakimiliki za wasanii na wanamuziki.
Licha
ya kusimamia Hakimiliki, kazi nyingine za COSOTA ni kukuza na kulinda maslahi
ya waandishi wa vitabu, waigizaji, wafasiri, wachapishaji, watengenezaji wa
rekodi za santuri, watangazaji na wachapishaji na hasa kukusanya na kusambaza
mirabaha yoyote na malipo mengine yanayostahili kuhusiana na haki zao. Aidha, chama
hiki pia ni kiungo kati ya wamiliki wa
haki kwa upande mmoja na watumiaji wa kazi zao kwa upande mwingine.
Ni
dhahiri shahiri kuwa Mzee Mkapa alizingatia maslahi mapana ya watu
wanaojihusisha na kazi za sanaa, uandishi na utangazaji na hivyo kutokana na
kifo chake watanzania tuna kila sababu ya kuendeleza kila zuri alilolifanya. Sambamba
na kujifunza namna bora ya kuendeleza vipaji, kazi za sanaa na kila mmoja
kuchangia kwa namna yake kwa lengo la kuboresha maisha katika jamii, kupunguza
umasikini kama yalivyokuwa maono yake kwa taifa hili.
Katika kitabu
alichoandika Mzee Mkapa miezi kadhaa kabla ya kifo chake na kuzinduliwa na Rais
wa Awamu ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe
Magufuli, alielezea juu ya maisha yake binafsi.
Katika
kitabu hicho chenye jina la “Maisha Yangu, Dhamira
Yangu: Rais wa Tanzania Akumbuka” Mzee Mkapa alielezea kuwa
maono yake ni “maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii
iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo
shirikishi wa kipato.”Sasa basi funzo la kifo cha Mzee Mkapa
kwa wasanii wa filamu na hasa Bongo movie ni lipi? Ama upi mchango wa Bongo movie
kwa taifa?
Mbali
na mafunzo yanayopatikana katika filamu za Nsuka,
dereva Tax na ile ya Chausiku,
ambayo siwezi kusahau kwani ina radha yake ya maisha ya uswazi, au ile ya kitambo ya ushuani ya Girlfriend iliyotoka mwaka 2003 ikiwa ni filamu iliyoleta mapinduzi katika
sekta ya uigizaji nchini.
Nadhani
wakati umefika sasa watengenezaji wa filamu na wadau wote wa tasnia hiyo wakaanza
kuandaa filamu zenye maslahi mapana ya
taifa, kuhusu masuala mbalimbali mfano historia ya nchi, maisha ya viongozi
mbalimbali kama vile Mama Getrude Mongella namna alivyowakilisha nchi katika
Mkutano wa Beijing mwaka 1990, ukombozi wa bara la Afrika na mambo kadha wa
kadha.
Hapo
bondeni (Afrika ya Kusini) wameandaa filamu kuhusu maisha ya baba wa taifa lao
Mzee Nelson Mandela, Marekani wao na filamu zao kama za Barrack Obama, Ton Braxton, Black Panther na ile ya The White house.
Nafahamu kuwa wametuzidi kwa teknolojia na taaluma kuhusu uandaaji wa filamu
lakini bado naamini hata sisi tuna ubunifu na tunaweza kuandaa filamu zetu kwa
teknolojia yetu, mazingira yetu na ubunifu wetu.
Ndugu
zangu wa Bongo movie, baada ya kusoma makala hii pengine mtataharuki mkidhani nimewachana kwa ubaya,
la hasha! Hakika dhamira yangu ni kuona filamu zetu zinakuwa zaidi ya kuonesha
mapenzi na hadithi za kawaida sana. Hakuna ubaya hata kidogo mki-act kuhusu historia ya nchi yetu.
Nchi
imepitia matukio mbalimbali,lakini katika filamu zetu kwa kiasi kikubwa maudhui
ni yale yale tena utakuta mwanamke wa kijijini eti amevaa wigi, kucha ndefu
mithili ya chui, rangi ya mdomo imekolea utadhani ametoka kuchinja kuku kwa
mdomo!
Kijana
wa kiume mwenye mkorogo, hereni masikioni achilia mbali tattoo zilizomjaa mikononi na miguuni. Kuhusu lugha,hapa nako
kunavioja vyake kede kede. Si ajabu wengi wenu
mmewahi kuangalia filamu ya
Kiswahili lakini jina (tittle) lake
limeandikwa kwa lugha ya kingereza. Hebu tujiulize, ni nani amewahi kuangalia
filamu ya kihindi yenye jina (title) lililoandikwa kispaniola? Mmeona wapi?
Kuhama
kwa COSOTA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo kutaakisi mabadiliko yanayohitajika kulingana na
wakati uliopo. Ni wazi kuwa watanzania wakiwemo wasanii bado wana majonzi kufuatia
kifo cha Mzee Mkapa kutokana na jinsi alivyowaondoa katika unyanyasaji,na
dhuluma kwa kuibiwa kwa kazi nyingi walizokuwa wakizifanya kwa jasho lao.
Leo
hii watanzania, hususan wasanii wa Bongo movie jiulizeni ni kitu gani cha
msingi zaidi ambacho mnakifanya katika kumuenzi Mzee Mkapa? Ni wazi kuwa
aliwajali na kuazisha COSOTA ili iwasaidie kulinda kazi zenu sambamba na
kuongeza thamani ya vipaji mlivyonavyo ili muweze kupata fedha zitakazowasaidia
nyinyi na familia zenu.
Nilisikia
na kuona wanamuziki mbalimbali wakiimba nyimbo kuhusu masuala kadha wa kadha
aliyoyafanya Mzee wa Uwazi na Ukweli ndani na nje ya urais wake, huenda ilikuwa
sehemu muhimu ya kuomboleza wakati wa
msiba wake.!
Niwakumbushe
tu kuwa na nyinyi mnawajibu wa kuvikumbusha vizazi vya sasa na vijavyo kuwa
taifa hili lilipata kuwa na bahati ya kuongozwa na Mzee Benjamin William Mkapa
kwani mchango wake katika maendeleo ya taifa hauna kifani. Nasisitiza alikuwa
kiongozi adhimu katika taifa hili na hakika ameacha alama itakayoishi milele.
Nafahamu
baadhi yenu mtasema kuandaa filamu si sawa na kuandaa muziki, kwa vile filamu
inahitaji muda zaidi, ujuzi na raslimali za kutosha ikiwemo fedha. Ni kweli na
sahihi kabisa, lakini ni lazima tujiulize kuwa pamoja kutokea matukio mbalimbali
katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 tangu Uhuru wa nchi hii sekta ya filamu
imeweza kuandaa filamu yenye taswira ya nchi ambayo ni urithi kwa vizazi
vijavyo na kuitambulisha nchi kimataifa?
Ni
wakati sasa mshirikiane na Vyuo Vikuu vinavyotoa taaluma ya sanaa ili kutoa
mchango wenu katika taifa. Natambua kuwa wengi wenu ni wasomi tena wenye vipaji.
Ni matarajio ya wengi kuona namna mnavyoweza
kutumia wasifu na muonekano wenu kwa kuigiza maisha ya mtu kama vile Mzee Mkapa
ili kusadifu wasifu wake kwa kutoa mafunzo mbalimbali katika jamii, na hata
kufundisha watoto na vijana kuhusu uzalendo.
Kwa
namna hiyo najua mtauza filamu zenu na kupata fedha nyingi na muhimu zaidi mtauza historia ya nchi kitaifa na kimataifa
na itakuwa such a beakthrough.
Nchi
ina matukio mengi yanayoweza kuitangaza Tanzania kimataifa yapo mengi na mazuri
ya kujifunza kutoka hapa sio kila kitu kizuri kinatoka ulaya. Kuna historia ya viongozi
mashujaa kama vile Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Mtemi Mkwawa, Bibi Titi Mohamed, Rais Dkt. John
Pombe Magufuli, vilevile kuna rasilimali hadhimu mfano Mlima Kilimanjaro, hata
kama mmeshindwa kuigiza kwenye filamu zenu kuhusu mlima huu mrefu zaidi barani Afrika
basi hata kuutaja kwenye filamu zenu mnashindwa, hapana!
Utadhani
ni dhambi, ahhaa... jamani tutasubiri
tena hadi Sterve Harvey akosee kuutaja kama Mlima Kilimanjaro uko nchini
Tanzania kisha Waziri wa Mali Asili na Utalii apiganie kuueleza ulimwengu kuwa mlima
huo uko Tanzania na sio kwa jirani?
Katika
hafla ya makabidhiano ya COSOTA yaliyofanyika Julai 15, 2020, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi anasema kuwa taasisi hiyo imejipanga kutekeleza majukumu yake kwa ari mpya na tija katika
shughuli za sanaa nchini, sambamba na kuandaa mafunzo maalum ya uandishi wa script ili kuongeza ubora wa filamu.
“Filamu
inaonesha mtu anatembea kwa dakika kumi, ili tu filamu ifikishe series mbili au tatu, mnatuchosha
watazamani, nataka tuwe na mafunzo ya muendelezo kuhusu uandishi wa script, picha jongefu na picha mnato”
anasema Dkt. Abbasi
Niwakumbushe
tu kuwa Tanzania ni nchi ya pili ikitanguliwa na Nigeria kwa uzalishaji wa
filamu nyingi katika bara la Afrika. Aidha, tuna uwezo wa kutengeneza filamu
zenye ubora zaidi kwa kutumia teknolojia iliyopo. ukitazama filamu
zinazotengenezwa na mwanamama kutoka nchini Nigeria Mo Abudu kama ile ya The Royal Hibiscus hotel na The Wedding party, utashangazwa na maudhui
pamoja na ubora wa filamu hizo, tena kutoka Afrika. iweje watayarishaji wa
filamu kutoka Tanzania washindwe?
Nafahamu
kuwa filamu bora zinahitaji uwekezaji kuanzia hadithi hadi mandhari za kuvutia,
lakini siamini kuwa bila kutengeneza mji maalum kwa ajili ya filamu kama ilivyo
Hollywood
au Bollywood basi haiwezekani kutengeneza filamu zenye ubora na
zitakazovutia soko la kimataifa, si kweli!.
Nchi
hii imekuwepo na wanasiasa maridhawa, wanamichezo hodari, wanamuziki mahiri,
waandishi wakongwe, utamaduni, raslimali adhimu, mila na desturi kutoka
takribani makabila 150 iweje katika miaka zaidi ya 50 ya Uhuru sasa tushindwe
hata kuwa na filamu bora zinazoitambulisha Tanzania huko duniani!
Nafahamu
itahitaji miaka kadhaa ili kuandaa movies made from the real lives mfano
filamu ya Princess Diana, lakini
tunaweza kuanza na zile za kabila la wahehe, wahaya, wachaga, wapogolo na
wengine, pengine namna shughuli za jando zinavyofanywa ama urithi wa uongozi wa
kijadi na nyinginezo.
Hivi
karibuni Serikali imeanza utekelezaji wa mipango madhubuti inayolenga kuleta
mapinduzi ya sekta ya filamu nchini.
Kaimu
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Kiagho Kilonzo anasema kuwa Serikali
imeanza kutekeleza mbinu mbalimbali ili kuboresha filamu zinazozalishwa nchini
kwa lengo la kufikia soko la kimataifa na kukuza wigo wa ajira nchini.
“Bodi
imeanza kukutana na waandaaji wa filamu katika vikao maalumu ambapo tunapitia filamu
kwa pamoja na kutoa maoni yanayolenga
kuboresha filamu husika na baadae filamu
zenye ubora zaidi zinawasilishwa kwenye kumbi za sinema, lengo ni kuongeza
ushindani na kuzalisha filamu bora zaidi” anasema Dkt. Kilonzo
Dkt.
Kilonzo anataja mkakati mwingine kuwa kuunda kamati maalum itakayosaidia
kufuatilia vigezo vya filamu zinazoweza kushiriki tuzo za kimataifa za Oscar
ili pia filamu za kitanzania zianze kushiriki tuzo hizo.
Sekta
ya filamu inatajwa kuzalisha ajira kwa kiasi kikubwa, ambapo filamu moja
inaweza kuzalisha ajira kwa watu 150
hadi 200, ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Agosti, 2020 tayari sekta hiyo
imezalisha filamu 26 ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na filamu saba tu
zilizotengenezwa mwaka 2019.
Fauku
ya hayo, Bodi ya Filamu imepokea jumla ya filamu 700 kwa ajili ya ukaguzi kabla
ya filamu hizo kusambazwa kwa watazamaji Swali linabaki kwa Bongo movies, je mtaendelea
kuongoza katika uzalishaji wa filamu nyingi Afrika ama mtaanza kuzalisha filamu
zenye ubora wa viwango vya kimataifa zenye kuakisi historia ya nchi yetu, watu
wetu, utajiri na raslimali zetu na mila na desturi zetu?
No comments:
Post a Comment