Habari za Punde

PROF. MSANJILA ASHUHUDIA KILO 2,271 YA MADINI YA BATI IKIUZWA

 

Katibu Mkuu Wizara Madini Prof. Simon Msanjila akisaini Kitabu katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akieleza jambo kwenye Mkutano uliofanyka katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.
Baadhi ya washiriki walioshiriki Mkutano wa Katibu Mkuu Wizara Madini Prof. Simon Msanjila katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof.Simon Msanjila ameshuhudia biashara ya Madini ya Bati (Tin) ikifanyika ambapo Shirika la Taifa la Uchimbaji Madini (STAMICO) likifanya manunuzi Kilo 2,271 ya Madini ya Bati yenye thamani ya shilingi Milioni 34 kutoka kwa Wachimbaji Wadogo.

Katika ziara yake hiyo, Prof. Msanjila alitembelea Soko la Madini la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera na kuzungumza na Wachimbaji Wadogo pamoja na Wafanyabiashara wa Madini hayo.

Aidha Prof. Msanjila amewataka wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara wa Madini ya Tin kulitumia Soko la Kyerwa kuuzia Madini yao ili wanapotaka mkopo kutoka benki inakuwa rahisi kwa Wizara kudhibitisha mauzo yao kwa kuwa yatatambuliwa kwenye mfumo wa Wizara.  

Pia Prof. Msanjila amewasihi Wachimbaji Wadogo na wafanyabishara wa Madini ya Bati kufungamanisha biashara ya madini na chumi zingine kama kilimo, ufugaji n.k. ili kujiongezea wigo wa fursa zitokanazo na Sekta ya Madini.

Katika ziara hiyo yenye lengo la kuhakikisha Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera limeanza kufanya kazi, Prof. Msanjila aliambatana na viongozi Mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu.

Vile vile, Prof. Msanjila amewasisitiza wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara wa Madini ya Bati kuongeza juhudi za uzalisha wa madini hayo kwani Soko la uhakika kwa sasa linapatikana na kuwataka kuepuka utoroshaji wa madini hayo.

Pia, Prof. Msanjila maipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kyerwa kwa ushirikiano na uzalendo waliouonesha katika kulinda Rasilimali Madini kwa manufaa ya Nchi.

“Mwaka jana mwezi wa pili Tanzania tulifanikiwa kupata Cheti cha Uhalisia wa Madini ya Bati ambapo Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa alikizindua cheti hicho hivyo, tuongeze juhudi kuzalisha Madini kwa wingi na kuyaongezea thamani na hatimaye tuyapeleke nje ya nchi tukawauzie”, alisema Prof Msanjila.

Wakati huo huo, Prof Msanjila alisikiliza kero na changamoto za Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Bati pamoja na Wafanyabiashara wa madini hayo na kuyatolea majibu papo hapo.

Pamoja na mambo mengine Prof. Msanjila alitembelea Viwanda vya kuchakata Madini ya Bati kikiwemo Kiwanda cha African Top Mineral Limited pamoja na Tanzplus ili kujionea shughuli za uongezaji thamani katika viwanda hivyo zinavyo fanyika.

Prof. Msanjila amewataka wanunuzi wa Madini ya Bati kuwalipa fedha zao Wachimbaji Wadogo kwa wakati na kuepuka usumbufu wa kuwacheleweshea malipo yao.

Aidha, Prof. Msanjila amewataka Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara ya Madini ya Bati kupendana, kuthaminiana na kuachana na mambo ya majungu ili waongeze tija kwenye shughuli yao ya uchimbaji madini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu alimpongeza Katibu Mkuu kwa ziara yake hiyo ambayo imesaidia kuondo changamoto za Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiasha wa Madini ya Bati ambayo yalidumu kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.