Na.
Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imeendelea
kuboresha sekta ya madini ili kukabiliana changamoto zinazoikabili sekta hiyo hatua
itakayosaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato nchini.
Akizungumza leo
jijini Dodoma wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Serikali ina
matarajio makubwa katika sekta ya madini na ndiyo maana ilirekebisha Sheria ya
Madini ya mwaka 2010 ili kuongeza tija.
“Nina imani Baraza
mtajikita kujadili namna ya kuipeleka mbele sekta ya madini kwa vile mwaka 2025
sekta hii inatarajiwa kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa,
Vilevile Serikali
inaiwezesha Tume ya Madini kwa mategemeo kwamba makusanyo yataongezeka na
wananchi watashirikishwa ili sekta iweze kuimarika zaidi” alisema Prof.
Msanjila.
Aliongeza kuwa, lengo
la Baraza hilo la Wafanyakazi ni kutoa mchango na ushauri wa namna bora ya wafanyakazi
kushirishirikiana na viongozi wa Tume ya Madini katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya taasisi na nchi kwa
ujumla.
Naye, Mwenyekiti wa
Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alikitaka Chama cha Wafanyakazi wa
Serikali Kuu na Afya (TUGHE) tawi la taasisi hiyo kutafuta njia muafaka za
kutatua matatizo ya wafanyakazi kwa kushirikiana na menejimenti ya Tume ili
kutunza taswira ya taasisi hiyo na kuongeza tija katika sekta ya madini nchini.
Aidha, Prof. Kikula
aliongeza kuwa Tume hiyo imeendelea kuimarisha sekta ya madini nchini na kuhakikisha
Serikali inapata mapato endelevu na kuvuka malengo ya makusanyo ambayo
yaliyowekwa mwaka hadi mwaka.
“Mwaka 2018/2019 zilikusanywa
shilingi bilioni 346.78 na kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 310.32 ambazo
ni sawa na asilimia 111.59 na mwaka 2019/2020 jumla shilingi bilioni 528.24
zilikusanywa na kuvuka lengo la shilingi bilioni 470.35 ambazo ni sawa na
asilimia 112” alisisitiza Prof. Kikula.
Mafaniko mengine ya Tume hiyo ni uanzishwaji wa masoko
28 na vituo vya ununuzi wa madini 28 pamoja na kupungua vitendo vya utoroshwaji
wa madini ambapo mwaka 2018/2019 madini yenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.72 na shilingi bilioni
27.66 yalikamatwa kutoka maeneo mbalimbali nchini yakiwa yanatoroshwa.
Katika hatua
nyingine, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alisema
kuwa Tume ya Madini imepanga kuendesha zoezi la uhakiki wa leseni zote za
madini kwa muda wa miezi miwili na kuzifuta leseni ambazo hazitakuwa
zimehakikiwa.
“Zoezi la kuhakiki
leseni za madini linaanza leo Septemba 3, 2020 hadi Novemba 02, 2020, mambo ya
msingi yatakayo hakikiwa ni uhalali wa leseni na leseni ambazo hazijaendelezwa
wala kulipiwa ada ya mwaka zitafutwa kwa mujibu wa sheria” alisema Prof. Manya.
Prof. Manya aliongeza
kuwa Tume hiyo inawataarifu wamiliki na waombaji wa leseni za utafutaji na
uchimbaji wa madini kurekebisha mapungufu ya maombi yao ndani ya kipindi cha siku
30, ambapo maombi yaliyopo ya wachimbaji wa kati ni leseni 15 na maombi 96 ya
leseni za utafutaji madini.
Fauka ya hayo, Maafisa
Madini Wakazi wametakiwa kuanzisha dawati la uhakiki wa leseni za madini katika
ofisi zao ili kuwapunguzia adha wateja wao hatua itakayosaidia kupunguza usumbufu
wakati wa kuhakiki leseni zao.
Wizara ya Madini
tayari imekamilisha utungaji wa kanuni za uongezaji thamani madini za mwaka
2020, ambazo zitatumika kusafirisha madini yaliyoongezwa thamani nje ya nchi
kwa mujibu wa kanuni hizo.
No comments:
Post a Comment