Na.Beatrice Sanga-MAELEZO
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ipo kisheria
kwa mujibu wa Katiba chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977, na lengo lake ni kuratibu na kusimamia uendeshaji Uchaguzi wa
Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.
Kupitia uandikishaji wa wapiga Kura, ugawaji wa majimbo na utoaji
wa elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la
kuimarisha demokrasia, NEC inatekeleza wajibu huo ili kuwawezesha wananchi
kufanya zoezi la kuchagua viongozi wao.
Katika
kutekeleza majukumu yake ya kila siku NEC ina mfumo wa uchaguzi unaotumika
katika kuchagua Rais, Wabunge
na Madiwani, ambapo mgombea anayepata kura nyingi na halali kuliko wenzake
ndiye hutangazwa kuwa mshindi. NEC pia hutoa miongozo na taratibu mbalimbali za
uchaguzi ili kuweza kufanikisha suala zima la uchaguzi.
Tunapoelekea
katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 28,Oktoba,2020 ni muhimu
sana Watanzania na wapiga kura wote wakapata elimu itakayo waongoza katika
kufanikisha mchakato mzima wa kupiga Kura, kuwaelimisha wananchi kuhusu mambo
ya msingi yatakayowawezesha kutekeleza
jukumu hilo la kikatiba ambalo litafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Wananchi
wanapaswa kujua na kupewa elimu ya nani anaruhusiwa kupiga kura, wapi anaweza
kupiga kura, kituo cha kupigia kura, muda wa kupiga kura, mambo muhimu ya
kuzingatia kabla ya kupiga kura na jinsi ya kupiga kura. Hii itawawezesha wananchi kuwa na uelewa mpana utakao wasaidia
wakati wa kutekeleza zoezi la upigaji kura.
Ibara
ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania inampa haki kila raia
aliyetimiza miaka 18 kupiga kura.
Kwa mujibu wa vifungu vya 13(1), 13(2),
35C, 61 (3)(a) na 63(1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na
kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani), Sura ya 292, ili mtu aweze kupiga kura na
kumchagua kiongozi anayemtaka ni lazima awe amejiandikisha katika Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura na kuwa na kadi ya mpiga
kura iliyotolewa na NEC.
Aidha, mwananchi anatakiwa kuwepo katika kituo
alichojiandikishia kwa sababu ndipo jina na taarifa zake zitakapoonekana.
Katika maeneo na vituo mbalimbali vya kupigia kura, Tume itabandika orodha ya
majina ya wapiga kura ili kila mwananchi aweze kujua ni kituo gani atapigia kura,
hata hivyo kwa sintofahamu yoyote ambayo mtu anaweza kuipata kutakuwa na makarani
waongozaji katika kila kituo cha kupigia kura ili kuwasaidia wapiga kura kutambua
vituo vyao na mambo muhimu kuhusu mchakato mzima wa kupiga kura.
Hata
hivyo mpiga kura anatakiwa kufika kituoni
katika muda uliotangazwa ambapo kwa
mujibu wa NEC, siku ya uchaguzi vituo vyote vya kupigia kura vitakuwa wazi saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi
kamili jioni kwa Tanzania Bara. Kwa
upande wa Tanzania Zanzibar, vituo vitakuwa wazi kuanzia saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja kamili jioni.
Muda huo ukiisha hakuna mtu atakayeruhusiwa
kuingia kwenye mstari kwa ajili ya kupiga kura.
Kila
raia anapaswa kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi ili
kuweza kuepuka sitofahamu yoyote inayoweza kujitokeza katika kituo cha kupigia kura na kufanya mtu
kukosa haki yake ya msingi ya kumpigia kura kiongozi anayemtaka. Aidha NEC inapaswa kuendelea kutoa Elimu, kuratibu
na kusimamia watu wanaotoa elimu hiyo ya uchaguzi kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi , Sura ya 343, na Sheria ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292.
Tanzania
inafanya uchaguzi wa sita tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza kutumika. Vyama
vilivyochukua fomu kwa ajili ya kugombea kiti cha Urais in 17 ambapo vyama
vilivyoteuliwa na NEC kugombea nafasi hiyo ni 15. Wagombea wa vyama viwili
walienguliwa na Tume kutokana na kutokidhi vigezo. Jumla ya wapiga kura
29,188,347 wamejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo
80,155 vitatumika katika shughuli ya kupiga kura.
No comments:
Post a Comment