Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Ameagwa na Wafanyakazi wa Ofisi Yake ya Faragha Ikulu Jijini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Wafanyakazi wa Ofisi yake ya Faragha wakati wa hafla ya kumuaga iliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee na Katibu wa Rais Ndg. Haroub Shaib na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Issa Haji Gavu na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na MBLM Ndg Salum Maulid. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Ofisi yake ya  faragha baada ya kumaliza mazungumzo  na chakula cha mchana wakati wa kuagana nao hafla hiyo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar.  


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo ameagana na wafanyakazi wake wa Ofisi yake ya Faragha na kuwapongeza kwa kushirikiana nae kwa muda wote wa miaka kumi ya uongozi wake.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar wakati akiwapongeza na kuwaaga wafanyakazi wake wa Ofisi ya Faragha ya Rais pamoja na kula nao chakula maalum cha mchana.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliwapongeza wafanyakazi hao kwa kufanya kazi nae vyema katika kipindi chote cha miaka kumi ya uongozi wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha, Rais Dk. Shein aliwataka wafanyakazi hao kuendelea kuwa watii, waaminifu na wavumilivu hasa ikizingatiwa kwamba ofisi wanayoifanyia kazi  ni ofisi maalum kwa umhimu wake.

Nao wafanyakazi wa Ofisi ya Faragha ya Rais kwa upande wao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwaongoza vyema, kuwalea na kufanya kazi kwa wema na kwuavumilia katika kipindi chake chote cha miaka kumi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Wafanyakazi hao walieleza kuwa wamefarajika kwa kiasi kikubwa na uongozi wa Rais Dk. Shein ambao umewafanyia mambo mengi wananchi wote wa Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo jambo ambalo Rais Dk. Shein ameacha alama.

Sambamba na hayo, wafanyakazi hao walieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika miaka kumi ya uongozi wa Rais Dk. Shein na wao wanaona faghari kwamba mafanikio hayo yamepatikana na wao wakiwa ni sehemu ya wasaidizi wa Rais.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.