Habari za Punde

Ufunguzi wa Jengo Jipya ya Ofisi ya Rais Pemba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia katika hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Chakechake Pemba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapainduzi Dk. Ali Mohamed Shen amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba, kufanya kazi kwa bidii na kuongeza kasi na ari ya utendaji kwani Ofisi hiyo ina heshima ya pekee.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi iliyopo Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa nyumba za Ikulu huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

 

Rais Dk. Shein aliwataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kuendelea kulinda hadhi na heshima ya Ofisi hiyo na kuwataka kuendelea kushirikiana huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kazi wafanyakazi wake wote.

 

Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi ya Rais na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ukiongozwa na Waziri Issa Haji Gavu kwa kusimamia vizuri kazi za ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika na leo kuzinduliwa.

 

Pia, aliwapongeza wakandarasi wazalendo na kutumia fursa hiyo kumpongeza Msanifu wa Majengo ambaye pia, ni Meneja wa Majengo Ikulu Mohamed Abdulrahman Machungwa pamoja na Ramadhan Mussa Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) ambayo ndio iliyojenga jengo hilo.

 

Alisema kuwa nyumba za eneo hilo la Ikulu zilikuwa zimechakaa sana na ndipo ndani ya mika kumi iliyopita Ofisi hiyo ilianza kazi ya kuzifanyia ukarabati na nyengine kuzijenga upya.

 

Alisema kuwa kwa upande wa Pemba Ofisi hiyo imefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha Ikulu ya Mkoani, kujenga Ikulu ya Micheweni pamoja na nyumba za Ikulu za eneo hilo na jengo hilo jipya la Ofisi lililozinduliwa hivi leo.

 

Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba majengo yote hayo yamejengwa kwa fedha za Serikali pamoja na yale yote aliyoyazindua hivi karibuni zikiwemo nyumba za Kwahani, Maduka ya biashara Michenzani, nyumba za Mbweni pamoja na ofisi kadhaa za Serikali zikiwemo zile za Gombani Pemba.

 

Alisisitiza haja ya kutunzwa kwa jengo hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu na kuwataka wafanyakazi waharakishe kuhamia ili kuanza kazi huku akisisitiza kuwa thamani mpya zitaingizwa hapo baadae na hivi sasa watumie walizonazo.

 

Alieleza kuwa lengo la kujenga ofisi mpya na nzuri ni kwa ajili ya kuwapatia wafanyakazi maeneo mazuri ya kufanya kazi na kuwaweka katika mazingira bora ya kazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

 

Alisema kuwa hatua hiyo itawapelekea wafanyakazi kuridhika kwani iwapo wafanyakazi wataridhika ndipo wataweza kufanya kazi vyema.

 

Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuyatunza na kuyalinda mazingira na kueleza kwamba kila mmoja ana jukumu la kulitunza na kulienzi jengo hilo na kutaka majengo yote ya Ikulu yaendelezwe na yatunzwe.

 

Alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Wakala wa Nyumba na Majenzi, Shirika la Nyumba pamoja na kuanzisha Kampuni ya Majenzi ya Serikali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza gharama za ujenzi kwa majengo ya Serikali.

 

Alisema kuwa uzoefu wa Serikali kujenga majengo yake wenyewe unatokana na uzoefu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani karume ambapo katika uongozi wake majengo mengi yalijengwa kwa gharama za Serikali.

 

Alitumia fursa hiyo kuwaongeza wafanya kazi wote wa Ofisi ya Rais wa Unguja na Pemba pamoja na wale wote waliowahi kufanya kazi katika Ofisi hiyo na hivi sasa wamehamishiwa Ofisi nyengine.

 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa maelekezo yake mbali mbali pamoja na miongozo yake katika kuhakikisha ujenzi unafanyika vyema katika majengo yote ya Ikulu za Pemba, Unguja, Dar es Salaam na Dodoma.

 

Waziri huyo alitoa shukurani kwa mashirikiano makubwa yaliyofanyika katika ujenzi huo na kumpongeza Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi kwa mashrikiano yake pamoja na Maafisa Wadhamini wote walioshiriki.

 

Alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kuelekeza na kuhakikisha kuwa jengo hilo linakamilishwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein.

 

Mapema katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Salum Maulid Salum alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kutia shime ya kujienga jengo hilo na kulimaliza kwa wakati.

 

Aidha, maamuzi ya ujenzi wa jengo hilo yanaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2015-2020.

 

Aliongeza kuwa matayarisho ya ujenzi wa jengo hilo yalianza mwezi Novemba 2018 ambapo Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) walilikagua eneo hilo kimazingira ili kuhakikisha hawaharibu mandhari ya eneo hilo ambalo asili yake lipo katibu na ufukwe wa bahari.

 

Vile vile, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Wakala wa Majengo walichukua sampuli ya udongo wa eneo hilo kwa ajili ya vipimo.

 

Alisema kuwa michoro ya awali ya jengo hilo ilitayarishwa na Msanifu wa Majengo Ikulu Mohamed Abdulrahman maarufu Machungwa ambae pia ni Meneja  wa Majengo Ikulu ambapo michoro hiyo baadae iliimarishwa na Wakala wa Majengo baada ya makubaliano na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

 

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa jengo hilo lina eneo la mita za mraba 654(sqm) ambapo kutokananna hali ya udongo wa eneo hilo msingi wa jengo una urefu wa mita 2na  umeongezwa nguvu ya zege na nondo zilizolazwa kwa mfano wa kiatu cha kusimamia jengo.

 

Alisema kuwa sehemu ya chini ya jego hilo lina vyumba vya Ofisi saba, ukumbi wa mkutano na ukumbi wa kusalia wageni ambapo pia kuna huduma za kutosha zikiwemo mazingatio ya watu wenye ulemavu.

 

Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu, sehemu ya juu ina vyumba sita vya Ofisi, ukumbi mkubwa wa mikutano na ukumbi wa kusubiria wageni ambapompia jengo hilo limezingatia masuala ya usalama wa moto kwa watumiaji wake na limezingatia masuala ya usalama wa moto kwa watumiaji wake na limewekewa njia ambazo ni rahidi kutumika wakati wa uokozi.

 

Alisema kuwa jengo hilo litakuwa na ‘lift’ ambayo hivi sasa ipo katika matengenezo na inategemewa kuwekwa baada ya wiki 15 ambapo jengo hilo linaweza kuongezwa ghorofa mojaa ya ziada kwa matumizi ya baadae.

 

Sambamba na hayo, alisema kuwa gharama za jengo hilo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndio iliyotoa fedha za ujeni huo ambapo iliingia mkataba na Wakala wa ujenzi kulijenga kwa TZS 528,465,875.

 

Gharama nyengine za nyongeza ni ya kuweka lift na vifaa vyengine kama vile vipoza hewa pamoja na vifaa vya umeme na vya kuzimia moto vitagharimu TZS 77,400,000.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.