Habari za Punde

DKT. MPANGO AHIMIZA KILIMO CHA KISASA KIGOMA

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiagana na wakazi wa Kata ya Kilelema, baada ya kuwashukuru kwa kumchagua kwa kishindo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na yeye binafsi kwa kura za kishindo wakati wa Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.
Waziri wa Fedha na Mipango (Mb), akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa Bw. Agustino Gwamama kwa niaba ya kikundi cha vijana cha Bodaboda-Kilelema, alipotembelea Kata ya Kilelema mkoani Kigoma, ambapo aliwaahidi vijana hao kuhakikisha asilimia 10 ya mikopo ya Halmashauri kwa vijana waliojiunga kwenye vikundi inawafikia.

Na Josephine Majura - Kigoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, amewataka wakazi wa mkoawa Kigoma kujishughulisha na kilimo cha mazao ya kimkakati na kutumia vema soko linalopatikana ndani ya nchi pamoja na nchi jirani ya Burundi kujipatia kipato ili kuondokana na umasikini.

Dkt. Mpango ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, ametoa rai hiyo alipotembelea Kata za Kilelema, Muyama na Kasumo, Wilayani Buhigwe, kuhamasisha shughuli za maendeleo na kuwashukuru wananchi kwa kumchagua Mhe. Dkt. John Magufuli, kuwa Rais wa Tanzania na yeye binafsi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa kura za kishindo.

Dkt. Mpango aliwashauri wananchi hao kujihusisha na kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo kilimo cha parachichi, mawese, tangawizi, kilimo cha mbogamboga na matunda na kwamba Serikali kwa upande wake itapeleka mbegu za kisasa ili kuwa na uzalishaji wa mazao wenye tija.

Aidha, Dkt. Mpango amewahimiza wakazi wa mkoa wa Kigoma kuhakikisha wanalinda amani, usalama na utulivu wa nchi kwa nguvu zote ili wananchi waendelee kujiletea maendeleo yao katika nyanja mbalimbali za kiuchumi katika mazingira ya amani na utulivu.

Aliwaahidi wananchi wa kata hizo za Kilelema, Muyama na Kasumo kwamba, ahadi zote alizo ahidi wakati wa kampeni kwenye sekta ya elimu, maji, afya, nishati, ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na kuendeleza kilimo, zitatekelezwa kwa awamu katika kipindi cha miaka 5 ijayo.

Akimkaribisha kuongea na wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma, Kanali Michael Ngayalina, alimwomba Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili wilaya yake kwa upande wa maji, barabara, soko la kimataifa pamoja na suala la elimu.

Kanali Ngayalina alieleza mikakati mbalimbali iliyopo ya kukabiliana na changamoto ya maji kwamba Serikali inatekeleza mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 2.8 utakao pita katika vijiji vya Migongo na Kilelema pamoja na ujenzi wa daraja la Mto Malagarasi litakaloiunganisha wilaya yake na nchi jirani ya Burundi, ikiwa ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kabingo mpaka Manyovu.

Katika ziara yake, Dkt. Mpango, ametembelea Kata nane kati ya ishirini zilizopo kwenye Jimbo lake la Buhigwe mkoani Kigoma, ambapo ametembelea Kata za Munanila, Mwayaya, Munzeze, Janda, Bukuba, Kilelema, Muyama na Kasumo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.