Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais Mstaaf wa Awamu ya Saba Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Aongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa  Chama Cha Mapinduzi Mhe,.Dk.Ali Mohamed Shein akifungua Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, kilichofanyika katika ukumbi wa Afisi Kuu  ya CCM Kisiwanduyi Jijini Zanzibar na (kulia kwake) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdalla.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein,amewataka viongozi na wanachama wa CCM kuendelea kuwa wamoja katika kulinda na kutetea maslahi ya Chama.

Rai hiyo aliitoa leo wakati akifungua Kikao cha kawaida cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar, kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Dk.Shein, alisema kuwa pamoja na ushindi mkubwa wa CCM uliopatikana hivi karibuni kupitia uchaguzi Mkuu wa dola wa mwaka huu, wanachama na viongozi wa chama wanatakiwa kuwa wamoja ili chama kiendelee kuwa imara zaidi.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimepokea na kujadili mapendekezo ya Wana CCM walioomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar mwaka 2020/2025.

Katika hatua ya kuwania nafasi hiyo jumla ya Wana CCM wapatao wawili walijitokeza kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea kuteuliwa nafasi ya Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambao ni Ndugu Mgeni Hassan Juma na Ndugu Mwanaasha Khamis Juma.  

Kikao cha kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa cha novemba 05,mwaka 2020 kilichofanyika Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli , pamoja na mambo mengine kiliamua kukasimu kwa kamati maalum kufanya uteuzi wa mwisho kwa wana CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Akizungumza katika kikao hicho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, alisema ataendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa kama alivyoahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita hivi karibuni.

Katika maelezo yake Dk.Hussein, aliwasihi wajumbe wa kikao hicho kumshauri na kutoa maoni yao juu ya utendaji wake ili aende sambamba na kasi ya maendeleo nchini.

Aidha, alipongeza uamuzi wa CCM kupitia kamati kuu kwa kutoa agizo la viongozi waliohudumu kwa kipindi kilichopita kwa nafasi ya Unaibu Spika wapitishwe ili kuepuka mipasuko ndani ya Chama.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye pia ni Makamu wa Pili mteule wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah, aliwashukru wananchi kwa maamuzi yao ya kuwachagua kwa kura nyingi viongozi waliopeperusha bendera ya CCM kupitia uchaguzi mkuu uliopita.

Pamoja na hayo alimshukru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kumuamini na kumteua ili amsaidia majukumu ya kiutendaji kupitia nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

''Nami naungana na msimamo wa Rais wetu Dk.Hussein kuwa tumeaminiwa na wananchi na kutupa ridhaa ya vuongozi ili tuwatumikie kwa vitendo ili wanufaike na rasilimali za nchi'', alisema Hemed.

Sambamba na hayo alisema kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka huu ni matayarisho ya uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2025.

Kikao hicho cha kawaida kimefanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017 ibara ya 109 (1), (3),(6) (a) -(d).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.