Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais, Mhe Hemed atembelea Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mh. Hemed Suleiman Abdalla Kushoto akitembezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mh. Hamid Mahmoud Hamid alipofanya ziara ya kutembelea Tume hiyo hapo Maisara.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mh. Hamid Mahmoud akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed alipotembelewa Ofisini kwake Maisara.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar Nd. Thabit Idarous Faina akimpatia maelezo Mheshimiwa Hemed alipokuwa akikagua Kiwanja kinachotazamiwa kujenga Jengo Kuu la Ofisi hiyo hapo Maisara.
Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mh. Hamid Mahmoud Hamid wa kwanza Kulia akitoa neno la makaribisho wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akijiandaa kuzungumza na Uongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC}.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah akizungumza na Uongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar hapo Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi na Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar wakisikiliza nasaha za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar Nd. Thabit Idarous Faina akitoa maelezo ya uwajibikaji wa Tume ya Uchaguzi mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla.

 Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Nd. Mabrouk Jabu Makame akitoa neneo la shukrani mara baada ya kukamilika kwa Mkutano wa  Viongozi wa Tume hiyo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Hapo Maisara.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis , OMPR


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alisema wakati Watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} wanapaswa kujipanga kwa ajili ya matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Serikali Kuu inajipanga kuwapatia Jengo kubwa na la Kisasa litakalokidhi mahitaji kwa Watendaji wa Taasisi hiyo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alisema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar baada ya kufanya ziara fupi kwenye Majengo yao hapo Maisara na kuwapongeza kwa kusimamia Uchaguzi Mkuu uliomalizika kwa salama na Amani.

Alisema Serikali pamoja na Wananchi wameendelea kujenga Imani kubwa kwa Watendaji na Viongozi wa Tume ya Uchaguzi kutokana na  Kazi ya Kizalendo ya kuratibu Uchaguzi iliyokwenda kwa umakini mkubwa jambo ambalo Watendaji hao wanapaswa kupatiwa maeneo salama yatakayowapa utulivu wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“ Ipo haja kwa Serikali Kuu kuangalia Watendaji wa Tume ya Uchaguzi wanapata Jengo Jipya na kubwa litakalokidhi mahitaji ya Watumishi wake. Nafarajika kuona hatua ya kwanza ya upatikanaji wa eneo imeshakamilika”. Alisisitiza Mtendaji Mkuu huyo wa Shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 umemalizika baada ya Tume ya Uchaguzi kusimamia Sheria na Miongozo iliyopelekea hata wale waliolalamika kutokana na zoezi hilo kutokuwa na sababu za msingi zinazoeleweka.

Alisema Watendaji wa Tume ya Uchaguzi  wamesimamia vyema maamuzi ya Wananchi jambo lililowapatia Heshima kubwa na kuwapa faraja Wazanzibari walio wengi Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman aliwahakikishia Viongozi na Watendaji wa Tume hiyo kwamba Serikali itajitahidi kuchukuwa hatua za haraka katika kuona changamoto zilizowakabili zinapatiwa ufumbuzi unaostahiki.

Alisema Moja ya Malengo ya Serikali Kuu  ni kuendelea kujenga mazingira bora ya Kazi kwa Watumishi wa Taasisi zake za Umma ili yale mahitaji na huduma zinazostahiki zinawafikia Wananchi mahali popote.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwakumbusha Wananchi kwa vile Uchaguzi Mkuu tayari umemalizika hadi Mwaka 2025 waendelee kuheshimu Sheria za Nchi katika maisha yao ya kila Siku ambayo yanaendelea kuwepo baada ya Uchaguzi huo.

Akitoa Taarifa fupi Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar Nd.Thabit Idarous Faina alisema Elimu kwa ajili ya kupatiwa Wapiga Kura ambao ni Wananchi bado itaendelea kuwa jukumu la Tume ya Uchaguzi kwa Mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo Nchini.

Alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika siku chache zilizopita ikiwemo Gharama za Uchaguzi zilizokadiriwa kutumiwa shilingi Bilioni 9.6 zilipungua na kutumika Shilingi Bilioni 6.5 tu na matokeo yake kunusuru Shilingi Bilioni 2.4.

Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi Zanzibar alifahamisha kwamba licha ya Tume hiyo kuwa na matarajio ya kujenga Ofisi Kuu nyengine mpya lakini pia inaendelea kuimarisha Ofisi zake zilizoko Wilayani ili kupunguza usumbufu unaowakabli Watendaji wake.

Alisema Tume ya Uchaguzi hivi sasa inatumia baadhi ya Majengo ya Taasisi nyengine za Umma kama Ofisi zake ingawa tayari imeshafanikiwa kujenga majengo ya Kudumu kwa Ofisi zake za Wilaya ya Magharibi A Unguja na ile ya Micheweni Kaskazini Pemba.

Mkurugenzi Faina alifafanua changamoto ya Gari inayokwaza Utekelezaji wa majukumu yao ya Kazi za kila siku ambayo yameshachakaa baada ya kutumika kwa kipindi kirefu.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mh. Hamid Mahmoud Hamid alisema moja ya siri kubwa ya Taasisi hiyo inayosimamia Uchaguzi inatokana na Viongozi pamoja na Watendaji wake kufanya Kazi huku wakizingatia na kuheshimu Maadili yao.

Mheshimiwa  Hamid alisema licha ya baadhi ya changamoto zinazowakabili Viongozi na Watendaji wa Tume hiyo lakini bado anafarajika kuona Watumishi hao wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi Mkubwa.

Alisema katika kuona Watumishi hao wanaendelea kuwajibika ipasavyo Uongozi wa Taasisi yake unajitahidi katika kuona kila fursa ikiwemo maslahi yao yanajengewa mazingira stahiki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman  Abdalla ameanza ziara Maalum ya kuzitembea Taasisi na Idara zilizo chini ya Ofisi yake Wiki Moja tu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.