Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ametengua Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya Katika Wizara ya Afya Dk. Jamala Adam Talib.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya katika Wizara ya Afya Dk. Jamala Adam Talib na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Dk. Ali Salum Ali.

Kutenguliwa kwa uteuzi wa viongozi hao kunatokana na ziara aliyoifanya Rais Dk. Hussein leo (Novemba 18,2020) katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kwa azma ya kujionea mwenyewe hali ya utoaji wa huduma na changamoto zinazoikabili Hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee utenguaji huo unafuatia ziara hiyo aliyoifanya Rais Dk. Hussein na kupelekea kutenguliwa kwa viongozi hao kuanzia leo tarehe 18 Novemba, 2020 na kueleza kwamba watapangiwa kazi nyengine kwa mujibu wa taaluma zao.

Leo Dk. Mwinyi alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, na kuangalia utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika maeneo na vitengo  tofauti  vya Hospitali hiyo na kueleza kutoridhishwa na huduma zinazotolewa Hospitali hapo.

Katika ziara yake hiyo Dk. Hussein alitoa muda wa miezi mitatu kwa uongozi wa Wizara ya Afya kurekebisha kasoro za kiutendaji zinazosababisha kutokuwepo  ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Alisema kwa kiwango kikubwa mambo mengi yanahitaji kufanyiwa marekebisho, akibainisha kuwepo changamoto mbali mbali za kiutendaji na hivyo kuzorotesha uapatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Alisema analenga kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watendaji wasiowajibika kazini na kusababisha wananchi kulalamika kutokana na ukosefu wa huduma, pamoja na kupewa lugha zisizoridhisha kutoka kwa wauguzi na watendaji  wa Hospitali hiyo.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema pamoja na Serikali kuipatia fedha za kutosha Hospitali hiyo kila mwezi bado kumekuwepo changamoto za ukosefu wa vifaa muhimu kwa wagonjwa ikiwemo magodoro, dawa na vifaa vya maabara hivyo, akautaka Uongozi wa Hospitali hiyo kubadilika na kuondokana na utendaji wa mazowea.

Alisema pale Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na hatimae wagonjwa wakakosa dawa hizo, ni dhahiri kuwa kuna tatizo mahala hapo.

Alieleza kuwa kumekuwepo matatizo madogo madogo katika uendeshaji wa Hospitali hiyo na kubainisha  kuwa kama yangelishughulikiwa ipasavyo ni wazi kuwa huduma bora zingepatikana.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi , aliahidi kufanya ziara nyingine katika siku zijazo na kuzungumza na wafanyakazi kwa lengo la kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Alisema wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia wagonjwa kikamilifu sambamba na kupata haki wanazostahili.

Aliwataka madaktari na wauguzi kuvaa vitambulisho ili kuondokana na urasimu kwa wagonjwa ambao hatimae huzaa rushwa.

Katika ziara hiyo Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Hospitali, ikiwemo OPD  , MRI, Jengo la kuhifadhia Dawa, Kitengo cha Macho pamoja  na kusikiliza changamoto mbali mbali zinazokwamisha na kuzorotesha  utendaji kazi, sambamba na kuwajuilia hali wagonjwa, wakiwemo wale waliopata ajali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.