Habari za Punde

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi afanya ziara Bandarini

Mkurugenzi wa Bandari Nahat Mohammed Mahfoudh akitoa maelekezo kwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi  Rahma Kasim Ail (wa kwanza kushoto) kuhusu zoezi la uondoshaji wa Makontena
Waziri wa Mawasiliano  na Uchukuzi Rahma Kasim Ali akitembelea maeneo ya Bandarini kuangalia utendaji wa kazi 
Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe akielezea changamoto mbalimbali zinazoikabali Shirika la Meli  kwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,  Rahma Kasim Ali alipofanya ziara kutembelea eneo la Bandarini.
Waziri wa Mawasiliano  na Uchukuzi, Mhe Rahma Kasim Ali akitoa maagizo kwa wafanyakazi wa Shirika la meli mara Alipofanya ziara  katika meli ya Mapinduzi II.

 Waziri wa Mawasiliano  na Uchukuzi, Mhe Rahma Kasim Ali akizungumza na Waandishi mara baada ya kukamilisha ziara yake iliyoanzia Wakala wa Barabara Saateni na kumaliza Ghala la kuhifadhia mizigo Maruhubi.

PICHA ZOTE NA MAELEZO

Bahati Habibu Na Khadija Khamis,  Maelezo 

Waziri wa mawasiliano na uchukuzi Mhe Rahma Kassim Ali amesikitishwa na ubovu  wa mashine ya meli ya MV Mapinduzi II tokea iliponunuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea mwaka 2015.

Hayo ameyasema leo wakati alipofanya ziara ya kuzitembelea taasisi zilizomo chini ya wizara yake ikiwa ni agizo kutoka kwa rais alilolitoa wakati  akiwaapisha mawaziri ya kuwataka kuzifahamu taasisi na idara wanazozisimamia .

Amesema anasikitishwa na meli ya MV Mapinduzi II kushindwa kuendelea kwa shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa muda wa miezi miwili sasa na kila siku meli hiyo inagharimu million nne kwa siku kwa ajili ya mafuta.

Kwa upande wa mhandisi mkuu wa meli hiyo Ramadhan Mwinyi Ramadhan amemthibitishia Waziri kuwa jambo linalopelekea meli hiyo kuharibika mara kwa mara ni kuwa meli hiyo ilinunuliwa na kukabidhiwa ikiwa na mashine mbovu.

Aidha ameutaka uongozi wa shirika la meli kuwasili wizarani  kwa lengo la kukaa pamoja na kuweza kulijadili tatizo hilo ili meli hiyo iweze kufanya safari zake za Unguja na Pemba.

Pia  Waziri huyo amefurahishwa na kasi ya uondoshwaji wa makontena katika bandari kuu ya Zanzibar na kumtaka mkurugenzi wa bandari Bw. Nahat  Mohammed Mahfoudh kuendelea na kasi hiyo ili kuongeza mapato ya Taifa.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa bandari amesema ili kuendana na kasi ya maendeleo iliyopo ipo haja kwa mamlaka ya bandari kutumia mfumo mpya wa teknolojia wa utoaji mizigo badala ya mfumo wa zamani ili kurahisisha huduma kwa watumiaji wa bandari hiyo.

Wakati huo huo waziri wa mawasiliano na uchukuzi ametoa agizo kwa wakala wa barabara kuhakikisha wanaunda kamati itakayoshughulikia ukarabatiwa barabara zote zenye mashimo kwa kuanza na barabara ya uwanja wa ndege ambayo imekuwa ikileta taswira mbaya ya mji wa Zanzibar.

Sambamba na hilo alisisitiza wafanyakazi wa wakala wa barabara kupatiwa stahiki zao wanazostahiki  ili wafanyakazi hao wafanye kazi kwa ufanisi.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.