Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na wadau wa
mifumo ya kuuza maudhui na kazi za Sanaa kwa njia ya mtandao, lengo likiwa ni kutafuta mifumo mizuri yenye ubora
na viwango itakayosadia wasanii kuuza kazi zao. Kikao hicho kimefanyika Desemba
17, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan
Abbasi amesema kuwa Serikali katika
kukuza na kuhakikisha maslahi ya wasanii
yanaboreshwa, imeanza kupokea mawazo kuhusu namna bora ya kutumia mifumo ya kiteknolojia katika kuuza kazi za Sanaa
Dkt. Abbasi ameyasema
hayo Desemba 17, 2020 Jijini Dar es Salaam alipokuatana na kufanya kikao na wadau wa
mifumo ya kuuza kazi za Sanaa ambapo amesema kuwa Serikali inataka kuweka
mazingira bora ya kufanya kazi ya Sanaa ambayo itawanufaisha na kuwasaidia
kupata soko la uhakika huku akisistiza kuwa mifumo ambayo wadau watapendekeza lazima
iwe bora katika kuonyesha maudhui na yenye viwango bora.
“Wasanii mnapaswa
kutumia teknolojia ambayo kwa sasa ndio inabeba soko la kuuza n kazi zenu, na
lazima mtambue kuwa “teknolojia huwezi kushindana nayo ila unaweza kufaidika
nayo” hivyo ni jukumu lenu kutumia fursa hiyo”,alisema
Dkt.Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi
amewataka wabunifu na wasanii wote kusajili kazi zao katika Taasisi ya Hakimili
Tanzania (COSOTA) ili zilindwe na Sheria ambazo zinasimamiwa na Serikali lengo
likiwa ni kuwanufaisha wasanii hao.
Vilevile, Dkt. Abbasi amewaagiza wasanii hao na wadau wote wa
Sanaa kuwasilisha serikalini tozo zote ambazo zimekuwa ni kero katika
kutekeleza kazi zao ifikapo Desemba 31, 2020 ili Serikali izifanyie kazi.
Naye Bw. Lumuliko
Mengele kutoka Kampuni ya Blackball ameishukuru Serikali kuona umuhimu wa
kutumia mifumo katika kuuza kazi za Sanaa ambapo ameshauri
kuwa mifumo hiyo iwe na uwanja mpana katika kufanya kazi hiyo.
Kwa upande wake Bw.Emmanuel
Godfrey ameshauri kuwa mifumo
itakayoridhiwa lazima iwekewe vigezo ambayo watumiaji wengi watakuwa na uwezo
wa kuvifikia huku akisistiza kuwa Serikali iiratibu mifumo hiyo.
No comments:
Post a Comment