Habari za Punde

Rais Dk Hussein Ali Mwinyi akutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Nchini Tanzania

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi  akizungumza na  Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Nchini  Tanzania Nd.Shalini Bahuguna alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo pamoja na kusalimiana na Mhe.Rais leo (kushoto) Mwakilishi wa Unicef hapa zanzibar Maha Damaj,PHD.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi  akizungumza na  Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Nchini  Tanzania Nd.Shalini Bahuguna alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo pamoja na kusalimiana na Mhe.Rais leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameliahidi Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendeleza mushirikiano na Shirika hilo ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.

Rais Dk. Hussein aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alikutana na  Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) nchini Tanzania Bi Shalini Bahuguna ambapo mbali ya mazungumzo hayo Mwakilishi huyo alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake Rais Dk. Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kwa kulipongeza na kulishukuru Shirika la UNICEF kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha malengo ya Shirika hilo yanafikiwa hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha ustawi wa watoto kwa kusaidia huduma mbali mbali zikiwemo zile za kijamii.

Rais Dk. Hussein alisema kwamba Serikali ya Awamu ya Nane iko tayari kushirikiana na Shirika hilo katika maeneo ya kipaumbele yaliyowekwa katika kuhakikisha mafanikio yanafikiwa.

Aidha, Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kusaidia uimarishaji wa huduma za kijamii hapa Zanzibar hatua ambayo imekuwa ikiwasaidia watoto, vijana na hata wanawake.

Aliongeza kuwa mashirikiano yaliopo katika sekta ya afya kati ya Serikali na Shirika hilo ndio yameweza kuleta mafanikio ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto hapa Zanzibar.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alimuahidi Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini kwamba changamoto zinazowakabili watoto likiwemo suala la ajira kwa watoto, ustawi wa watoto wa kiume katika sekta ya elimu vyote hivyo vinafanyiwa kazi.

Rais Dk. Hussein alieleza kuvutiwa na mikakati pamoja na programu mbali mbali zilizowekwa na Shirika hilo hapa nchini katika kuhakikisha linaendelea kuwasaidia watoto katika nyanja mbali mbali zikiwemo huduma za elimu, afya na uwezeshaji.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) nchini Tanzania  Bi Shalini Bahuguna alianza mazungumzo yake kwa kumpongeza  Rais Dk. Hussein kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar na kuwa Rais wao huku akiahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kumuunga mkono yeye na Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Nane.

 Mwakilishi huyo alieleza kuwa Shirika la UNICEF lina hitoria ya muda mrefu katika kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika nyanja mbali mbali za maendeleo ikiwemo kuwasaidia watoto.

Aliongeza kuwa tayari shirika hilo limeshaweka mikakati pamoja na programu mbali mbali katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi na kuondosha changamoto kadhaa zinazowakabili.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua jitihada kubwa katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi na kuahidi kwamba Shirika lake litaendelea kuunga mkono jitihada hizo.

Mwakilishi huyo pia, alipongeza hatua zilizochukuliwa na uongozi katika kukabiliana na kupambana na janga la COVID 19 ambapo Tanzania ikiwemo Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kukabiliana nalo.

Kiongozi huyo alieleza kwamba lengo la Shirika hilo ni kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio makubwa katika sekta ya afya hasa kwa upande wa watoto.

Sambamba na hayo, Mwakilishi huyo alipongeza juhudi za Serikali zilizofikiwa katika kupiga hatua za kupambana  na vifo vya akina mama na watoto na kuweza kupunguza idadi kubwa ya akina mama na watoto wanaofariki wakati wa kujifungua.

Alieleza kwamba miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Shirika hilo ni kuhakikisha huduma za afya zinaongezeka ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa katika hospitali mbali mbali hapa Zanzibar sambamba na kuweka ustawi katika sekta ya elimu.

Alieleza azma ya Shirika hilo ya kuziendeleza programu ziliopo na kuziongeza zaidi kwa lengo la kupata mafanikio zaidi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi zikiwemo huduma zote za kijamii.

Nae kwa upande wake Bi Maha Damaj ambaye ni Mkuu wa Ofisi za UNICEF Zanzibar alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Shirika hilo katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa  mashirikiano ya pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuhakikisha

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.