Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania

                                                          

                                        

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaomba Wawekezaji kutoka nchi za Jumuiya ya  Kiarabu (UAE) kuja kuwekeza nchini, hususan katika sekta ya Utalii.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Khalifa Abdulrahman Almarzouqi,  aliefika kujitambulisha kwa Rais.

Alisema katika dhana ya kuimarisha uchumi, Zanzibar  inalenga  kuimarisha uchumi wake kupitia Uchumi wa Buluu, hivyo inahitaji Wawekezaji kutoka mataifa mbali mbali Duniani, ikiwemo UAE ili kuwekeza kupitia sekta ya Utalii yenye vivutio mbali mbali katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga  kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo muhimu la Uwekezaji, hivyo akawataka wawekezaji kutoka nchi hizo kuja kuwekeza katika miradi mbali mbali.

Alisema sheria za Uwekezaji, ikihusisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya miradi mbali mbali zinatoa fursa kwa Wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbali mbali yakiwemo ya visiwa.

Aidha, Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa nchi za Jumuiya hiyo kwa uhusiano na ushirikiano mzuri na wa muda mrefu kati yake na Zanzibar, pamoja na misaada mbali mbali inayoendelea kutolewa kupitia nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Alisema nchi za Jumuiya ya Kiarabu zimekuwa zikiunga mkono juhudi za serikali na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, ambapo kwa nyakati tofauti zimesaidia miradi mbali, ukiwemo Mfuko wa ‘Khalifa Fund’ unaolenga kuwawezesha  kiuchumi  Vijana  wa Zanzibar.

Vile vile aliziomba taasisi na  wadau wa maendeleo  kutoka nchi hizo kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuuweka katika mazingira bora zaidi Mji Mkongwe wa Zanzibar, (ulio katika Urithi wa Ulimwengu) ili uweze kuwa eneo la kiuchumi.

Nae, Balozi wa UAE nchini Tanzania Khalifa Abdulrahman Almarzouqi alimshakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa UAE itaendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Zanzibar, sambamba na kuendelea kuisaidia nchi hiyo katika nyanja za Kiuchumi na kijamii.

Aidha, aliahidi kuwashajiisha Wawekezaji wa nchi hizo kuja nchini kuwekeza, akibainisha kuwepo kwa kampuni mbali mbali zinazowekeza katika sekta ya utalii kupitia miradi mbali mbali, ikiwemo ya ujenzi wa Hoteli kubwa za kitalii, michezo ya baharini na miradi mengineyo.     

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.