Habari za Punde

Rais Magufuli:Mawaziri Msiogope Kufanya Maamuzi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwaapisha Mawaziri pamoja na Manaibu Waziri katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma


Na Immaculate Makilika-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka mawaziri kutoogopa kufanya maamuzi kwa  kuogopa kufanya uamuzi mabaya.

Akizungumza leo, Ikulu Chamwino  Dodoma mara baada ya kuwaapisha mawaziri 21 na manaibu waziri 22, Rais Magufuli alisema sasa mawaziri wanatakiwa kufanya maamuzi  bila kuogopa kukosea. “Ni vizuri ukafanye uamuzi mbaya kuliko kutokufanya uamuzi, unashindwa kutoa uamuzi kwasababu hutaki uonekane mbaya, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita  miradi ya maji zaidi ya  1,400  imekamilika, kwa hiyo mkafanye kazi, kafanyeni uamuzi hasa unaohusu maslahi ya taifa”, alisema Rais Magufuli

Aidha, Rais Magufuli amewataka mawaziri na viongozi wa Serikali  kuzingatia  uadilifu na kuhakikisha kuwa maagizo na maelekezo ya Serikali yanafuata utaratibu. “Ndani ya Serikali sasa hivi kuna ugonjwa mmoja wa ajabu, kwamba hata mawasiliano yanatumwa kwenye ‘group za WhatsApp, barua nyingine ni za siri na zinaishia kuvuja. Tuzingatie maadili ya viapo vyetu na tufanye kazi zetu kwa uadilifu mkubwa, Serikali hufanya kazi kwa maandishi”, alisisitiza Rais Magufuli.

Kuhusu somo la historia, Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa somo hilo linakuwa somo la lazima kufundishwa mashuleni ili wanafunzi waweze kujua historia ya nchi yao.

“Nataka wanafunzi wetu wafundishwe historia ya Tanzania na hii itasaidia kujenga uzalendo, vijana hawajui historia ya nchi yetu, inawezekana masomo haya yatasaidia kujua jinsi wageni walivyokuja wakadanganya wazee wetu”, alisisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizungumzia changamoto zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo matumizi mabya ya fedha za umma ambapo alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha yaliyofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kununua gari la gharama ya zaidi ya shilingi milioni 400.

Halikadhalika, Rais Magufuli alisema kuwa  katika kipindi cha miaka mitano iliyopita vijiji 9,880 vilipata umeme na katika kipindi cha miaka mitano ijayo vijiji 2,338, vilivyobaki pia vipate umeme, sambamba na kuanza mradi wa uzalishaji megawati 350  za umeme wa maji mkoani Njombe zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Vilevile, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa kuhakikisha kero za wasanii na wanamichezo  zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo kusaidia wasanii kupata haki zao.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwataka mawaziri  kafanya kazi kwa bidii, ili kutimiza matumaini ya  wananchi  katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Naye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kuwa mawaziri, wameapa kumsaidia mhe. Rais kazi na jukumu kubwa  ni kufanya kazi kwa kuwatumikia watanzania. “Tunahitaji kuona matokeo ya kazi maana miongozo tayari tunayo. Twende tukachape kazi”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.