Habari za Punde

Alhaj Dk Mwinyi Amewataka Wananchi wa Zanzibar Kudumisha Amani na Uwajibikaji Katika Sekta za Umma.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waumini wa Kiislam katika Masjid Afraa Bint Issa baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika leo 1-1-2021. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa baada ya kupatikana amani na umoja nchini kilichobaki hivi sasa  ni kuendelea kuhubiri uwajikaji katika sekta za umma na sekta binafsi ili kuleta maendeleo ya haraka.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akiwasilimia waumini wa dini ya Kiislamu huko katika Masjid Afraa Bint Issa (Msikiti Shurba), Kidongochekundu, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mara baada ya kujumuika nao katika Sala ya Ijumaa.

Katika salamu zake kwa waumini wa Msikiti huo pamoja na wananchi wote kwa jumla Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuwajibika kwa kila mtu kwa nafasi yake aliyonayo kwa lengo la kuleta maendeleo yaliyokusudiwa.

Akieleza mambo matatu muhimu ambayo yakifuatwa yataleta maendeleo ikiwemo amani, umoja na suala zima la uwajibikaji,Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa nafasi aliyonayo.

“Anaekushanya kodi akushanye maana asipokusanywa hatuwezi kuwa na fedha za kuleta maendeleo, anayetakiwa kuzoa taka azoe vyenginevyo miji itakuwa michafu, anetibu hospitali atoe huduma nzuri kwa wagonjwa na aliyekuwa maskulini atoe elimu bora, sote tukiwajibika maendeleo makubwa tutayapata”, alisisitiza Alhaj Dk. Mwinyi.

Katika maelezo yake Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa akiwa kiongozi tayari ameanza kuchukua hatua dhidi ya mambo ambayo yanarudisha nyuma hatua za kuleta maendeleo nchini.

Alisema kuwa wapo watu ambao hawatoridhika na hatua hizo anazozichukua ambazo ni muhimu katika kuleta nidhamu ya utumishi wa umma na nidhamu ya uwajibikaji na nidhamu ya kuhakikisha kwamba fedha za Serikali nivyema zikatumika kwa watu wote na sio kwa mtu binafsi.

Hivyo, aliwataka waumini kuendelea kumomba dua  kwani wapo ambao hawatoridhika na wapo watakaoridhika na hatua hizo hivyo dua zao ni muhimu kutokana na lengo lililopo la kuwatumikia wananchi  kwa kadri matarajio yao yalivyo.

Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa viongozi wa dini kwa kuendelea kuwaunga mkono mara zote wanapochukua hatua zenye lengo la kujenga.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwasisitiza wafanyakazi wote kwa nafasi walizonazo wawajibike ipasavyo ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana.

Rais Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa wananchi na waumini wote kwa kuiitikia wito wa kudumisha amani ambalo ni miongoni mwa mambo matatu aliyoyataja na kutoa shukurani kwa wananchi kwa kuidumisha katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu watu waliombwa kuwachagua viongozi wanaowataka ambapo kila aliyechagua alikuwa na matumaini na kiongozi anayemtaka kwa lengo la kuleta maendeleo.

Aidha, katika mambo hayo matatu aliyoyaeleza Alhaj Dk. Mwinyi ni umoja ambapo alisisitiza kwamba kwamba hatua ya kudumisha umoja imesaidia kwa kiasi kikubwa wkani hapo siku za nyuma haukuwepo hatua iliyopelekea mfarakano kutokana na imani za kisiasa jambo ambalo lisingeweza kuleta maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote kwa kudumisha umoja na kueleza kwamba kwa upande wao viongozi wa kisiasa wameshaanza kuchukua hatua kwa kuanza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kuwaunganisha watu na kuleta umoja nchini kwa azma ya kuleta maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote kuendeleza tunu ya amani na umoja ili kuweza kupata maendeleo.

Aliongeza kuwa waumini walimuomba Mwenyezi Mungu kuleta amani na umoja ambapo hivi sasa vyote hivyo vimepatikana na kusisitiza kwamba kazi iliyobaki ni kuleta maendeleo na wale waliokuwa bado hawajakubaliana na hali ya umoja  waendelee kuwaelisha.

Mapema akisoma hotuba ya Ijumaa, Sheikh Omar Bin Abeid alisisitiza haja kwa waumini wa dini ya Kiislamu kusimamia maadili ya uongozi huku akitumia fursa hiyo kueleza hatua anazozichukua Alhaj Dk. Mwinyi katika suala zima la uwajibikaji kuwa ni sehemu ya kutekeleza majukumu yenye tija katika umma.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.