Habari za Punde

Homa ya mapafu (Pneumonia) kwa watoto



 

Homa ya mapafu (Pneumonia) kwa watoto

 

MWILI wa binadamu una mapafu mawili yenye maumbile yanayofana na kazi kuu ya mapafu ni sehemu ya mwili inayoingiza oksijeni mwilini na kuipeleka kwenye seli za mwili. Ni kiungo kikuu kwenye mfumo wa upumuaji.

 

Inapotokea mtu au mtoto kapata homa ya mapafu, vifuko hivi hujaa maji au usaha, hivyo huathiri upitishaji wa hewa safi kwenye damu na kusababisha tatizo la kupumua.

 

Homa ya mapafu au ‘pneumonia’ ni ugonjwa unaoshambulia mfumo mzima wa hewa, ni aina ya maambukizi yanayoathiri mapafu. Aidha ni ugonjwa unaoua watoto wengi hasa katika nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Zazibar. Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio chini ya miaka mitano wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.

 

Vihatarishi vya homa ya mapafu

 

v  Watoto wenye ukosefu wa kinga mwilini

v  Ukosefu wa lishe bora hasa kwa watoto wachanga ambao hawanyonyeshwi ipasavyo.

v  Aidha uwepo wa magonjwa mengine, kwa mfano, maambukizi ya virusi vya UKIMWI, saratani na ugonjwa wa surua hupelekea kinga ya mwili kuwa dhaifu.

v  Mazingira duni yenye moshi wa sigara au moshi ndani ya nyumba unaosababishwa na kupikia kuni au mkaa.

v  Msongamano ndani ya nyumba kutokana na watu kuwa wengi sehemu moja nayo huweza kusababisha watoto kupata homa ya mapafu.

 

Sababu za ugonjwa wa homa ya mapafu

 

Homa ya mapafu inasababishwa na vimelea vya maradhi kama vile bacteria, virusi, parasiti na fangasi.

 

Kwa kawaida vimelea hushambulia mwili wa binadamu kulingana na umri na kinga ya mwili. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa watoto wakubwa.

 

Baadhi ya vimelea wa bakteria wanaoshambulia watoto ni pamoja na ‘streptococcus pneumoniae’ ambao ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto katika visiwa vyetu.

 

Wapo pia ‘haemophilus influenzae’ aina b (HIB) ambao ni aina ya pili ya bacteria walio maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa mapafu kwa watoto.

‘Staphylococcus aureus’ ni aina nyingine ya bacteria ambao hushambulia zaidi watoto wachanga. Kuna pia group B streptococci, ambao pia hushambulia zaidi watoto wachanga.

 

Kwa upande wa virusi, virusi wa aina ya ‘respiratory syncytial virus’, ndiyo wanaoongoza kwa kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.

 

Aidha, vimelea wa ‘pneumocystis jiroveci’ ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasiti ni maarufu zaidi miongoni mwa parasiti wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini hususani watoto wenye VVU.

 

Aina nyingine za bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na ‘mycoplasma pneumonia’ na ‘chlamydia pneumonia’.

 

Jinsi homa ya mapafu inavyoenezwa

 

Mara nyingi inapotokea kinga ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yeyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji (lower respiratory tract) na hatimaye kushambulia mapafu.

 

Halkadhalika, vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya kuzaliwa, yaani kipindi cha mimba.

 

Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu

 

Kwa watoto wadogo, dalili za awali zinaweza kuwa homa kali pamoja na mtoto kuhangaika, kunyong’onyea kung’ang’anaa. Watoto wanaozaliwa wakiwa na uambukizi wa bakteria aina ya ‘streptococcus’ kundi ‘B’ wanaweza kuwa na homa na kupumua kwa shida.

 

Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na dalili ambazo si maalum kama vile kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yeyote ya kushindwa kupumua. Hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.

 

Dalili za kawaida za homa ya mapafu ambazo huwapata karibu watoto wote wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja na; homa kali, kuhisi baridi, kikohozi, kupumua kwa haraka kuliko kawaida, kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa kupumua, mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa kupumua na maumivu ya tumbo.

 

Dalili nyengine kupoteza hamu ya kucheza, kupoteza hamu ya kula na kushindwa kunyonya, mtoto kubadilika rangi na kuwa na rangi buluu katika midomo na kucha (CYANOSIS).

Hata hivyo, si lazima dalili zote hizi ziwepo kwa kila mtoto. Baadhi ya watoto huonesha kupumua kwa haraka kama dalili pekee ya homa ya mapafu.

 

Iwapo vimelea vimeshambulia sehemu za chini ya mapafu karibu ya tumbo, sehemu ijulikanayo kama kiwambo au ‘diaphragm’, mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya kushindwa kupumua ingawa anaweza kuwa na homa na kujihisi maumivu makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika.

 

Kwa watoto wachanga zaidi wanaweza kushindwa kunyonya na pia kupoteza fahamu na kupata degedege.

 

Uchunguzi na vipimo

 

Daktari humchunguza mtoto kwa kusikiliza dalili za ugonjwa kutoka kwa  kutumia kipimo kinachoitwa ‘stethoscope’.

 

Vipimo hivyo ni pamoja na X-ray ya kifua, au CT-scan ya kifua, pamoja na damu ili kuchunguza madhara yaliyoletwa na homa hii ya mapafu.

 

X-ray ya kifua na CT-scan ya kifua vina uwezo wa kuonesha tatizo hata pale ambapo daktari ameshindwa kusikia sauti maalum kwa kutumia kifaa chake cha ‘stethoscope’.

 

Matibabu

 

Matibabu homa ya mapafu hutegemea ni aina gani ya vimelea ya maradhi, umri na hali ya yule mtoto ilivyo.

 

Mara nyingi dawa za maji za ‘antibiotics’ kama vile ‘erythromycin’, ‘benzylpenicillin’, ‘cefotaxime’, ‘amoxycillin’, ‘clarithromycin’ nakadhalika  hutumika kutibu homa na maambukizi huku dawa za panadoli na ‘ibumex’ hutumika kushusha homa ya mwili.

 

Ikumbukwe kwamba dawa za ‘antibiotics’ hazina uwezo wowote wa kutibu homa inayosababishwa na virusi (viruses), kwa hiyo hupona kwa kutumia tu dawa za kushusha homa, lishe, mazingira yenye hewa safi na kumpa mtoto maji mengi.

 

Na hii ieleweke kwambaa ni daktari pekee ndiye anayeweza kufahamu kama mtoto wako anahitaji ‘antibiotics’ au dawa za aina nyingine. Kwa hiyo ni muhimu kwa mzazi ama mlezi kumpeleka mtoto kituo cha afya au hospitalini haraka pindi anapoonesha dalili za ugonjwa badala ya kuamua kumpa dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

 

Kinga homa ya mapafu

 

Homa ya mapafu inaweza kuzuiliwa kwa chanjo, chanjo dhidi ya Hib, pneumococcus, surua na kifaduro ni njia mojawapo ya kuzuia homa ya mapafu.

 

Mtoto kuishi katika mazingira yenye hewa safi.

 

Lishe ya kutosha ni muhimu kwa kuboresha kinga ya mwili ya mtoto ambapo inashauriwa mama kunyonyesha mtoto bila kuchanganya na kitu chochote walau kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha yake.

 

Kuhimiza usafi katika makaazi kama kutotumia jiko la mkaa au kuni ndani ya nyumba na uvutaji wa sigara ni jambo linaloshauriwa pia.

 

Kwa watoto wenye virusi vya UKIMWI, matumizi ya dawa ya ‘cotrimoxazole’ kila siku husaidia kupunguza uwezekano wa kupata homa ya mapafu.

 

Indhari

 

Tafiti nyingi duniani zimeonyesha kwamba kinga na tiba sahihi ya homa ya mapafu inaweza kuzuia vifo milioni moja kwa watoto duniani kila mwaka. Hivyo ni wajibu wetu sote kushirikiana kupambana na ugonjwa huu.

 

 

Imetayarishwa na:

Mohammed Sharksy

Mkufunzi Msaidizi,

Skuli ya Afya Sayansi za Tiba,

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, SUZA

 

0777432493  email: ruruma96@gmail.com

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.