Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Kesho Kushuhudia Utiaji wa Saini ya MOU Mpango ya Ujenzi wa Bandari Mangapwani.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kesho anatarajiwa kushudia utiaji saini wa Hati ya Maelewano (MOU), inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani unaojumuisha Bandari tofauti ikiwemo bandari ya mizigo, uvuvi, mafuta na gesi asilia, chelezo pamoja na Mji wa kisasa.

Utiaji saini huo unatarajiwa kufanyika Ikulu Jijini Zanzibar kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakae saini Hati hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakari ambapo kwa upande wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman anaetarajiwa kusaini ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Sheikh Mohammed Al-Tooq ambaye ataongoza ujumbe wa watu watatu.

Utiaji saini Hati ya Maelewano inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi katika Bandari ya hiyo ya Mangapwani ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kutekeleza Sera yake ya Uchumi wa Buluu.

Aidha, hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi kuelekea siku mia tokea alipoapishwa kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.