Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Azungumza Katika Hafla ya Utiaji wa Saini ya Maaelewano ya Ujenzi Bandari ya Uvuvu na Mradi wa Ufuaji Umeme wa Gesi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya utiaji wa Saini ya Maelewano (MOU) Mpango Mkuu wa Upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa Bandari Shirikishi ya Uvuvi katika eneo la Mpiga Duri na Mkoani Pemba na Mradi wa Ufuaji wa Umeme wa Nishati ya Gesi Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetia saini Hati za Maelewano (MOU) zinazohusu Mpango Mkuu wa Upembuzi yakinifu juu ya  ujenzi wa Bandari Shirikishi ya Uvuvi katika eneo la Mpiga Duri Unguja na Bandari ya Mkoani Pemba pamoja na Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa Nishati ya Gesi.

Hafla ya utiaji saini hati za Maelewano (MOU), imefanyika leo Ikulu Jijini Zanzibar ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alishuhudia utiaji saini huo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya INTERTORCO yenye makao makuu yake mjini Madrid Hispania.

Utiaji saini Hati ya Maelewano kuhusu kazi ya Upembuzi yakinifu wa Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa Nishati ya Gesi kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulisainiwa na Katibu Wizara ya  Maji na Nishati Dk. Mngereza Mzee Miraji ambapo kwa upande wa Kampuni ya TANGEN & INTERTORCO GROUP ilisainiwa na Allan Kessler Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ambaye pia ni mkuu wa Kampuni ya “Monitor Power System”  .

Aidha, kwa upande wa Hati ya Maelewano juu ya ujenzi wa Bandari ya uvuvi aliyesaini kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Katibu Mkuu, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dk. Aboud Suleiman Jumbe ambapo kutoa Kampuni ya TANGEN & INTERTORCO GROUP , aliyesaini ni Injinia Michael Angaga ambaye ni mwakilishi wa Kampuni hiyo.

Mara baada ya utiaji saini hati hizo za Maelewano, Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwahutubia wananchi waliofika katika hafla hiyo pamoja na wale waliokuwa wakifuatilia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambapo alisema kwamba Zanzibar imeanza safari mpya ya uchumi wa buluu.

Alisema kuwa  amefurahishwa na utiaji saini mradi huo mkubwa ambao unajumuisha bandari za uvuvi Unguja na Pemba ambao utahusisha ujenzi wa maegesho ya meli za uvuvi zenye gati tano kwa upande wa Mpigaduri Unguja na gati mbili  katika bandari ya Mkoani Pemba.

Aidha, alisema kuwa  kutakuwa na ununuzi wa  meli za uvuvi kwa ajili ya uvuvi bahari kuu, ujenzi wa chelezo cha kujenga na kutengeneza meli, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza boti ndogo kwa wavuvi, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nyavu na zana za uvuvi.

Ujenzi mwengine ni kiwanda cha kusindika minofu ya sakami, kiwanda cha kutengeneza mbolea itakayotokana na mabaki ya samaki, ujenzi wa soko la mnada wa samaki la Kimataifa, ujenzi wa majokofu mbali mbali ya kuhifadhia samaki, pamoja na Chuo Kikuu cha kufundishia uvuvi na ubaharia.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mradi huo ukitekelezwa uchumi wa Zanzibar utakuwa kwa haraka sana ambapo Serikali itatekeleza Mradi huo kwa mashrikiano na Kampuni  12, kutoka nchi tano za Norway, Hispania, Ujerumani, Korea Kusini na Marekani.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru Wabia hao ambao wameona haja ya kuiunga mkono Serikali kwa kuleta miradi mbali mbali hapa Zanzibar.

Aliwasisitiza wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar kwani miradi bado iko mingi na Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa utaratibu wa aina tatu.

Alisema kuwa mradi wa aina ya kwanza ni ile miradi ya miundombinu ya kibiashara kama ule uliotiwa saini wiki iliyopita ya mradi wa Bandari ya Mangapwani/Bumbwini pamoja na Bandari ya Mpigaduri ambayo itahusisha uvuvi.

Aliongeza kuwa aina ya miradi inayotaka kuanzishwa itahitaji umeme mwingi na hivi sasa kwa upande wa Unguja ina umeme wa megawati 100 tu na Pemba megawati 20 tu ambapo ni vyema safari ya kuzalisha umeme mwingi ikaanza kwani umeme huo bado ni mdogo ambayo haiendani na maendeleo yaliokusudiwa.

Hivyo,  alisema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kuingia makubaliano ya kuzalisha umeme, huku akieleza kwamba miradi hiyo ya biashara itakuwa ni ya ubia kati ya wawekezaji na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Alisema kuwa  miradi mengine ni ile ya huduma kama vile barabara, elimu, afya na maji, hiyo itatekelezwa na Serikali ambapo itatafuta fedha kwa njia mbali mbali ikiwemo bajeti yake pamoja na mikopo ya masharti nafuu na ufadhili wa nchi rafiki.

Aina ya tatu alisema ni ile miradi itakayotekelezwa na sekta binafsi peke yake ambapo bado Zanzibar ina hitaji wawekezaji katika viwanda, hoteli pamoja na mambo mengi katika utalii na mambo mengineyo.

Rais Dk. Mwinyi alifurahishwa na mradi huo kutoka kampuni hiyo ya INTERTORCO GROUP ambao wanakusudia kuwekeza Zanzibar Dola za Kimarekani Bilioni 6.3 ambazo ni fedha nyingi huku Rais Dk. Mwinyi akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kuja kuekeza Zanzibar.

Aliyataja maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji likiwemo eneo la Hoteli ya Bwawani, Mji Mgongwe wa Zanzibar, viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba kwani mradi kama huo wa Mpigaduri utahitaji usafiri wa kutosha hivyo ni vyema mipango ikapangwa juu ya uwekezaji katika viwanja vya ndege.

Aliongeza kuwa tayari ameshapokea maombi kadhaa kutoka kwa wawekezaji ambao wanataka kuja kuekeza katika viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba na kusisitiza kwamba kasi hiyo ikiendelea Zanzibar itapata miradi mikubwa sana ya kimaendeleo

Alisema kuwa wananchi ni vyema wakatambua kwamba miradi hiyo  inawahusu kwani wageni wanaokuja kujenga miradi hiyo watahitaji makaazi, hivyo ni vyema wakajenga nyumba kwa ajili ya kukodisha, hoteli, vyakula na mambo mengine mengi.

Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kubadilisha hali ya maisha ya Wazanzibari kwa kiwango kikubwa na kuishukuru Kampuni hiyo kwa kuonesha njia ya Sera ya Serikali ya uchumi wa buluu.

Sambamba na hayo, alisema kuwa mradi huo utasaidia hata wavuvi wadogo kwani tayari watakuwa na soko la uhakika ambapo pia, miradi hiyo italeta neema kwa wananchi wote hasa vijana ambao watachangamkia fursa nyingi za ajira zitakazotokana na miradi hiyo.

Pamoja na hayo, alieleza kwamba yale yaliyokuwa yakisemwa sasa mwanga unaanza kuonekana na kueleza kwamba hatua kama hizo za utiaji saini hati za maelewano zitaendelea hatua ambayo tabadilisha uchumi wa Zanzibar.

Allan Kessler Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni TANGEN & INTERTORCO GROUP ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya “Monitor Power System”  alisema kuwa Zanzibar ambayo imo ndani ya Jamhuri ya Muuungano inaendelea kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbali mbali dunini.

Alieleza kuwa kuwepo kwa utulivu wa kisiasa, historia tajiri ya biashara ya Zanzibar inafanya kuwa ni eneo bora la usafirishaji wa biashara hasa ikizingatiwa kwamba umeme ni ufunguo wa ukuaji wa viwanda na kueleza azma ya Kampuni hiyo kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Mwinyi za kuimarisha uchumi wa buluu.

Kessler alieleza hatua na njia itakayotumika kupatikana kwa umeme huo wa gesi ambao utasaidia katika kuendeshea mradi huo pamoja na miradi mengine ambapo tayari miradi kama hiyo wameshaifanya katika nchi za Sudan, Somalia, Msumbiji, Iswatini na nchi nyenginezo.

Alisema kuwa mradi huo utakuwa na kituo chake  kikubwa huko Fumba ambapo bomba la gesi kutoka Tanzania Bara litaingiza kupitia baharini.

Nae  Mwakilishi wa  Kampuni hiyo ya TANGEN & INTERTORCO GROUP , Injinia Michael Angaga alisema kuwa  ujenzi huo utaanza mara moja na wawekezaji wako tayari na kueleza kushirikiana na serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara.

Alisema kuwa ujenzi huo utatekelezwa pia, katika bandari ya Mkoani ambao umejumuisha miradi mengine  kumi ambayo itaifanya Zanzibar kuwa sehemu maalum ya bandari ya uvuvi katika ukanda wa Afrika.

Alisema kuwa hatua hiyo itapelekea wawekezaji na wafanyabiashara wengi kuvutiwa na kuja kufanya biashara Zanzibar badala ya kwenda nchini Dubai.

Utiaji saini miradi hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi za Rais Dk. Mwinyi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar hasa uchumi wa Buluu sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina fursa maalum ya kuendeleza uchumi wake kupitia rasilimali za bahari.

Wiki iliyopita Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alishuhudia utiaji saini Hati ya Maelewano (MOU) kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman inayohusu Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari huko Mangapwani/Bumbwini.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.