Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi Ajumuika na Wananchi Katika Maziko ya Marehemu Dkt.Mohammed Seif Khatib.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Waumini wa Kiislam katika Sala ya kuusalia mwili wa Marehemu Mohammed Seif Khatib iliofanyika katika Masjid Noor Muhammad S.A.W ,ilioongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na (kulia kwa Rais) Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Hassan Othman Ngwali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaaf wa Zanzibar Awamu ya Saba Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Abdalla Talib na Balozi Seif Ali Iddi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaaf swakishiriki katika Sala hiyo iliofanyika leo 16-2-2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyileo amewaongoza wananchi katika mazishi ya Marehemu Dk. Mohamed Seif Khatib yaliyofanyika huko kijijini kwao Umbuji, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa,dini na Serikali pamoja na wananchi walihudhuria katika mazishi hayo ambapo mapema Alhaj Dk. Mwinyi aliungana nao katika sala ya kumuombea Marehemu iliyosaliwa huko katika Masjidi Noor Muhammad (S.A.W), Mombasa kwa Mchina, Jijini Zanzibar.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika mazishi hayo ni Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, Rais wa Zanzibar Mstaafu wa Awamu ya Saba, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mstaafu Balozi Seif Ali Idd pamoja na  Viongozi wengine wa Serikali, viongozi wa CCM na vyama vyengine vya siasa.

Akisoma Wasifu wa Marehemu Dk. Mohamed Seif Khatib huko Umbuji, Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Khamis Abdalla Said alisema kuwa  Marehemu amezaliwa tarehe 10 Januari 1951 huko kijijini kwao Umbuji, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema kuwa marehemu Mohamed Seif Khatib ambaye kifo chake kilichotokea jana (Februari 15,2021) huko katika Hospitali ya Al-rahma  jijini Zanzibar baada ya kuugua kwa muda mfupi, Marehemu ameoa na kubahatika kuwa na watoto sita.

Alisema kuwa katika elimu, Marehemu alijiendeleza sana kielimu na  kutunukiwa Shahada mbali mbali ikiwemo Shahada ya Ualimu ya Chuo cha Ualimu Nkrumah Zanzibar, Shahada ya  Kwanza ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar-es Salaam, Shahada ya Uzamili katika Sanaa, London University SOAS na Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Katika uongozi wa Vijana, Naibu katibu Mkuu huyo alisema kuwa, Marehemu alianza uzoefu wa kazi kama Mwalimu wa Skuli mbali mbali akiwemo Mwalimu wa Skuli za Msingi, Mwalimu wa Skuli za Sekondari, Mkufunzi Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar pamoja na Mhadhiri wa muda, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Kwa upande wa uongozi katika Wizara mbali mbali kuanzia mwaka 1988 hadi 2010, Marehemu aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ofisi ya Makamu wa Rais anaeshughulikia Mambo ya Muungano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na Waziri wa Mambo ya Ndani, Ofisi ya Waziri Mkuu (Habari na Siasa).

Naibu Katibu Mkuu huyo akisoma Wasfu huo alieleza kwamba kwa upande wa uzoefu katika Siasa, Marehemu aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Uzini kuanzia mwaka 1988 hadi 2015, Mjumbe wa NEC, CCM kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 2017, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa CCM (Idara ya Siasa na Uenezi kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 20170.

Sambamba na hayo, kwa maelezo ya Naibu katibu Mkuu huyo, marehemu ameandika vitabu mbali mbali kama vile, Fungate ya Uhuru, Wasaka Tonge, Utenzi wa Ukombozi, Chanjo, Vifaru Weusi na Kipanga ambapo pia, ana miswada ambayo haijachapishwa.

Pia, alisema kuwa Marehemu amesimamia wanafunzi wa Uzamili na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na kutunga  nyimbo mbali mbali  za taarabu na  kuandika makala nyingi za Kiswahili.

Pamoja na hayo, Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba  Marehemu vile vile alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar kuanzia mwaka 2014 hadi kufariki kwake lakini pia, alikuwa Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi Serikali.

Katika wasfu huo pia, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Marehemu alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo waliochukua Uzamivu (PhD ya Kiswahili) hapa nchini.

Halikadhalika,Wasfu huo ulieleza kwamba Marehemu Dk. Mohamed Seif Khatib ameacha athari kubwa kwenye lugha ya Kiswahili.Inalilahi waina ilaihi Rajiun, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amin.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.