Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza na Maafisa Utalii waliohudhuria Mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma
Na Happiness Shayo - Dodoma
Serikali iko katika mikakati ya kuhakikisha
idadi ya watalii inaongezeka kutoka milioni 1.5 kabla ya Covid 19 hadi kufikia watalii
milioni 5 ifikapo mwaka 2025 na pia kuongeza mapato yatokanayo na utalii kutoka
dola milioni 2.6 hadi kufikia dola milioni 6 mwaka 2015.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya
Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi alipokuwa akifunga mafunzo ya Usajili wa
Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT)
yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma leo.
Dkt. Kijazi ameiagiza Idaraya Utalii
kuwa kinara katika kuongoza shughuli za Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
kuhakikisha lengo la Serikali la kuongeza idadi ya watalii na kuongeza mapato
yatokanayo na utalii linafikiwa.
“ Mafunzo haya ni moja ya mkakati wa Wizara hii
ya kuhakikisha tunafikia lengo la Serikali la kuongeza idadi ya watalii na
kuongeza mapato yatokanayo na utalii nchini” Dkt. Kijazi amefafanua.
Aidha, Dkt. Kijazi ameongeza kuwa moja ya
changamoto iliyopo ni kutokuwapo kwa takwimu sahihi za idadi ya maeneo yanayotoa
huduma za malazi nchini hivyo kupelekea makusanyo ya mapato yatokanayo ya
wageni kuwa kidogo kuliko hali halisi.
“Nimepewa taarifa kwamba kumbukumbu za maeneo
yenye huduma za malazi zinafikia 1800, lakini kiuhalisia huduma za malazi
zinatolewa katika maeneo mengi nchini” Dkt. Kijazi amesisitiza.
Ameongeza kuwa idadi ndogo ya huduma za malazi zilizopo
zinazotumiwa naMamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya mapatoni ishara ya
Serikali kupoteza mapato katika maeneo mengi ambayo bado hayajaorodheshwa.
Amefafanua kuwa mafunzo ya Usajili wa Huduma za
Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT)
ni muhimu kwa sababu yatasaidia katika zoezi la utambuzi na uhakiki wa huduma
za malazi kufanyika kwa ufanisi mkubwa ili Serikali iweze kupata matokeo
yanayotarajia na pia yatasaidia kuwapo kwa kumbukumbu sahihi za watalii wanaopokelewa
katika maeneo mbalimbali nchini.
Dtk. Kijazi amewataka Maafisa watakaoshiriki
katika zoezi la utambuzi na uhakiki wa huduma za malazi kuwa na nidhamu,
uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili kufanikisha zoezi hilo.
“Hatutegemei mtumie rasilimali za Wizara halafu
mje na takwimu ambazo si sahihi. Tusije tukaona kwamba hii ndio fursa ya kwenda
kutembea yaani unaenda maeneo mawili halafu unaishia mtaani” Dkt.Kijazi amesema.
Pia ametoa onyo la kuwachukulia hatua za
kinidhamu Maafisa watakaobainika kufanya
kazi kwa mazoea.
“ Tukigundua kwamba haufanyi kazi yako kwa
umakini tutakuchukulia hatua kwa sababu hii ni fursa pekee ya kutuwezesha sisi
kupata takwimu sahihi kuhusu maeneo yenye huduma za malazi” Dkt. Kijazi
amesema.
Naye,Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii,
Philip Chitaungakwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameahidi kutekeleza
maagizo yote ya Katibu Mkuu, Dkt. Kijazi na kwamba kila mshiriki wa zoezi
utambuzi na uhakiki wa huduma za malazi atapimwa kwa matokeo kwa sababu ni kazi
muhimu sana kwa Wizara nakwa nchi.
Mmoja wa washiriki wa Mafunzo hayo ambaye ni
Afisa Utalii Mwandamizi, Franklin Mwenyembegu, amesema kuwa mafunzo hayo yamegawanyika
katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza iligusia mfumo wa Kieletroniki wa
Tathmini ya Upangaji wa Huduma za Malazi na Chakulakatika ubora wa Madaraja (Accommodation
Services in Tanzania – AserT)utakaotumika na wamiliki wa huduma za
malazi kufanya tathmini binafsi (Self-Assessment) ya huduma
wanazozitoa kwa mujibu wa vigezo na hivyo kupanga madaraja ya ubora wa nyota
wao wenyewe kabla ya kuthibitishwa na wathamini wa Serikali.
Amesema sehemu ya pili ya mafunzo hayo
ilihusisha namna bora ya uchukuaji wa taarifa za huduma za malazi nchi nzima zitakazosaidia
katika ukusanyaji wa tozo ya maendeleo ya utalii.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Maafisa Utalii
kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Maafisa Utalii kutoka Ofisi za Utalii
za Kanda ya Dar es Salaam, Arusha, Iringa na Mwanza
No comments:
Post a Comment