RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi
ameuhakikishia uongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikia nao kwani inatambua
mchango wao katika kusaidia huduma za jamii hapa nchini.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu
Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Kanisa la Waadventista
Wasabato Tanzania ambao umefika kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na
kumpongeza Rais kwa kuchaguliwa katika Awamu hii ya Nane ukiongozwa na Askofu
Mark Walwa Malekana.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema
kwamba Serikali ya Mapindzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake kwa Kanisa
hilo kutyokana na kuthamini mchango wake mkubwa katika kutoa huduma za jamii
hapa nchini.
Alisema kuwa kanisa hilo limeweza
kuwajenga kiimani waumini wake katika kushirikiana na Serikali katika
kuimarisha sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya kwa Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa juhudi za Kanisa hilo za
kusaidia katika sekta ya afya na sekta ya elimu zitaendelea kuungwa mkono na
Serikali anayoiongoza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inazifanyia kazi
changamoto zilizopo.
Alifahamisha kwamba Serikali itakuwa
tayari katika kuhakikisha miradi inayoanzishwa na Kanisa hilo ikiwemo ile ya
elimu na afya inafikia malengo yaliyokusudiwa katika kutoa huduma kwa jamii.
Aidha, alitoa pongeza kwa Kanisa hilo kwa
kusaidia katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya elimu kwa
kusaidia uimarishaji wa sekta hiyo katika Skuli ya Ali Khamis Camp iliyopo
Pemba kwa kusaidia walimu wa Sayansi pamoja na vitabu.
Pia, alilipongeza Kanisa hilo kwa
kusaidia uimarishaji wa sekta ya afya katika Zahanati yake iliyopo Meya katika
eneo la Magomeni Jijini Zanzibar ambayo imekuwa ikitoa huduma za afya kwa
kipindi kirefu.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi
aliupongeza utayari wa Kanisa hilo wa kutaka kuanzisha Chuo cha Ufundi hatua
ambayo itasaidia kuimarisha sekta ya elimu na ufundi hasa
kwa vijana.
Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba kwa
vile Zanzibar inahitaji kujenga uchumi madhubuti hivyo imani na utendaji
sambamba na mashirikiano ya pamoja yanahitajika ili kuweza kuijenga Zanzibar
yenye maendeleo zaidi.
Nae Askofu Mark Malwa Malekana ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini
mwa Tanzaniaakiwa na ujumbe wake wa Maaskofu kutoka Zanzibar na Tanzania Bara,alimpongeza
Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa ushindi mkubwa na wananchi wa Zanzibar.
Aidha, Askofu Malekana alimpongeza Rais
Dk. Mwinyi kwa kasi kubwa ya kuiletea maendeleo Zanzibar aliyoanza nayo ikiwa
ni pamoja na maono yake ya uchumi wa buluu huku akiahidi kwamba Kanisa lake
litaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufikia
malengo yake iliyojiwekea.
Askofu Malekana alimueleza Rais Dk.
Mwinyi kwamba Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa likipata mashirikiano
mazuri kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusisitiza haja ya
kuimarishwa zaidi.
Akitoa historia ya Kanisa hilo Askofu
Malekana alisema kuwa kwa hapa Zanzibar Kanisa hilo lilianza rasmi mnamo mwaka
1986 ambapo kuanzishwa kwake kuliambatana na utoaji wa huduma za kiroho na za
kijamii.
Alisema kuwa katika huduma za kijamii,
Kanisa hilo lilianzisha huduma za utabibu kwa kuwa na vituo viwili vya afya
Unguja na Pemba pamoja na kuanzisha skuli ya awali na Msingi huko Tomondo na kwa
sasa limo katika hatua ya kuanzisha skuli ya Sekondari.
Alisema kuwa elimu inayotolewa na skuli
zao inazingatia mitaala na miongozo yote inayotolewa na Wizara ya Elimu pamoja
na kutoa elimu bila ya kujali tofauti za kidini au kikabila.
Kwa upande wa Pemba alisema kwamba Kanisa
hilo lilitoa vitabu katika skuli ya Ali Khamis Camp vyenye thamani ya TZS
milioni nne pamoja na kutuma walimu wawili wa masomo ya Sayansi ambao walikuwa
wakihudumiwa na Kanisa kwa miaka mitano mfululizo hatua iliyopelekea kuongeza
ufaulu katika skuli hiyo.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo aliitaja
Zahanati iliyopo Meya eneo la Magomeni ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa jamii
pamoja na kituo cha afya kilichopo Wawi-Pemba ambacho kinaendelea kutoa huduma
nzuri.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment