Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana Mabalozi wa Nchi ya Marekani, Ufaransa na Switzerland Nchini Tanzania.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania.Mhe. Donald John Wright  alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza utayari wa Mabalozi kutoka nchi za Marekani, Ufaransa na Switzerland wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hayo leo kwa nyakati tofauti wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald John Wright, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier pamoja na Balozi wa Switzaland nchini Tanzania Didier Chassot, Ikulu Jijini Zanzibar.

Mabalozi hao wote walitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi wake mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020 na kumuweza kuiongoza Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imeanza kupata mafanikio makubwa.

Mabalozi hao wameleza matarajio yao makubwa ya Zanzibar kuimarika kiuchumi, kisiasa na kijamii chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.

Katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Marekani Donald John Wright Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Balozi huyo kwa azma yake ya kuiunga mkono Zanzibar hasa katika kuimarisha sekta ya afya.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa miongoni mwa vipaumbelea ilivyoweka Serikali anayoiongoza ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya hivyo hatua hizo za Marekani za Marekani ni chachu katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wa sekta ya uwekezaji, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba azma ya Marekani kuleta wawekezaji pamoja na Kampuni za uwekezaji katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii kutazidi kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba hatua na utayari wa Marekani wa kuendeleza mashirikiano katika sekta ya biashara na viwanda kutasaidia hasa kuweza kukuza soko la ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald John Wright alieleza malengo ya nchi yake ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya afya, uwekezaji, biashara na nyenginezo.

Aidha, Balozi Wright akiwa na ujumbe wake alimuelezaRais Dk. Mwinyi kwamba Marekani inathamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza na kueleza kwamba nchi yake iko tayari kuziunga mkono kwani zinaonesha mwanga wa maendeleo kwa Zanzibar na wananchi wake.

Rais Dk. Mwinyi pia, alifanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavierambapo Balozi huyo ameahidi kuiunga mkono Zanzibar katika mikakati yake ya kuimarisha uchumi wa buluu.

Aidha, Balozi Clavier alieleza hatua atakazozichukua katika kuhakikisha wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wa Ufaransa wanakuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali zilizopo ikiwemo sekta ya utalii.

Balozi Clavier pia, alitumia fursa hiyo kumueleza rais Dk. Mwinyi azma ya nchi yake kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya nishati, kilimo, usafiri na usafirishaji, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mafumzo mbali mbali ya ujasiriamali.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Clavier akiwa na ujumbe wake walimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba Ufaransa ina mpango wa kuikutanisha Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Zanzibar pamoja na ile ya Ufaransa ambazo zitakutakana katika mkutano maalum uliotayarishwa na Ubalozi huo.

Pia, ubalozi huo umeeleza azma ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sanaa, lugha pamoja na mashirikiano kwa vyuo vikuu kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya Vyuo Vikuu vya Zanzibar na Ufaransa.

Nae Rais Dk. Mwinyi kwa upande wake aliipongeza Ufaransa kwa azma yake hiyo na kueleza kwamba sekta zote ambazo imeahidi kuiunga mkono Zanzibar tayari Zanzibar imeshazipa kipaumbele hivyo juhudi hizo zitasaidia kwakiasi kikubwa katika kufikia lengo lililokusudiwa.

Aidha, alimueleza Balozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha uchumi wake unaimarika na wananchi wake wanapata maendeleo ikiwa ni pamoja na kuifanya Pemba kuwa ni sehemu maalum ya uwekezaji sambamba na kuiwekeza mazingira mazuri ya uwekezaji

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Balozi wa Switzerland nchini Tanzania Didier Chassot, ambapo katika mazungumzo yao viongozi hao wameahidi kuendeza ushirikiano uliopo hasa katika sekta ya afya ambapo nchi hiyo imeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sambamba na hayo, Balozi huyo wa Switzerland alieleza hatua ambazo itazichukua nchi yake katika kuiunga mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwajengea uwezo pamoja na mafunzo kwa vijana ili kukuza ubunifu na hatimae waweze kujiari wenyewe.

Balozi Chassot pia, alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma Switzerland ya kuiunga mkono Zanzibar kwa kusaidia wataalamu wa Bima ya Afya pamoja na kuiimarisha Taasisi ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ili kumpa nguvu Rais katika juhudi zake za kupambana na rushwa.

Rais Dk. Mwinyi kwa upande wake alimpongeza Balozi Chassot kwa azma ya serikali yake ya kuiunga mkono Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, kuwajengea uwezo vijana katika sekta ya ajira, kupambana na rushwa pamoja na kuwaendeleza akina mama mambo ambayo yote hayo yamepewa kipaumbele na Serikali anayoiongoza.

Sambamba na hayo, Rais Dk.Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba Wazanzibari kuwa kitu kimoja kwa kushirikiana katika Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa kutaendeleza umoja, amani, mshikamano sanjari na maendeleo endelevu kwa nchi na wananchi wake.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.